Winga Chelsea ashinda kesi, kurudi dimbani
Muktasari:
- Mudryk mwenye umri wa miaka 25 hajacheza mechi yoyote ya mashindano tangu Novemba 2024 baada ya vipimo kuonyesha alikuwa na kiwango cha dawa iliyokatazwa ya meldonium mwilini.
RENNES, UFARANSA: WINGA wa Chelsea, Mykhailo Mudryk ameruhusiwa kurejea mara moja kucheza soka baada ya Mahakama ya Usuluhishi wa Michezo (CAS) kukubali kwa sehemu rufaa yake dhidi ya adhabu ya miaka minne aliyokuwa amepewa kutokana na matumizi ya dawa zilizopigwa marufuku.
Mudryk mwenye umri wa miaka 25 hajacheza mechi yoyote ya mashindano tangu Novemba 2024 baada ya vipimo kuonyesha alikuwa na kiwango cha dawa iliyokatazwa ya meldonium mwilini.
Baada ya kusimamishwa kwa muda na Chama cha Soka cha England (FA), baadaye alipewa adhabu ya miaka minne, lakini aliikatia rufaa katika Mahakama ya CAS.
Sasa CAS imeamua kuwa Mudryk anaweza kurejea uwanjani mara moja, baada ya kukubali kuwa alikiuka kanuni za matumizi ya dawa zilizokatazwa na kufikia makubaliano ya adhabu ambayo inahesabiwa tayari ameimaliza kutokana na muda aliokuwa nje ya mchezo.
Mahakama hiyo ilieleza kuwa kipimo chake kilionyesha kiwango kidogo sana cha dawa hiyo iliyokatazwa. Pia ilibainisha tangu wakati huo, Wakala wa Dunia wa Kupambana na Matumizi ya Dawa Haramu Michezoni (Wada) umefanya maboresho kwenye miongozo ya kiufundi ya upimaji wa meldonium, dawa inayotumika kutibu matatizo ya mfumo wa moyo na mzunguko wa damu.
Katika taarifa yake, Chelsea ilisema: “Tangu mwanzo huu umekuwa kipindi kigumu sana kwa Misha, kitaaluma na binafsi. Tunafurahia suala hili sasa limefikia tamati na linamruhusu kurejea kucheza soka mara moja.”
Chelsea iliongeza imeendelea kumuunga mkono Mudryk katika mchakato wote huku ikiheshimu mfumo wa kupambana na matumizi ya dawa zilizokatazwa pamoja na taratibu za kisheria.
Klabu hiyo pia ilikaribisha utambuzi kwamba maendeleo ya kisayansi katika viwango vya upimaji yameongeza usahihi wa matokeo, na kwamba kama sampuli ya Mudryk ingechunguzwa kwa kutumia viwango vya sasa, isingetangazwa kuwa na matokeo chanya wala asingepatikana na kosa la kukiuka kanuni za matumizi ya dawa zilizokatazwa.
Chelsea ilisisitiza Mudryk amekuwa akisisitiza mara zote hakuwahi kutumia kwa makusudi dawa yoyote iliyopigwa marufuku na hajui namna mabaki ya dawa hiyo yalivyoingia mwilini mwake.
“Katika kipindi chote cha mchakato huu ameendelea kuwa mtaalamu na mwenye uvumilivu, licha ya kupitia moja ya nyakati ngumu zaidi katika maisha yake ya soka,” ilieleza klabu hiyo.
Mudryk sasa anatarajiwa kujiunga na kikosi cha Chelsea kinachojiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu England. Chelsea, inayonolewa na Xabi Alonso, inatarajiwa kucheza mechi ya kirafiki dhidi ya Tottenham Hotspur Jumamosi.
Mataifa wa Ukraine mwenye mechi 28 za kimataifa alijiunga na Chelsea akitokea Shakhtar Donetsk mwaka 2023 kwa ada ya Pauni 62 milioni, akisaini mkataba wa miaka minane na nusu.
Kwa upande wake, Mudryk alisema kipindi cha kusimamishwa kwake ndicho kilikuwa kigumu zaidi katika maisha yake ya soka.
Katika ukurasa wake wa Instagram aliandika: “Baada ya mapambano marefu, adhabu ya miaka minne niliyokuwa nimepewa imefutwa na sasa nina uhuru wa kuendelea na maisha yangu ya soka mara moja.”
Aliongeza: “Ninashukuru mchakato huu umefikia mwisho, nimeruhusiwa kurejea uwanjani na sasa ninaweza kuangalia mbele kuelekea mustakabali wangu. Hiki kimekuwa kipindi kigumu zaidi katika maisha yangu ya soka.”