Xavi apewa mikoba Uholanzi
Muktasari:
- Xavi, mwenye umri wa miaka 46, anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka minne wa kuinoa timu hiyo maarufu kwa jina la Oranje, ikiwa ni mara yake ya kwanza kurejea kwenye benchi la ufundi tangu kuachana na Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2023/24.
AMSTERDAM, UHOLANZI. Gwiji wa zamani wa Barcelona, Xavi Hernandez, amekubali kurejea kwenye ukocha baada ya kufikia makubaliano ya kuwa kocha mpya wa timu ya taifa ya Uholanzi.
Xavi, mwenye umri wa miaka 46, anatarajiwa kusaini mkataba wa miaka minne wa kuinoa timu hiyo maarufu kwa jina la Oranje, ikiwa ni mara yake ya kwanza kurejea kwenye benchi la ufundi tangu kuachana na Barcelona mwishoni mwa msimu wa 2023/24.
Shirikisho la Soka la Uholanzi lilitangaza ujio huo kupitia akaunti yake rasmi ya X kwa ujumbe uliosomeka: “Kwa fahari tunamtambulisha kocha wetu mpya. Karibu, Xavi Hernandez!”
Kwa mujibu wa mwandishi mashuhuri wa habari za usajili, Fabrizio Romano, Xavi amesaini makubaliano ya kuwa kocha mpya wa Uholanzi.
Kocha huyo ambaye aliwahi kutwaa Kombe la Dunia akiwa mchezaji, sasa anatarajiwa kurejea kwenye soka la kimataifa akiwa na Uholanzi, timu ambayo imewahi kufika fainali ya Kombe la Dunia mara tatu.
Shirikisho la Soka la Uholanzi limekuwa likitafuta kocha mpya tangu Ronald Koeman kujiuzulu kufuatia timu hiyo kutolewa kwenye Kombe la Dunia na Morocco.
Roberto Martinez alikuwa miongoni mwa makocha waliokuwa wakipewa nafasi kubwa ya kuchukua nafasi hiyo baada ya kuachana na timu ya taifa ya Ureno kufuatia kampeni yao iliyokatisha tamaa kwenye Kombe la Dunia.
Martinez, aliyewahi kuinoa Everton, alifanyiwa mahojiano kwa ajili ya nafasi hiyo, lakini kwa mujibu wa talkSPORT, amepitwa na Xavi ambaye sasa ndiye anayetarajiwa kupewa jukumu hilo.
Kazi kubwa ya Xavi itakuwa kuiongoza Uholanzi kuelekea Euro 2028, huku Ligi ya Mataifa ya Ulaya ikiwa mtihani wake wa kwanza wa ushindani mwezi ujao.
Xavi anakumbukwa kwa kuisaidia Hispania kuifunga Uholanzi kwa bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Dunia mwaka 2010 mjini Johannesburg, wakati wa enzi zake za uchezaji.
Baada ya kustaafu soka la kucheza, Xavi alianza safari yake ya ukocha katika klabu ya Al-Sadd ya Qatar kabla ya kurejea Barcelona mwaka 2021.
Akiwa Barcelona, alifanikiwa kutwaa ubingwa wa LaLiga pamoja na Kombe la Super Cup la Hispania.
Uteuzi wake pia utamfanya kuwa kocha wa kwanza wa kigeni kuinoa timu ya taifa ya wanaume ya Uholanzi katika kipindi cha miaka 48, tangu Mwaustria Ernst Happel aliposhika nafasi hiyo mwishoni mwa miaka ya 1970.