Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wembanyama sasa kutamba na viatu vya Nike sokoni

Muktasari:

  • Makubaliano hayo yanamaanisha mchezaji huyo sasa atakuwa na viatu vyake maalumu vinavyobeba jina lake (signature shoe line), hatua ambayo ni heshima kubwa kwa mchezaji yeyote wa NBA na ishara ya hadhi yake inayoendelea kupanda ndani na nje ya uwanja.

SAN ANTONIO, MAREKANI: NYOTA wa kimataifa wa mpira wa kikapu kutoka Ufaransa, Victor Wembanyama ameandika historia nyingine kubwa katika maisha yake ya mchezo huo baada ya kufikia makubaliano ya mkataba mpya wa muda mrefu na kampuni kubwa ya kutengeneza vifaa vya michezo duniani, Nike.

Makubaliano hayo yanamaanisha mchezaji huyo sasa atakuwa na viatu vyake maalumu vinavyobeba jina lake (signature shoe line), hatua ambayo ni heshima kubwa kwa mchezaji yeyote wa NBA na ishara ya hadhi yake inayoendelea kupanda ndani na nje ya uwanja.

Kwa mujibu wa vyanzo vilivyolinukuu ESPN kupitia mwandishi Shams Charania, mkataba huo ni wa muda mrefu, ingawa thamani yake na masharti mengine ya kifedha bado hayajawekwa wazi.

Habari hizo zimeibuka wakati mkataba wa awali wa Wembanyama na Nike ulikuwa unatarajiwa kumalizika mwezi Oktoba mwaka huu.

Makubaliano hayo mapya yanakuja wiki chache baada ya Wembanyama kusaini mkataba mwingine mkubwa wa miaka mitano wenye thamani ya Dola 252 milioni na klabu yake ya San Antonio Spurs, ambao ndiyo kiwango cha juu kabisa alichostahili kupata kama nyota aliyemaliza kipindi chake cha mkataba wa awali (rookie-scale extension).

Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 alipata fursa ya kuanza kufanya mazungumzo ya kuongeza mkataba na Spurs mara tu baada ya timu hiyo kutolewa kwenye Fainali za NBA kutokana na kupoteza mfululizo wa michezo dhidi ya New York Knicks kwa ushindi wa michezo 4-1.

Mbali na mafanikio yake ya NBA, Wembanyama ameendelea kuwa sura inayovutia kampuni kubwa duniani. Tangu mwaka 2024 amekuwa balozi wa kampuni maarufu ya mavazi ya kifahari ya Ufaransa, Louis Vuitton, jambo linaloonyesha namna umaarufu wake ulivyozidi kuvuka mipaka ya mchezo wa mpira wa kikapu na kuingia kwenye ulimwengu wa mitindo na biashara.

Katika kipindi kifupi tangu ajiunge na NBA, Wembanyama ameendelea kuvunja rekodi mbalimbali. Alikuwa mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuwahi kutwaa tuzo ya Mchezaji Bora wa Kujihami wa Mwaka (Defensive Player of the Year), huku pia akiwa wa kwanza kushinda tuzo hiyo kwa kura zote za wapigakura.

Msimu uliopita aliiongoza NBA kwa kuzuia mashuti ya wapinzani (blocks), jambo lililomwezesha kuchaguliwa katika Kikosi Bora cha Mwaka cha NBA (All-NBA First Team). Aidha, aliteuliwa kwa mara ya pili kushiriki mchezo wa NBA All-Star, lakini safari hii akiwa miongoni mwa wachezaji walioanza kikosini.

Kwa mafanikio hayo, Wembanyama aliingia kwenye historia ya San Antonio Spurs kwa kuwa mchezaji wa sita pekee wa klabu hiyo kuchaguliwa kuanza katika mchezo wa All-Star. Aliungana na majina makubwa yaliyowahi kuitumikia Spurs kama George Gervin, Alvin Robertson, David Robinson, Tim Duncan na Kawhi Leonard.

Katika msimu wa 2025/26, ambao ulikuwa wa tatu kwake kucheza NBA, Wembanyama alicheza jumla ya michezo 64 na kuweka rekodi mpya binafsi katika karibu kila eneo muhimu. Alimaliza akiwa na wastani wa pointi 25.0 kwa kila mchezo, rebaundi 11.5 na asisti 3.1.

Pia aliiongoza ligi kwa wastani wa blocks 3.08 kwa mchezo na kuongeza wastani wa steals 1.03, takwimu zilizomfanya amalize msimu akiwa mchezaji wa saba tu katika historia ya NBA kufikisha wastani wa angalau pointi 25, rebaundi 10 na blocks tatu katika msimu mmoja.

Ubora wake ulionekana pia kwenye uthabiti wake wa takwimu. Katika michezo 42 alikusanya rebaundi 10 au zaidi, akarekodi double-double 42 na kuongeza triple-double moja, takwimu zinazoonyesha uwezo wake wa kufanya makubwa katika pande zote mbili za uwanja.

Kupata viatu vyake maalumu kutoka Nike ni hatua inayofikiwa na idadi ndogo ya wachezaji wa NBA na huashiria kuwa kampuni hiyo ina imani kubwa na uwezo wa mchezaji huyo, pamoja na nguvu yake katika soko la kimataifa. Viatu hivyo vinatarajiwa kuzinduliwa katika kipindi kijacho na vinaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa Nike wa kumjenga Wembanyama kama mmoja wa nyota wakubwa wa kizazi kipya cha mchezo wa mpira wa kikapu duniani.