Prime
Straika Mkongomani ajadiliwa Simba
WAKATI zikisalia takribani wiki mbili kabla ya dirisha la usajili kuelekea msimu wa 2026-2027 kufungwa, inaelezwa mabosi wa Simba SC wameamua kuingia sokoni wakifanya mchakato wa kumnasa mshambuliaji raia wa DR Congo, Glody Kilangalanga.
Taarifa za ndani kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza, nyota huyo ambaye msimu wa 2025-2026 ameitumikia Al-Washm ya Saudi Arabia, yupo kwenye mazungumzo ya mwisho na mabosi wa Simba.
“Bado tunaendelea kuimarisha kikosi chetu na maeneo ambayo tunahitaji kuyaboresha zaidi ni eneo la ushambuliaji,” kilisema chanzo.
Kilangalanga si jina geni katika ramani ya soka la Afrika. Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 26, alizaliwa Agosti 8, 1999, nchini DR Congo.
Safari yake ya soka imepitia katika klabu mbalimbali kubwa, akianzia AS Maniema Union ya nchini kwao kati ya mwaka 2018 na 2020, ambako alijitengenezea jina kabla ya kutimkia nchini Tunisia.
Baada ya kuondoka Maniema Union, Kilangalanga alicheza nchini Tunisia katika kikosi cha CS Chebba na baadaye kwa mkopo katika klabu ya Olympique Béja, ambako alisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Tunisia (Tunisian Cup). Pia alipata uzoefu Algeria akiwa na JS Kabylie kabla ya kuelekea Saudi Arabia ambako amepita timu za Bisha FC, Wej SC na Al-Washm.
“Matumaini yetu ni kwamba kabla ya dirisha la usajili kufungwa, tutakuwa tumeboresha kikosi tayari kwa kuanza kupambania malengo ya msimu ujao,” alibainisha bosi mmoja wa Simba.
Kilangalanga anasifika kwa kuwa na kasi, uwezo wa kucheza nafasi nyingi za ushambuliaji ambazo ni winga wa kulia na mshambuliaji wa kati, huku akitumia zaidi mguu wa kushoto.
Uamuzi wa Simba kumuhitaji Kilangalanga unakuja ikiwa ni siku chache tangu klabu hiyo imtambulishe mshambuliaji raia wa Mali, Ibrahim Doumbia.
Doumbia, 22, amejiunga na Simba akitokea AS Korofina ya Mali akiwa na rekodi nzuri ya ufungaji.
Katika msimu uliopita wa 2025-2026 nchini Mali, Doumbia alimaliza akiwa mfungaji bora wa Ligi Kuu akipachika mabao 17 katika mechi 24, huku akiwa na jumla ya mabao 21 katika mashindano yote.
Wakati suala la Kilangalanga likiendelea kujadiliwa, bado Simba inapambana kuhakikisha inamchukua tena Selemani Mwalimu, kwa mkopo kutoka Wydad Casablanca ya Morocco.
Mwalimu ambaye alikuwa Simba kwa mkopo wa msimu mmoja 2025-2026, amerejea Wydad baada ya muda wake kumalizika, huku kukiwa na mazungumzo ya kumchukua tena kufuatia awali klabu hiyo kutangaza kuendelea naye, kabla ya Wydad kuibuka na kusema hakuna makubaliano hayo.
Hata hivyo, mazungumzo hayo yanadaiwa kuanza upya kutokana na mabadiliko ya uongozi ndani ya klabu ya Wydad Casablanca, jambo ambalo Meneja wa Habari wa Simba, Ahmed Ally, amethibitisha uongozi unapambana kulimaliza mapema.
Simba katika kuboresha kikosi chake kuelekea msimu ujao wa 2026-2027, tayari imewatambulisha wachezaji wapya sita na watatu wa kigeni ni Doumbia, Ibraheem Jabaar na Keletso Makgalwa. Wazawa ni Kelvin Nashon, Bakari Msimu na Nathaniel Chilambo.
Katika ushambuliaji, kuondoka kwa Mwalimu na Jonathan Sowah aliyerejea Singida Black Stars, kunaifanya Simba kubaki na Doumbia ambaye ni usajili mpya.
Mwingine ni Baraka Mwangosi ambaye alitua Simba dirisha dogo la Januari 2026, huku akiwa bado hajapewa nafasi kubwa ya kucheza hali inayoifanya klabu hiyo kuhitaji kuimarisha zaidi eneo hilo.