Inter sasa yatua kwa Jones
Muktasari:
- Kupitia kwa wawakilishi, Inter waliwasilisha nia yao ya kufanya usajili huo, lakini Liverpool wamesisitiza mchezaji huyo, 25, ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, ana thamani ya angalau Pauni 35 milioni.
INTER Milan ipo tayari kutoa Pauni 30 milioni kwa Curtis Jones, lakini Liverpool wanataka zaidi.
Kupitia kwa wawakilishi, Inter waliwasilisha nia yao ya kufanya usajili huo, lakini Liverpool wamesisitiza mchezaji huyo, 25, ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake, ana thamani ya angalau Pauni 35 milioni.
Hapo awali, Liverpool walikataa ofa ya mwisho ya Inter yenye thamani ya pauni 12.75 milioni.
Wakati huohuo, Liverpool wanaendelea na mazungumzo na Paris Saint-Germain kuhusu uwezekano wa kumsajili Bradley Barcola, huku pia wakitathmini maeneo mengine ya kikosi yanayohitaji kuimarishwa.
Aidha, klabu hiyo imepokea maombi kutoka kwa timu mbalimbali kuhusu baadhi ya wachezaji wake ambao hawapo kwenye kikosi cha kwanza lakini walionyesha kiwango kizuri katika ziara ya maandalizi nchini Marekani. Wachezaji hao ni Luke Chambers, Lewis Koumas, Calum Scanlon na Ifeanyi Ndukwe.
Mkurugenzi wa michezo wa Inter Milan, Piero Ausilio, alithibitisha mapema majira haya ya joto Jones bado yuko kwenye orodha ya wachezaji wanaowafuatilia.
“Curtis Jones tunamfuatilia kwa karibu. Hatukuficha hilo. Tunasubiri kuona maendeleo yatakavyokuwa,” alisema Ausilio.
Liverpool wanajiandaa kuanza msimu wao wa kwanza chini ya kocha mpya Andoni Iraola, aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya Arne Slot baada ya kuondolewa mwishoni mwa msimu uliopita.
Bruno Guimaraes
Arsenal imefikia makubaliano ya awali na Newcastle United ya kumsajili kiungo wa Brazil, Bruno Guimaraes, kwa ada inayokadiriwa kufikia Euro90 milioni (Pauni milioni 77). Sasa kinachosubiriwa ni kukamilishwa kwa makubaliano ya mwisho kabla ya nyota huyo kutua Emirates. Alikuwa mmoja wa nyota walioiwakilisha Brazil Kombe la Dunia nchi hiyo ikiishia hatua ya 16 bora.
Cristian Romero
MPANGO wa Inter Milan wa kumsajili beki wa Tottenham Hotspur, Cristian Romero, umekwama kutokana na kutofautiana kuhusu maslahi binafsi ya mchezaji huyo. Sasa wawakilishi wa nyota huyo wa Argentina wanachunguza uwezekano wa kumpeleka Hispania, huku Real Madrid, Barcelona na Atletico Madrid zikitajwa kuonyesha nia kubwa ya kumsajili kabla ya dirisha la usajili kufungwa.
Ethan Nwaneri
AC Milan imeanza mawasiliano na Arsenal kuhusu uwezekano wa kumsajili winga chipukizi wa England, Ethan Nwaneri. Nyota huyo mwenye miaka 19 anaendelea kuvutia vigogo mbalimbali wa Ulaya kutokana na kiwango chake kizuri. Arsenal bado inamwona kama sehemu ya mipango yake ya baadaye, lakini Milan inaamini inaweza kumshawishi kuhamia Serie A.
Vinicius Jr
REAL Madrid haina mpango wa kuboresha ofa yake ya mwisho ya kuongeza mkataba wa Vinicius Jr. Endapo mshambuliaji huyo wa Brazil hatakubali kusaini mkataba mpya, mabosi hao wako tayari kusikiliza ofa zitakazowasilishwa. Arsenal inatajwa kuwa miongoni mwa klabu zinazofuatilia kwa karibu maendeleo ya mazungumzo hayo kabla ya kufanya uamuzi.
Lukas Hornicek
NEWCASTLE United ipo hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kipa wa Czech Republic, Lukas Hornicek, kutoka Braga kwa ada inayokadiriwa kufikia pauni milioni 25. Pande zote zimepiga hatua kubwa katika mazungumzo, huku nyota huyo akitarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya kabla ya kutambulishwa rasmi kama mchezaji mpya wa klabu hiyo.
Amadou Kone
HULL City inakabiliwa na ushindani mkali katika mbio za kumsajili kiungo wa Ivory Coast, Amadou Kone, anayekipiga Neom. Leeds United na West Ham nazo zimeingia kwenye vita ya kuwania saini ya nyota huyo mwenye miaka 21. Klabu hizo zinaamini uwezo wake unaweza kuimarisha safu ya kiungo kuelekea msimu mpya wa mashindano.
Morgan Whittaker
WEST Ham inataka kumaliza usajili wa winga wa England, Morgan Whittaker, kutoka Middlesbrough kabla ya msimu mpya kuanza ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji. Mazungumzo kati ya pande hizo yanaendelea vizuri, huku viongozi wa klabu wakiamini dili hilo linaweza kukamilika ndani ya siku chache zijazo ikiwa makubaliano yatafikiwa.
Max Arfsten
MIDDLESBROUGH ipo hatua za mwisho kukamilisha usajili wa beki wa pembeni wa Marekani, Max Arfsten, kutoka Columbus Crew katika dili linaloweza kufikia pauni milioni 5.6. Klabu hiyo inaamini mchezaji huyo ataongeza ushindani kwenye safu ya ulinzi, huku taratibu za mwisho zikitarajiwa kukamilika kabla ya kutangazwa rasmi.
Ladislav Krejci
WOLVES imekataa ofa iliyowasilishwa na Real Sociedad kwa ajili ya beki wa kati wa Czech Republic, Ladislav Krejci. Klabu hiyo ya England bado haiko tayari kumuachia nyota huyo mwenye miaka 27 na inaamini ataendelea kuwa sehemu muhimu ya kikosi katika msimu ujao, licha ya kuendelea kwa maslahi kutoka Hispania.