England, Wales zamgeuka Infantino mbio za urais FIFA
Muktasari:
- Wales ilikuwa taifa la kwanza kutangaza hadharani kutomuunga mkono Infantino, kabla ya England nayo kufuata nyayo hizo kwa kumwandikia barua rasmi rais huyo wa FIFA na kumjulisha kuwa hana tena uungwaji mkono wao.
Chama cha Soka cha England (FA) kimeungana na Shirikisho la Soka la Wales kupinga azma ya Gianni Infantino ya kugombea tena urais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).
Wales ilikuwa taifa la kwanza kutangaza hadharani kutomuunga mkono Infantino, kabla ya England nayo kufuata nyayo hizo kwa kumwandikia barua rasmi rais huyo wa FIFA na kumjulisha kuwa hana tena uungwaji mkono wao.
Hatua hiyo ni pigo kubwa kwa Infantino, ambaye kwa sasa anakabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu mustakabali wa uongozi wake ndani ya FIFA.
Kupoteza sapoti ya mataifa mawili yenye ushawishi mkubwa katika soka la dunia kunaashiria kuongezeka kwa upinzani dhidi ya uongozi wa Infantino, huku kukiwa na dalili kwamba mataifa mengine yanaweza kufuata mkondo huo.
Iwapo wimbi hilo litaendelea kuongezeka, linaweza kubadili mwelekeo wa uchaguzi ujao wa urais wa FIFA na kuweka hatarini nafasi ya Infantino kuendelea kuiongoza taasisi hiyo ya soka duniani.
Kwa sasa, macho ya wadau wa soka duniani yanaelekezwa kwa mataifa mengine wanachama wa FIFA ili kuona kama yataendelea kumuunga mkono Infantino au yatajiunga na England na Wales katika kumpinga.