Hispania kutegua mtego wa miaka 15?
Muktasari:
- Ni mwaka huo nchini Afrika Kusini ambapo La Roja iliandika historia kwa kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo, ikiongozwa na kizazi cha dhahabu kilichoundwa na nyota kama Iker Casillas, Xavi Hernández, Andrés Iniesta, Xabi Alonso, David Villa, Sergio Ramos na Fernando Torres.
HISPANIA inapowania kutwaa taji lake la pili la Kombe la Dunia, kumbukumbu za safari yake ya kihistoria ya mwaka 2010 zinaendelea kubaki kwenye vitabu vya historia kama moja ya mafanikio makubwa zaidi katika soka la dunia.
Ni mwaka huo nchini Afrika Kusini ambapo La Roja iliandika historia kwa kutwaa Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo, ikiongozwa na kizazi cha dhahabu kilichoundwa na nyota kama Iker Casillas, Xavi Hernández, Andrés Iniesta, Xabi Alonso, David Villa, Sergio Ramos na Fernando Torres.
Hispania ilimaliza mashindano hayo kwa rekodi ya kuvutia baada ya kushinda mechi sita mfululizo, huku ikiruhusu mabao mawili pekee katika mechi saba na kutunza mechi tano bila kufungwa (clean sheets). Mafanikio hayo yaliifanya kuwa nchi ya nane kutwaa Kombe la Dunia na hadi sasa ndiyo bingwa wa hivi karibuni kuingia kwenye orodha ya mataifa yaliyowahi kushinda taji hilo.
Safari ya Hispania ilianza kwa mshtuko baada ya kupoteza mchezo wake wa kwanza wa Kundi H kwa bao 1-0 dhidi ya Uswisi, Gelson Fernandes akifunga bao pekee la mchezo dakika ya 52. Hata hivyo, kipigo hicho hakikuyumbisha kikosi hicho cha Vicente del Bosque.
Katika mchezo uliofuata, Hispania iliifunga Honduras mabao 2-0, huku David Villa akifunga mabao yote mawili. Ushindi huo uliwarejesha kwenye mbio za kufuzu hatua ya mtoano.
Baadaye walihitimisha hatua ya makundi kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Chile. Villa alifungua ukurasa wa mabao kabla ya Andrés Iniesta kuongeza la pili, ushindi uliowapeleka kileleni mwa kundi.
Hatua ya 16 bora iliwakutanisha na majirani zao, Ureno, ambapo Villa aliendelea kung’ara kwa kufunga bao pekee lililoipa Hispania ushindi wa 1-0 na tiketi ya robo fainali.
Katika robo fainali dhidi ya Paraguay, Hispania ilipata ushindi mwingine wa bao moja baada ya Villa kufunga dakika ya 85, na kuipeleka timu hiyo nusu fainali kwa mara ya kwanza katika historia yake ya Kombe la Dunia.
Nusu fainali iliwakutanisha na Ujerumani, timu iliyokuwa ikipewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa. Hata hivyo, beki Carles Puyol aliifungia Hispania bao la ushindi kwa kichwa akimalizia mpira wa kona, na kuipeleka kwenye fainali yake ya kwanza kabisa ya Kombe la Dunia.
Fainali dhidi ya Uholanzi iliyochezwa Julai 11, 2010, kwenye Uwanja wa Soccer City jijini Johannesburg, ilibaki kuwa moja ya mechi zenye ushindani mkubwa katika historia ya Kombe la Dunia.
Dakika 90 zilimalizika kwa sare ya bila kufungana huku timu zote zikishindwa kutumia nafasi zilizopatikana. Mchezo huo uliingia kwenye historia pia kwa kutolewa kwa kadi 14 za njano, ambapo Uholanzi ilionyeshwa kadi nane, jambo lililoonyesha ugumu na ukali wa pambano hilo.
Dakika ya 109, beki wa Uholanzi, John Heitinga alitolewa nje kwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi ya pili ya njano, na kuwaacha wenzake wakicheza pungufu kwa dakika zilizobaki.
Faida hiyo iliitumia vyema Hispania pale Andrés Iniesta alipofunga bao la pekee dakika ya 116 baada ya kupokea pasi safi ndani ya eneo la hatari na kuipatia nchi yake ushindi wa 1-0 uliotangaza mwanzo wa enzi mpya katika soka la Hispania.
Katika fainali hiyo, Hispania ilitawala mchezo kwa kumiliki asilimia 57 ya mpira na kupiga mashuti 19 dhidi ya 13 ya Uholanzi. Kipa Iker Casillas pia alikuwa mhimili muhimu kwa kuokoa nafasi kadhaa za wazi na kumaliza mashindano akiwa ameruhusu mabao mawili pekee katika mechi saba.
Kwa upande wa washambuliaji, David Villa alikuwa nyota wa Hispania katika mashindano hayo baada ya kufunga mabao matano kati ya mabao manane yaliyofungwa na timu hiyo, huku matatu kati ya hayo yakiiwezesha timu kushinda mechi muhimu za hatua ya mtoano.
Zaidi ya miaka 15 baadaye, ushindi huo wa mwaka 2010 bado unabaki kuwa mafanikio makubwa zaidi katika historia ya soka la Hispania, huku kizazi hicho cha Casillas, Xavi, Iniesta na Villa kikitajwa kuwa miongoni mwa vikosi bora kuwahi kutwaa Kombe la Dunia.
Jumapili hii, kikosi hicho kikiwa na kizazi kipya, kinaingia uwanjani pale Marekani kucheza fainali ya Kombe la Dunia 2026 dhidi ya bingwa mtetezi, Argentina, hali itakuwaje? Tusubiri kama Hispania itategua mtego wa kubeba ubingwa wa dunia baada ya miaka 15.