Zamalek yaiduwaza RS Berkane, ikibeba Kombe la Shirikisho Afrika
Muktasari:
- Pambano hilo la marudiano, lililopigwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, lilishuhudiwa vijana hao wa kocha Jose Gomes raia wa Ureno, wakibeba taji hilo kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni sare ya 2-2 baada ya awali Berkane kushinda 2-1 nyumbani wiki iliyopita.
BAO pekee lililofungwa dakika 23 na Ahmed Hamdi katika pambano la pili la fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, iliyopigwa usiku wa jana jijini Cairo, Misri iliiwezesha wenyeji, Zamalek kubeba ubingwa wa michuano hiyo kwa mara pili mbele ya RS Berkane ya Morocco kwa kuichapa bao 1-0.
Pambano hilo la marudiano, lililopigwa kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Cairo, lilishuhudiwa vijana hao wa kocha Jose Gomes raia wa Ureno, wakibeba taji hilo kwa kanuni ya faida ya bao la ugenini kwani matokeo ya jumla yalikuwa ni sare ya 2-2 baada ya awali Berkane kushinda 2-1 nyumbani wiki iliyopita.
Hii ni mara ya pili kwa Zamalek kuinyima Berkane taji, kwani msimu wa 2018-2019 zilikutana pia katika mechi za fainali, ambapo kila timu ilishinda nyumbani kwa bao 1-0 kabla ya mikwaju ya penalti kuamua bingwa na Wamisri waliokuwa nyumbani kama jana walishinda kwa 5-3.
Katika pambano la jana wenyeji, Zamalek walionyesha dhamira ya kupindua meza mapema mbele ya The Orange', baada ya kuanza kwa kasi na kutengeneza mashambulizi makali langoni mwa Wamorocco kabla ya Hamdi kufunga bao dakika ya 23 akimalizia pasi tamu ya Ahmed Sayed Zizo.
Kabla ya bao hilo, Zamalek ilifanya shambulizi kali na mabeki wa Berkane kufanikiwa kuokoa, lakini mmoja wa mabeki hao alifanya uzembe alipokuwa na mpira na kunyang'anywa na Ibrahim Ndiaye aliyemgongea Zizo aliyepiga pasi yenye macho iliyounganishwa wavuni na mfungaji.
Hata hivyo, mfungaji wa bao hilo, Hamdi hakumaliza kipindi hicho cha kwanza baada ya kuumia dakika ya 41 n kutolewa n nfasi yake kuchukuliwa na Youssef Obama.
Kipindi cha pili timu zote zilifanya mabadiliko ya wachezaji na kuongeza kasi ya mchezo huku, wageni wakionekana kucharuka zaidi wakisaka bao la kusawazisha, japo haikufanikiwa kutokana na Zamalek kutumia uzoefu kuwabana washambuliaji wa Berkane iliyomaliza ikiwa pungufu.
Beki Hamza El Moussaoui alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 90 kwa mchezo usio wa kiungwana kwa kumkanyanga mchezaji wa Zamalek na mwamuzi Issa Sy kutoka Senegal, kumzawadia kadi hiyo muda mchache baada ya kuongezwa kwa dakika saba za ziada.
Licha ya Berkane kupambana kwa dakika hizo za nyongeza ili ijikomboe, mambo yalikuwa magumu kwani filimbi ya mwisho iliyoashiria kumalizika kwa pambano hilo, ilijikuta ikilala 1-0 na kuwafanya wenyeji Zamalek kubeba ubingwa mbele ya maelfu ya mashabiki waliofurika kwenye Uwanja wa Cairo.
Hilo ni taji la kwanza kwa Kocha Gomes akiwa na Zamalek, lakini ni la pili kwa timu hiyo katika michuano ya Shirikisho, kwani ilishabeba mwaka 2019 kwa kuifunga pia RS Berkane, lakini hilo ni taji la 12 la CAF kwa Wamisri, baada ya kubeba Ligi ya Mabingwa mara tano, Kombe la Washindi mara moja na CAF Super Cup mara nne.
Matokeo ya mechi ya fainali ya msimu huu yanalingana ya yale ya msimu uliopita ambao Yanga ililikosa taji mbele ya USM Alger ya Algeria baada ya matokeo ya jumla kuwa sare ya 2-2.
Yanga ilipoteza awali nyumbani kwa mabao 2-1 kabla ya kushinda ugenini bao 1-0 lililofungwa kwa penalti na beki Djuma Shaban ambaye hayupo kwa sasa katika kikosi hicho huku Waalgeria wakibeba taji ikiwa chini ya Kocha Abdelhak Benchikha aliyeajiriwa na Simba baadae kabla ya kuikacha hivi karibuni kwa madai ya kuuguliwa na mkewe.
Katika michuano ya msimu huu, wachezaji watatu, Paul Basseme wa RS Berkane, Abdoulye Kanou wa USM Alger na Abdulaziz Issah wa Dreams ya Ghana waliibuka wafungaji bora kila mmoja akifunga jumla ya mabao manne.
Msimu uliopita Fiston Mayele aliyekuwa na Yanga, ndiye aliyeibuka Mfungaji Bora akifunga mabao saba.
Kwa sasa straika huyo anakipiga katika klabu ya Pyramids ya Misri iliyoishia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Jiji la Cairo, linatajiwa kushuhudia tena mechi ya fainali, wakati Al Ahly ya Misri ambao ni watetezi wa taji hilo itakapoikaribisha Esperance ya Tunisia katika mchezo wa marudiano baada ya wikiendi iliyopita kushindwa kutambiana na kutoka suluhu jijini Tunis.
Al Ahly inalisaka taji la 12 la michuano hiyo ya Afrika wakati, Esperance kama italibeba litakuwa ni la tano na hivyo kulingana na Zamelak na TP Mazembe ya DR Congo.
Mechi hiyo ta marudiano ya fainali ya Ligi ya Mabingwa itapigwa Jumamosi hii.