Yanga Princess inakwama hapa
Muktasari:
Timu hiyo imekuwepo kwenye Ligi Kuu ya Wanawake tangu msimu wa 2018/19, lakini hadi sasa haijabeba ubingwa wa ligi.
KAMA kuna eneo ambalo mashabiki wa Yanga SC wamekuwa wakisubiri kuona mabadiliko makubwa, basi ni upande wa timu yao ya wanawake, Yanga Princess.
Timu hiyo imekuwepo kwenye Ligi Kuu ya Wanawake tangu msimu wa 2018/19, lakini hadi sasa haijabeba ubingwa wa ligi.
Tangu ligi ianzishwe mwaka 2016 ni timu tatu tu ambazo zimebeba ubingwa wa ligi hiyo, Mlandizi Queens iliyokuwa mabingwa wa kwanza kabisa mwaka 2017, kisha JKT Queens iliyochukua mataji manne na Simba Queens yenye nayo matano.
Safari yake imekuwa ndefu kutoka kwenye kipindi ambacho ilionekana kuzidiwa sana na Simba Queens katika Kariakoo Dabi hadi sasa na imekuwa mshindani wa nafasi za juu.
MWENDELEZO
Tatizo la kwanza ni kutokuwa na mwendelezo wa kujenga kikosi cha ubingwa. Kila msimu Yanga Princess imekuwa ikifanya usajili, lakini kinachoonekana zaidi ni mabadiliko ya wachezaji badala ya kujenga msingi wa kikosi unaodumu kwa muda mrefu.
Timu ya ubingwa haihitaji tu majina mapya kila dirisha inahitaji kutambua maeneo dhaifu, kuyaimarisha na kuhakikisha wachezaji wanaounganishwa na kikosi wanaendana na mfumo wa muda mrefu.
Hapo ndipo Yanga inapaswa kujiuliza kama usajili wake unafanywa kwa mpango wa miaka kadhaa au kwa presha ya kutaka matokeo ya msimu mmoja.
VIPAJI
Yanga Princess inaonekana kuchelewa kwenye soko la vipaji. Badala ya kuwa timu inayowinda vipaji bora kabla havijawa majina makubwa, mara nyingi imekuwa ikihitaji wachezaji ambao tayari wamecheza muda mrefu sehemu nyingine.
Hata kwenye usajili wake, imekuwa ikiwachukua baadhi ya wachezaji kutoka kwa wapinzani wake, akiwamo Simba Queens. Hilo si tatizo lenyewe, lakini kama mkakati mkuu unakuwa kusubiri mchezaji ambaye tayari ametumika kwa muda kwa mpinzani, timu inaweza kukosa nafasi ya kujenga kizazi chake kipya cha wachezaji wenye njaa ya mafanikio.
ENEO LA UFUNDI
Yanga Princess haiwezi kushindania ubingwa kwa kutegemea uwezo wa wachezaji pekee. Inahitaji mfumo unaoanzia kwenye usajili, maandalizi ya msimu, uchambuzi wa wapinzani, maendeleo ya mchezaji mmoja mmoja hadi namna timu inavyocheza mechi kubwa.
Hili ni eneo ambalo linahitaji wataalamu wanaolijua soka la wanawake kwa undani. TFF yenyewe inaonyesha ukubwa wa msingi wa vipaji vya Yanga Princess kwa kuwa wachezaji wake kadhaa waliitwa kwenye kikosi cha Twiga Stars kwa WAFCON 2026, akiwamo Ester Mabanza, Diana Mnaly na Fatuma Aron.
Timu hiyo mara nyingi imekuwa ikifanya vizuri kwenye mechi nyingine lakini haina mpango maalumu inapokwenda kukutana na timu kubwa zinazowania ubingwa.
Mfano mzuri msimu uliopita, Yanga ilipoteza mechi mbili dhidi ya Simba ambao walikuwa wanawania nafasi ya ubingwa, ikachukua pointi nne kwa JKT ambayo ilionekana kuwa mbali kidogo na taji hilo.
KARIAKOO DABI
Mashabiki wanaweza kusamehe kupoteza pointi dhidi ya timu nyingine mara moja moja, lakini kushindwa tena mbele ya mpinzani mkuu kunauma zaidi.
Mfano, Novemba 2024 Simba Queens iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Yanga Princess. Tatizo hapa si matokeo ya mechi moja ni ujumbe unaojengwa kila msimu kwamba Yanga bado haijawa bora kuliko Simba katika vita ambayo mashabiki wake wanaipa uzito mkubwa.
Hivyo ni ngumu kuifananisha Yanga dhidi ya Simba ambayo tayari imejitengenezea ufalme wake kwenye soka la wanawake na ina uzoefu mkubwa kuanzia kwenye matokeo uwanjani, usajili na uzoefu wa kimataifa.
Tangu mwaka 2019, timu hizo zimekutana mara 19 kwenye mashindano mbalimbali ikiwemo Ngao ya Jamii, Simba ikiibuka na ushindi mara 13. Yanga ikishinda mara tatu, huku mechi tatu zikitoka sare.
Lakini kwenye ligi timu hizo zimekutana mara 15, Simba ikishinda mara 11, sare mbili na kupoteza mechi mbili huku Yanga ikishinda mechi mbili, sare mbili na kupoteza 11.
AHADI ZA VIONGOZI
Kila msimu kunakuwa na matarajio makubwa, lakini mwishowe mashabiki wanataka kuona kombe. Msimu wa 2025/26 Yanga Princess ilikuwa ikifuatilia Simba Queens katika mbio za ubingwa, lakini Simba hatimaye ilimaliza juu kwa pointi 57 na kutwaa taji.
Hapo ndipo Yanga inapaswa kuacha kuangalia nafasi ya pili au tatu kama mafanikio ya mwisho na kuanza kuuliza ni kitu gani kinakosekana ili kutatua changamoto hiyo na kumaliza kiu ya mashabiki zao ya takribani misimu nane bila kugusa kombe.
Timu hiyo inapaswa kufanya tathmini ya kutosha kama ni kweli inataka kubadilika na kuwapa furaha mashabiki wake.Iangalie eneo lipi linapaswa kurekebishwa kama ni kuongeza wataalamu au makocha wenye uzoefu na ligi ya wanawake ili wawe msaada kwa timu.
Timu hiyo ina kila kitu Yanga ina jina, ina mashabiki wa kuhudhuria mechi zao na uwezo wa kifedha wa kujenga timu unao kinachotakiwa sasa ni mpango sahihi, utekelezaji na uwajibikaji.
MSIKIE MRATIBU
Mratibu wa timu hiyo, Kibwana Matokeo anasema timu hiyo itafanya maboresho machache msimu huu kutokana na tayari imetengeneza timu yenye ushindani.
"Tumekuwa na tathmini ya timu na kuna baadhi ya maeneo tutarekebisha kuelekea msimu mpya hatutabomoa timu yote lakini tubaboresha baadhi ya maeneo tu," alisema Matokeo.