Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wanapojifua mastaa Man United usipime

CARRINGTON Pict

Muktasari:

  • Unajua kwa nini? Sababu ni nyingi, lakini mojawapo ni hii, mazingira tulivu na bora kwenye uwanja wa mazoezi wa miamba hiyo ya Old Trafford.

MANCHESTER, ENGLAND: MATHEUS Cunha amechagua mwenyewe kwenda Manchester United. Bryan Mbeumo ametaka mwenyewe kutua Man United. Benjamin Sesko amechagua pia kutua kwa miamba hiyo ya Old Trafford, sawa na kinachokwenda kutokea kwa Carlos Baleba. Kila mtu, anataka kwenda Man United.

Unajua kwa nini? Sababu ni nyingi, lakini mojawapo ni hii, mazingira tulivu na bora kwenye uwanja wa mazoezi wa miamba hiyo ya Old Trafford.

Man United imetambulisha kituo chake cha mazoezi ilichokifanyia maboresho makubwa kilichopo huko Carrington. Man United imetumia Pauni 50 milioni kufanya maboresho makubwa kwenye viwanja hivyo vya mazoezi na kuwa vya kisasa zaidi, ukarabati huo ukifanyika kwa mwaka mmoja.

Taarifa ya klabu ya Man United imefichua ukarabati huo umekamilika kwa wakati na umekwenda sawa na bajeti rasmi iliyokuwa imepangwa.

CARR 01

Vifaa bora na teknolojia ya hali ya juu imeboreshwa kwenye kituo hicho cha mazoezi huku mkazo zaidi ukiwekwa kwenye ufiti wa wachezaji, lishe, matibabu na umoja wa timu. Kituo hicho kilichojengwa kama jengo la ghorofa, sehemu ya juu kuna eneo maalumu kwa ajili ya wachezaji kumpumzika baada ya mazoezi.

Ndani ya kituo hicho pia kuna eneo maalumu kwa ajili ya mastaa wa Man United kuwaleta vinyozi wao, ikiwa ni mara ya kwanza kwenye viwanja vya mazoezi vya timu za England kuwa na eneo kama hilo lililowafikiria zaidi wachezaji.

CARR 02

Eneo la chini kabisa ardhini, kuna kantini ya kiwango bora kabisa na bwawa jipya la kuogelea. Ukarabati na maboresho hayo yamelenga kuwafanya wachezaji kubaki kwenye eneo hilo la Carrington kwa muda mrefu baada ya vipindi vya mazoezi.

Kuifanya timu kuwa pamoja ni jambo muhimu kwa Kocha Ruben Amorim, anayehitaji kikosi hicho kurudi kibabe msimu huu baada ya kufanya vibaya kwenye Ligi Kuu England msimu uliopita.

Kwa eneo la chini, kumetengenezwa kwa mazingira matata kabisa na wachezaji wanaweza kwenda kwenye vyumba vya kubadilishia, gym, bwawa, chumba cha matibabu na masaji ili kuhakikisha wanakuwa fiti kabisa ya kuingia kwenye viwanja vya mazoezi. Gym zake ni za kisasa kwelikweli.

CARR 03
CARR 03

Supastaa, Cristiano Ronaldo alikosoa hali ya Carrington wakati aliporejea mara ya pili man United kati ya mwaka 2021 na 2022. Alilalamikia bwawa la kuogelea halikuwa limefanyiwa mabadiliko yoyote tangu alipoondoka Man United kwenda Real Madrid miaka 12 iliyopita.

Sasa kila kitu kimebadilika, huku ofisi zote sasa zikihamishiwa kwenye ghorofa ya pili na kutakuwa na idara mbalimbali ili kufanya kazi kwa ushirikiano.

Huko Carrington kwa sasa ni mahali ambako mambo mengi ya klabu yatakuwa yanafanyika hata idara ya biashara pia ofisi zake zimehamishiwa huko badala ya Old Trafford.

CARR 04

Mmiliki mwenza wa Man United, bilionea Sir Jim Ratcliffe alisema: “Baada ya kufanyia tathmini viwanja vyetu vya mazoezi tulichukua uamuzi wa kufanya maboresho kwa haraka ili kutengeneza mazingira bora ya kuweza kuleta viwango vya kidunia kwa ajili ya wafanyakazi wetu na wachezaji kwenda sambamba na dira ya Manchester United.

“Tumefurahi kwa hiki kilichofanyika na tunahakika kituo hiki kipya sasa kitakuwa chachu muhimu katika kutengeneza utamaduni wa ushindi klabuni.”