Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Yanga yageukia sayansi ya soka

SAYANSI Pict


KWA miaka ya hivi karibuni, mafanikio ya Yanga yamekuwa yakihusishwa zaidi na ubora wa kikosi chao kutokana na usajili mkubwa ambao wamekuwa wakifanya karibu kila msimu lakini kuelekea msimu ujao, mabingwa hao wa Tanzania wameamua kubadili mtazamo, wamekuja na jambo jipya baada ya kushusha makocha wa viwango vya juu.


Katika hatua ambayo imeonyesha dhamira ya kwenda mbali zaidi ya kutawala zaidi katika soka la ndani na kimataifa, Yanga imewekeza nguvu kubwa kwenye benchi la ufundi kwa kukusanya wataalamu wenye uzoefu wa viwango tofauti vya soka la Afrika na kimataifa, likiwa ni jambo ambalo kwa miaka mingi halijawahi kufanyika hapa nchini.


Chini ya kocha Manqoba Mngqithi ambaye amefanya kazi katika moja ya klabu kubwa Afrika, Mamelodi Sundowns, Yanga sasa imeunda benchi ambalo linaunganisha uzoefu wa ukocha, uchambuzi wa kisasa, maendeleo ya wachezaji na usimamizi wa maeneo maalumo ya mchezo.

Hata hivyo, jambo pekee ambalo linaonekana kuwateka wengi ni Yanga kuleta kocha maalum kwa ajili ya mipira ya kutenga pekee kitu ambacho hakikuwahi kufanywa na timu yoyote huko nyuma zaidi ya Azam ambayo iliwahi kumtambulisha aliyekuwa kocha wao Kally Ongala kuwa kocha wa washambuliaji.

Baada ya Mngqithi kutua nchini juzi, klabu hiyo imekamilisha safu yake ya benchi kwa kumleta Simo Dladla kama kocha msaidizi, Yardaan Valodia kama mchambuzi wa utendaji wa kimbinu, Greg Etafia kuwa kocha wa makipa na aliyekuwa kiungo wa zamani wa Afrika Kusini, Kagisho Dikgacoi, kama sehemu ya timu ya ufundi akiwa na jukumu la kufanyia kazi faulo tu.

Pia wameamua kuendelea na Abdihamid Moallin, aliyekabidhiwa timu mwishoni mwa msimu uliopita na kufanikiwa kuiongoza kutwaa ubingwa wa tano mfululizo wa Ligi Kuu Bara, pamoja na mchambuzi wa video, Thulani Thekiso.

Uamuzi huo unaonyesha kitu kimoja, Yanga haitaki tena kutegemea uwezo wa mtu mmoja pekee. Imeamua kujenga mgawanyo wa majukumu ambapo kila mtaalamu atakuwa na eneo lake la kuhakikisha timu inakuwa bora zaidi.

Katika soka la kisasa kama zilivyo klabu nyingi kubwa ndani na nje ya Afrika, ushindi hauanzi siku ya mechi. Unaandaliwa siku nyingi kabla kupitia uchambuzi wa wapinzani, tathmini ya wachezaji, mipango ya mazoezi na matumizi ya takwimu. Hilo ndilo eneo ambalo Yanga imeonekana kulipa kipaumbele kikubwa.


MNGQITHI NA FALSAFA YA SOKA JIPYA

Mngqithi anaingia Yanga akiwa na jina kubwa ndani ya soka la Afrika. Ni kocha ambaye amejenga heshima yake kupitia falsafa ya mpira unaotawaliwa na nidhamu ya kiufundi, umiliki wa mpira na matumizi sahihi ya nafasi uwanjani.

Akiwa sehemu ya mafanikio makubwa ya Mamelodi Sundowns, Mngqithi amekuwa akihusishwa na mfumo unaosisitiza timu kucheza kwa mpangilio, kujenga mashambulizi kuanzia nyuma na kuwafanya wachezaji kuelewa majukumu yao ndani ya mfumo.

Tofauti na baadhi ya makocha wanaotegemea zaidi uwezo binafsi wa wachezaji, Mngqithi anaamini nguvu ya timu inatokana na mfumo unaoeleweka na kufanyiwa kazi kila siku.

Hilo ndilo jambo ambalo Yanga inatarajia kulipata kutoka kwake siyo tu ushindi wa mechi, bali utambulisho mpya wa namna timu hiyo inavyocheza.


DLADLA, MTU WA KUJENGA MFUMO

Kwa upande wa Simo Dladla, Yanga imepata kocha ambaye ana uzoefu wa kufanya kazi kwenye mazingira tofauti ya soka la Afrika Kusini.

Akiwa amewahi kufanya kazi katika klabu kama Richards Bay, Moroka Swallows, Uthongathi, Maritzburg United na Golden Arrows, Dladla amepitia changamoto mbalimbali zinazomjenga kuwa kocha anayefahamu namna ya kusimamia kikosi.

Moja ya vitu vinavyomfanya kuwa muhimu ni uwezo wake wa kuandaa programu za mazoezi, kusaidia maendeleo ya wachezaji na kuwa kiungo kati ya kocha mkuu na kikosi.

Kwa timu yenye malengo makubwa kama Yanga, nafasi ya kocha msaidizi ni kubwa kuliko wengi wanavyodhani. Mara nyingi ndiye anayekuwa macho ya pili ya kocha mkuu ndani ya uwanja wa mazoezi.


DIKGACOI, UZOEFU WA LIGI KUU ENGLAND

Jina la Kagisho Dikgacoi linaongeza uzito mwingine kwenye benchi hilo.

Aliyekuwa kiungo wa Crystal Palace, Fulham na Cardiff City anakuja na uzoefu wa kucheza katika mazingira ya ushindani mkubwa.

Mbali na kucheza soka la kiwango cha juu England, Dikgacoi aliichezea Afrika Kusini mara 55 na kushiriki mashindano makubwa kama Kombe la Dunia 2010 na kama mashabiki wanakumbuka staa huyo ndiye alitoa pasi kwenye mchezo wa kwanza wa Afrika Kusini dhidi ya Mexico na bao likafungwa na Tshabalala mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1.

Uwepo wake unaweza kuwa na mchango mkubwa kwa wachezaji wa Yanga hasa eneo la viungo, kwa kuwasaidia kuelewa mambo ambayo mara nyingi hayaonekani kwenye takwimu kama kusoma mchezo, kufanya maamuzi haraka na kucheza kwa nidhamu huyo atakuwa na jukumu la kusaidia mipira ya adhabu.


YANGA KWENYE SAYANSI YA SOKA

Moja ya maeneo ambayo yanaonyesha mabadiliko makubwa ni uwekezaji kwenye uchambuzi.

Yanga sasa itakuwa na wataalamu wawili wanaohusika na eneo hilo, Yardaan Valodia na Thulani Thekiso.

Valodia akiwa mchambuzi wa utendaji wa kimbinu anatarajiwa kusaidia zaidi kwenye mipango ya mechi, uchambuzi wa wapinzani na matumizi ya takwimu.

Akiwa amewahi kufanya kazi Mamelodi Sundowns na timu mbalimbali Afrika Kusini, anaelewa umuhimu wa taarifa kabla ya mchezo.

Kwa upande mwingine, Thekiso ataendelea kusimamia eneo la uchambuzi wa video, kuhakikisha benchi linapata picha kamili kuhusu mwenendo wa timu yake na wapinzani.

Huu ni mfumo ambao unatumiwa na klabu kubwa duniani ambako maamuzi mengi hayafanywi kwa mawazo ya mtu mmoja bali kwa taarifa kutoka kundi kubwa la watu.


ENEO LA GOLIKIPA

Katika eneo la makipa, ujio wa Greg Etafia ni hatua nyingine muhimu.

Etafia ana uzoefu wa muda mrefu akiwa mchezaji na kocha. Aliwahi kuwa mmoja wa makipa bora Afrika Kusini akiwa na Moroka Swallows na pia aliwahi kutumika kama kipa wa timu ya Taifa ya Nigeria kwenye mashindano makubwa.

Katika kipindi ambacho makipa wamekuwa sehemu muhimu ya ujenzi wa timu, uwezo wa kuwaandaa vizuri unaweza kuwa tofauti kati ya kushinda na kupoteza. Yanga inatarajia kupata faida hiyo kupitia uzoefu wake lakini uwepo wa makipa wakubwa kama Djigui Diarra unaweza kumsaidia kazi yake kuwa rahisi.


WASIKIE WADAU

Akiongelea benchi hilo, nyota wa zamani wa Mbeya Kwanza, Boniface Nyagawa ambaye aliwahi kucheza soka la kulipwa Seychelles amesema; “Kile ambacho Yanga imefanya ndicho ambacho klabu nyingi kubwa imekuwa ikifanya hasa katika mataifa yaliyoendelea kama Misri, Afrika Kusini na hata Morocco,”

“Leo mpira mkubwa unahitaji watu wengi wenye majukumu tofauti. Kocha mkuu hawezi kufanya kila kitu peke yake. Ukiwa na wachambuzi, kocha wa makipa na wasaidizi wenye uwezo, unakuwa na nafasi kubwa ya kufanya maamuzi sahihi.”

Kwa upande wake, nyota wa zamani wa Yanga, Credo Mwaipopo amesema; “Yanga imeonyesha imeelewa mwelekeo wa soka la kisasa. Sasa mpira haujengwi kwa mazoezi pekee, unahitaji taarifa, takwimu na maandalizi ya kina. Hili ni jambo ambalo klabu kubwa Afrika zimekuwa zikifanya.”

Naye beki wa zamani wa Yanga, Ladislaus Mbogo amesema “Kitu kizuri kwenye benchi hili ni mchanganyiko wa uzoefu wa kimataifa na watu wanaojua mazingira ya Tanzania. Wakipata muda wa kufanya kazi pamoja, Yanga inaweza kuwa na mfumo imara zaidi kuliko misimu iliyopita.”

Nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua amesema uwekezaji huo utaonekana zaidi kwenye mashindano ya kimataifa, ambako timu hiyo imekuwa ikihitaji kuongeza ushindani dhidi ya vigogo.

“Hesabu kubwa za Yanga kwa sasa  nadhani ni kwenye michuano ya kimataifa, ndani ya nchi wameonyesha kwa miaka kadhaa kuwa wana uwezo wa kushindana, lakini hatua inayofuata ni kuhakikisha wanakuwa na ushindani mkubwa Afrika. Benchi lenye wataalamu wa maeneo tofauti linaweza kusaidia timu kufanya maandalizi bora kabla ya kukutana na wapinzani wa kiwango cha juu,” amesema Chambua.

Kwa upande wake, Mzee John Tegete ambaye aliwahi kuwa kocha wa Toto Africans ya Mwanza amesema hatua ya Yanga kuwa na benchi pana ni ishara kuwa klabu hiyo imeanza kuwekeza zaidi kwenye ufundi kuliko kutegemea ubora wa wachezaji pekee.

“Kwenye soka la sasa, mafanikio hayaji kwa kusajili wachezaji wazuri peke yake, unahitaji kuwa na mfumo wa kuwaandaa, kuwafuatilia na kuboresha kila eneo. Yanga imefanya jambo ambalo linaweza kuipa faida kubwa lakini kinachofuata ni kuwapa muda wataalamu hawa kufanya kazi na kuona matokeo,” amesema Tegete.