Prime
Hii hapa sababu Mpanzu kutokwenda Rwanda
KIUNGO wa Simba, Elie Mpanzu hatakuwa sehemu ya kambi ya maandalizi ya timu hiyo nchini Rwanda baada ya kushindikana kusafiri kutokana na utaratibu ambao umekwekwa kwa watu wanaotoka Jamhuri ya Kidemokrasia Congo kutoka na uwepo wa ugonjwa wa Ebola.
Kutokana na mlipuko wa ugonjwa huo nchini DR Congo kumekuwa na sheria kali ambazo zinawazuia watu kutoka nchini humo kwenda nchini nyingine.
Awali kulikuwa na jitihada kubwa zilizofanywa kuhakikisha kiungo huyo anajiunga na wenzake waliokwenda Rwanda kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya, lakini mipango hiyo imegonga mwamba baada ya kushindikana kukamilika kwa taratibu za usafiri haraka.
Kutokana na hali hiyo, uamuzi wa mwisho uliotolewa na uongozi wa Simba ni kwamba Mpanzu ataendelea kubaki jijini Dar es Salaam, ambako atafanya mazoezi maalumu chini ya programu iliyoandaliwa na benchi la ufundi akisubiri wenzake warejee kutoka kambini.
Ofisa wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema mchezaji huyo alishindwa kuingia Rwanda moja kwa moja akitokea DR Congo kutokana na masharti ya uhamiaji yaliyopo kwa sasa ambapo anatakiwa kukaa kizuizini kwa siku 14 au zaidi.
“Mpanzu ameshindwa kwenda Rwanda moja kwa moja kutokea Kongo kutokana na mambo ya kisheria. Kwa sasa mtu anayetokea huko anatakiwa kwanza akae siku 14 katika nchi nyingine ndipo aruhusiwe kuingia Rwanda,” amesema Ahmed Ally.
Amesema klabu ilifanya kila juhudi kuhakikisha mchezaji huyo anasafiri na kujiunga na kikosi, lakini mazingira yaliyokuwepo hayakuruhusu jambo hilo kutekelezeka.
Ahmed Ally aliwataka mashabiki kutokuwa na wasiwasi kuhusu kutokuwepo kwa Mpanzu kambini, akieleza kuwa hali hiyo haijatokana na uzembe wa mchezaji huyo wala uamuzi wa klabu.
“Sijui kama mashabiki wanamsema Mpanzu mitandaoni, ingawa ni kweli amekuwa na bahati mbaya hasa katika kipindi hiki cha maandalizi. Labda wao wanadhani kukosekana kwake ni kwa makusudi, lakini sivyo ilivyo,” amesema.
Alifafanua kuwa Mpanzu tayari yupo Dar es Salaam baada ya kushindwa kuendelea na safari yake na sasa ataendelea na mazoezi binafsi kwa kufuata programu ya benchi la ufundi hadi kikosi kitakaporejea kutoka Rwanda.
“Mpanzu yuko Dar es Salaam. Alirudishwa akiwa uwanja wa ndege na sasa atawasubiri wenzake warejee kutoka Rwanda ili aungane nao kwa siku zitakazokuwa zimesalia kabla ya msimu mpya kuanza,” alisisitiza Ahmed Ally.
Hii sio mara ya kwanza kwa Mpanzu kutoshiriki ‘pre season’ kwani kukosekana kwake kambini ni pigo kwa benchi la ufundi la Simba ambalo lilikuwa linatarajia kumtumia katika mechi za Kagame ambayo sio tu mashindano bali maandalizi ya msimu ujao, lakini uongozi unaamini ataendelea kuwa katika kiwango kizuri kupitia programu maalumu ya mazoezi atakayoifanya nchini hadi atakapoungana tena na wenzake.