Prime
'MACHO KWENYE SKRINII'
AZAM imegoma kukaa mezani na mabosi wa Yanga ambao wanawania saini ya kiungo wao, Feisal Salum ‘Fei Toto’ ambaye pia anawaniwa na Simba kwenye dirisha hili la usajili linalotarajiwa kufungwa Agosti 15, 2026.
Yanga imepiga simu moja kwa moja kwa mabosi wa Azam wakitaka kukaa nao chini kumaliza dili hilo, lakini vigogo wa matajiri wa Chamazi wakadai hawapo nchini kwa safari za kikazi.
YANGA IMEKUWAJE
Yanga ilishakubaliana na Fei Toto ikitaka kumpa kiasi cha Sh3 bilioni ikiwa ni ada yake ya kusaini mkataba, dau ambalo lilishakubaliwa na kiungo wao huyo wa zamani.
Hata hivyo, Fei Toto bado ana mkataba na Azam FC wa mwaka mmoja ambapo Yanga ililazimika kukaa chini na matajiri hao wa Chamazi lakini wakaingia mitini.
DAU LA KUVUNJA MKATABA
Kama Fei Toto angetaka kuondoka kwa njia ambayo akitumia kuondoka Yanga kwa kununua mkataba wake Azam iliweka kipengele cha Dola 1.5 milioni (Sh4 bilioni) kununua mkataba huo.
Yanga ambayo ilimuuza Fei Toto kwa si zaidi ya Sh250 milioni mwishoni mwa msimu wa 2022-2023 baada ya kuwepo mvutano mkubwa, hakutaka kutumia kiasi hicho kununua mkataba huo, ikitaka kukaa mezani na wenzao wa Azam kisha kukubaliana.
SIMBA NAO WAMO
Simba nayo ilikuwa inataka kumnunua Fei Toto lakini ikakwama kukaa mezani na matajiri hao wa Chamazi kutokana na tofauti za kibiashara na mabosi wa Wekundu hao.
Simba iliishia kukubaliana na Fei Toto pekee ikitaka kumpa kiasi cha Sh2.8 bilioni kama dau la kusaini lakini bado ikatakiwa kumalizana na matajiri hao wa Chamazi.
Timu ambayo ingekuwa inataka kumsajili Fei Toto ilitakiwa kuwa na kiasi cha Sh7 bilioni ikiwemo ni dau la usajili la kiungo huyo Sh3 bilioni na zile Sh4 bilioni za kuvunja mkataba wake, mfupa mgumu ukibaki hapo kwa Simba na Yanga.
YANGA INGEVUNA HIKI
Kama Azam ingefanikiwa kukaa mezani na Simba, kisha kukubaliana kuuziana mchezaji huyo basi Yanga ingevuna kiasi cha Sh1 bilioni kutokana na makubaliano ya klabu hizo mbili, wakati wakiuziana Fei Toto misimu mitatu iliyopita.
Maana yake Azam ilitakiwa kuweka fedha ndefu zaidi ili kuhakikisha inafanya biashara ya faida kisha kuwalipa Yanga chao kulingana na makubaliano ya klabu hizo mbili.
FEI AFICHWA ARUSHA
Azam katika kuzikomoa Simba na Yanga, ikaweka mitego miwili, kwanza ikamuwekea ulinzi mkali kiungo huyo kwenye kila hatua kuhakikisha hayatokei makosa kama ambayo yalitokea kwa aliyekuwa mshambuliaji Seleman Mwalimu ambaye alifanya mazoezi na Simba jioni ya Agosti 10, 2026, kisha Agosti 11, 2026, akatua Yanga.
Azam mbali na kumuwekea ulinzi huo Fei Toto, ikabadili akili ambapo baada ya kuvunja kambi yake ya maandalizi ya msimu mpya pale nchini Rwanda, jana ikaelekea moja kwa moja jijini Arusha ambako Jumamosi Agosti 15, 2026 siku ambayo dirisha la usajili linafungwa, itacheza mchezo wake wa kwanza wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Polisi Tanzania.
Hesabu hizo za Azam ni kumuweka mbali Fei Toto na ukaribu na mabosi wa Simba na Yanga endapo wangekuja moja kwa moja jijini Dar es Salaam ingeongeza presha kwa kiungo huyo.
MSIKIE BOSI AZAM
Akizungumzia hatua ya usajili huo wa Fei Toto, Rais wa Azam, Nassoro Idrissa ‘Father’ ameliambia Mwanaspoti kuwa, hawana mpango wa kumuuza mchezaji yeyote kwasasa ambaye yupo kwenye kikosi hicho.
“Kama unavyofahamu, tuna malengo yetu, wachezaji ambao tumeachana nao tulishamaliza kuwatangaza, hawa ambao wamesalia hakuna ambaye tunataka kumuachia au kumuuza, na hatujapokea ofa yoyote kutoka klabu yoyote.”