Prime
Kiungo awagawa mabosi Simba
BADO haijaeleweka kama kiungo mkabaji wa klabu ya Simba, Alassane Kante ataendelea kusalia kikosini ama kuachwa, kutokana uwepo wa taarifa za viongozi kutofautiana mawazo, kuna wanaotaka mkataba wake usitishwe na wengine kumtaka abakie.
Tayari Simba imeshamsajili kiungo Kelvin Nashon kwenye nafasi ya kiungo mkabaji na awali ilielezwa amepelekwa kwenye timu hiyo kwa ajili ya kuchukua nafasi ya Kante ambaye Simba inataka kumpiga bei, hata hivyo, kuna mabishano makali kwa viongozi wa klabu hiyo wengine wakiamiani anaweza kuwasaidia msimu ujao na wengine wakiamini Yusuf Kagoma na Nashon wanaweza kufanya mambo makubwa msimu ujao wa ligi.
Kwa mujibu wa chanzo cha ndani toka kwa mtu wa karibuni na kiungo huyo kimelieleza Mwanaspoti Kante yupo nchini kushughulikia suala la mkataba wake, wakati Simba ikiendelea na majukumu ya michuano ya CECAFA Kagame Cup 2026 nchini Rwanda.
Kante ni miongoni mwa wachezaji ambao walisajiliwa chini ya aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids msimu wa 2024/2025, wengine ni Naby Camara, Chamou Karaboue, Jonathan Sowah, Neo Maema hao tayari wameachwa na ambaye bado anaendelea kusalia kwa uhakika ni Rushine De Reuck ambaye ameshafanya mambo makubwa kwenye kikosi hicho cha Msimbazi.
Chanzo hicho kilisema: “Kuna viongozi wanataka Kante aendelee kusalia kikosini kwa sababu wanaona bado huduma yake inahitajika, wengine wanataka aondoke atafutwe mbadala wake lakini hata kama atakosekana Kagoma na Nashon wanaweza kufanya kazi nzuri kwenye kikosi hicho na kuipa timu hiyo ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu ujao.
“Hadi sasa suala la mchezaji huyo halijafikia uamuzi, ndiyo maana hayupo pamoja na timu Rwanda, kama akiachwa kila kitu kitawekwa wazi na akisalia mtamwona uwanjani.”
Chanzo hicho kilisema viongozi wanaotaka aendelee kusalia, wanataka aongeze ushindani wa namba dhidi ya Kagoma na Nashon aliyejiunga na timu akitokea Pamba ambayo alijiunga nayo akitokea Singida BS.
Kate alikuwa mhimili sahihi kwenye kikosi cha Simba msimu uliopita akiisaidia timu hiyo kutwaa ubingwa wa Kombe la Muungano pamoja na lile la Shirikisho la CRDB.