Mastaa 15 watakaotikisa dirisha la usajili
Muktasari:
- Wachezaji wengi wameongeza thamani yao kutokana na kiwango walichoonyesha kwenye mashindano hayo, jambo linalowafanya kuwa miongoni mwa majina makubwa yanayoweza kubadili klabu kabla ya dirisha kufungwa.
LONDON, ENGLAND: KOMBE la Dunia 2026 limehitimishwa, lakini sasa vita vinahamia kwenye dirisha la usajili, huku klabu zikianza kufuatilia kwa karibu nyota walioangaza nchini Marekani, Canada na Mexico.
Wachezaji wengi wameongeza thamani yao kutokana na kiwango walichoonyesha kwenye mashindano hayo, jambo linalowafanya kuwa miongoni mwa majina makubwa yanayoweza kubadili klabu kabla ya dirisha kufungwa.
15. James Trafford (Manchester City)
Kipa wa Manchester City ameendelea kupanda thamani baada ya kuitwa katika kikosi cha England cha Kombe la Dunia.
Ingawa Jordan Pickford alikuwa kipa namba moja, Trafford (23) anaonekana kama mrithi wa baadaye wa lango la England.
Newcastle United na Leeds United ni miongoni mwa klabu zinazomuwania.
14. Djed Spence (Tottenham)
Beki huyo wa kulia anatajwa kuwa tayari kuondoka Tottenham.
Inter Milan inatajwa kuwa mbele katika mbio za kumsajili kama mbadala wa Denzel Dumfries, huku Spurs wakimthaminisha kwa takribani pauni milioni 40.
13. Joao Cancelo (Al-Hilal)
Cancelo bado anatamani kubaki Barcelona, lakini Al-Hilal haitaki kumuachia kwa bei ya chini.
Klabu hiyo ya Saudi Arabia inadaiwa kutaka pauni milioni 13 na haiko tayari kumtoa kwa mkopo tena.
12. John Stones
Beki huyo wa England anahusishwa na kujiunga na Arsenal baada ya kuondoka Manchester City.
Jeraha la William Saliba limeifanya Arsenal kutafuta beki mwenye uzoefu, huku Mikel Arteta akimfahamu vizuri tangu walipokuwa pamoja Etihad.
11. Cristian Romero (Tottenham)
Romero anaonekana kuwa karibu kuondoka Spurs.
Atletico Madrid inaendelea kufanya juhudi kubwa za kumsajili beki huyo wa Argentina, huku Tottenham ikiendelea kujenga kikosi kipya chini ya Roberto De Zerbi.
10. Ayyoub Bouaddi (Lille)
Kiungo huyo mwenye miaka 18 alikuwa mmoja wa nyota waliovutia zaidi kwenye Kombe la Dunia baada ya kuisaidia Morocco kutinga robo fainali.
Manchester United, Liverpool na Manchester City zote zinamfuatilia, huku Lille ikidaiwa kumuwekea thamani ya karibu pauni milioni 100.
9. Folarin Balogun (Monaco)
Balogun ameendelea kuwavutia vigogo baada ya kufunga mabao 19 akiwa Monaco na kuongeza mengine matatu katika Kombe la Dunia akiwa na Marekani.
Sunderland, Newcastle, Nottingham Forest, Everton, Leeds United, Fulham, Borussia Dortmund, Juventus na Atletico Madrid zote zinatajwa kumuwania mshambuliaji huyo.
8. Bradley Barcola (Paris Saint-Germain)
Liverpool imepiga hatua katika mbio za kumwania Barcola baada ya kuwasilisha ofa ya kwanza.
Arsenal pia bado inamuhitaji, lakini PSG inaendelea kusisitiza kuwa haitaki kumuuza mmoja wa nyota wake muhimu.
7. Ferran Torres (Barcelona)
Bao lake la ushindi kwenye fainali ya Kombe la Dunia limeongeza thamani yake sokoni.
Liverpool inadaiwa kuingia kwenye mbio za kumsajili, huku PSG pia ikiendelea kumuwania.
Barcelona inaweza kumuuza kutokana na mkataba wake kubakiza mwaka mmoja.
6. Yan Diomande
Kijana huyo wa Ivory Coast alikuwa mmoja wa nyota chipukizi wa Kombe la Dunia.
Liverpool ilijaribu kumchukua dakika za mwisho, lakini PSG inaonekana kuwa karibu kukamilisha usajili wake kutoka RB Leipzig.
5. Goncalo Inacio (Sporting CP)
AC Milan bado ina nia ya kumsajili beki huyo wa Ureno licha ya kuwa karibu na Mario Gila wa Lazio.
Sporting inatajwa kutaka takribani pauni milioni 35 kwa mchezaji huyo mwenye miaka 24.
4. Rodri (Manchester City)
Nahodha wa Hispania na mshindi wa Tuzo ya Golden Ball ya Kombe la Dunia anaendelea kuwindwa na Real Madrid.
Hata hivyo, Manchester City inataka kumuongezea mkataba mpya ili kumzuia kuondoka.
3. Marcus Rashford (Manchester United)
Mustakabali wa Rashford unaendelea kuwa kitendawili.
Baada ya kuisaidia England kutinga nusu fainali ya Kombe la Dunia, mshambuliaji huyo amerudi Manchester United huku hatma yake ikiwa bado haijulikani.
2. Bruno Guimaraes (Newcastle United)
Arsenal imeanza mazungumzo ya moja kwa moja na Newcastle kwa ajili ya kiungo huyo wa Brazil baada ya kushindwa kumsajili Morgan Rogers.
Guimaraes pia ameonyesha nia ya kujiunga na mabingwa wa Premier League.
1. Enzo Fernandez (Chelsea)
Kiungo wa Argentina ndiye anayeshika nafasi ya kwanza kwenye orodha hii.
Baada ya kung'ara tena kwenye Kombe la Dunia, Enzo anaendelea kuhusishwa na Real Madrid.
Chelsea inasisitiza haitaki kumuachia, lakini jina lake linatarajiwa kuendelea kutawala mijadala ya usajili hadi dirisha litakapofungwa.