Mabao 38! Yanga U-17 yatikisa ligi ya vijana
Muktasari:
- Chini ya uongozi wake, Yanga U-17 imebadilika na kuwa moja ya timu zinazocheza soka la kuvutia zaidi kwenye Ligi ya Vijana chini ya miaka 17, huku ikiwa mbioni kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
LICHA ya kuwa ni miezi mitatu pekee tangu akabidhiwe jukumu la kusimamia mradi wa Yanga Soccer Schools, kocha Mohamed Badru ameanza kuonyesha matunda ya kazi yake kwa kumuibua Reny Nyanguge ‘Cunha’ huku wadau wakitia neno.
Chini ya uongozi wake, Yanga U-17 imebadilika na kuwa moja ya timu zinazocheza soka la kuvutia zaidi kwenye Ligi ya Vijana chini ya miaka 17, huku ikiwa mbioni kutwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Badru ameijenga timu inayocheza kwa kasi, kushambulia muda mwingi na kutumia vyema nafasi za kufunga, jambo lililoifanya Yanga kuwa timu yenye mabao mengi zaidi kwenye ligi mpaka sasa.
Mabadiliko hayo yameifanya klabu hiyo kuamini kuwa mradi wa kuandaa vipaji vya baadaye unaanza kutoa matokeo yanayoonekana uwanjani.
Safari ya ubingwa sasa ipo mikononi mwa Yanga yenyewe. Vijana hao wanahitaji kushinda michezo yao miwili iliyosalia dhidi ya Transit Camp na TDS ili kutwaa taji hilo.
Kwa sasa Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo ikiwa na pointi 29 baada ya kucheza mechi 12, ikishinda tisa, kutoka sare mbili na kupoteza mmoja pekee. Wanaachwa kwa tofauti ya pointi moja na vinara JKT Tanzania ambao tayari wamecheza michezo 13.
Hali hiyo inaifanya Yanga kuwa na nafasi kubwa ya kupanda kileleni kwani bado ina mchezo mmoja wa kiporo dhidi ya Tanzania Prisons. Ushindi kwenye mchezo huo utaipeleka kileleni mwa msimamo na kuwapa nafasi nzuri ya kumaliza kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo.
Kilichoifanya Yanga kuwa tofauti na wapinzani wake msimu huu ni uwezo mkubwa wa kushambulia. Katika michezo 12, tayari imefunga mabao 38, ikiwa na wastani wa mabao 3.18 kwa kila mchezo, rekodi inayoiweka mbele ya timu nyingine kwenye ligi hiyo.
Mbali na safu kali ya ushambuliaji, Yanga pia imeonyesha uimara mkubwa nyuma baada ya kuruhusu mabao nane pekee katika mechi hizo 12, wastani wa bao 0.55 kwa mchezo. Takwimu hizo zinaonyesha timu hiyo imekuwa na uwiano mzuri kati ya kushambulia na kujilinda, jambo ambalo mara nyingi huwa msingi wa kutwaa ubingwa.
Tofauti ya mabao ya Yanga (+30) inaweza kuwa silaha muhimu katika hatua za mwisho za ligi endapo timu zitamaliza zikiwa na idadi sawa ya pointi.
Katika vita hiyo ya ubingwa, Simba U-17 nao hawapo nyuma. Kikosi hicho kinachonolewa na nahodha wa zamani wa Wekundu wa Msimbazi, John Bocco kipo nafasi ya tatu kikiwa na pointi 29 baada ya kucheza michezo 12 sawa na Yanga.
Hata hivyo, takwimu zinaonyesha tofauti kubwa katika nguvu ya ushambuliaji. Simba imefunga mabao 32 pekee katika michezo hiyo 12, ikiwa na wastani wa mabao 2.67 kwa kila mchezo huku ikiruhusu mabao saba. Hiyo ina maana tofauti kubwa kati ya timu hizo ipo kwenye uwezo wa kutengeneza na kutumia nafasi za kufunga.
Mchezaji anayebeba matumaini makubwa ya Yanga ni mshambuliaji Reny Nyanguge, maarufu kwa jina la “Cunha” ambaye amekuwa katika kiwango cha juu msimu huu. Nyota huyo tayari amefunga mabao 16 katika michezo 12, amekuwa na wastani wa kufunga katika kila mchezo wa ligi hiyo.
WASIKIE WADAU
Beki wa zamani wa Yanga, Abdallah Shaibu ‘Ninja’ amesema; “Kwenye soka la vijana matokeo ni muhimu lakini maendeleo ya mchezaji ndiyo jambo kubwa zaidi. Kama umewahi kupata nafasi ya kuwaona Yanga U-17 wakicheza kama mimi kiukweli vijana wajiamini na kucheza kwa utulivu.”
Aliongeza kwa kusema; “Hata idadi ya mabao waliyoifunga inaonyesha, kwangu huo ni mwelekeo mzuri kwa klabu na naamini viongozi wataendelea kuwekeza nguvu huko kwa sababu kama nchi tunahitaji vijana wengi wenye vipaji kuendelezwa, mambo haya hayakuwepo miaka ya nyuma.”
Kwa upande wake, Hassan Nassoro ambaye alikuwepo katika mchezo dhidi ya Coastal Union ya Tanga, amesema kama ile ndio kazi ya miezi mitatu basi huenda ikashuhudiwa kitu kikubwa zaidi kama kocha huyo wa zamani wa Azam.
“Kuna dogo anaitwa Reny nilivutiwa naye, alifunga mabao yote manne ya Yanga dhidi ya Coastal, yule mtoto anaweza kufika mbali pia kuna kiungo mmoja niliona jina lake simkumbuki ni mali sana,” amesema.