Saliba kuikosa Arsenal kwa muda mrefu
Muktasari:
- Beki huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa akisumbuliwa na tatizo hilo kwa wiki kadhaa kabla ya mashindano, lakini aliamua kuendelea kucheza hadi alipolazimika kutolewa baada ya dakika 30 katika mchezo wa nusu fainali ambao Ufaransa ilifungwa na Hispania.
LONDON, ENGLAND: ARSENAL imethibitisha kuwa beki wake tegemeo William Saliba atakosekana uwanjani kwa muda mrefu baada ya kupata jeraha la mgongo alipokuwa akiitumikia Ufaransa kwenye Kombe la Dunia.
Beki huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa akisumbuliwa na tatizo hilo kwa wiki kadhaa kabla ya mashindano, lakini aliamua kuendelea kucheza hadi alipolazimika kutolewa baada ya dakika 30 katika mchezo wa nusu fainali ambao Ufaransa ilifungwa na Hispania.
Baada ya kurejea London na kufanyiwa uchunguzi na madaktari bingwa, imebainika kuwa hatohitaji upasuaji, badala yake atapitia programu maalumu ya matibabu na ukarabati hadi atakapokuwa tayari kurejea uwanjani.
Kutokana na jeraha hilo, Saliba pia alikosa mchezo wa kuwania nafasi ya tatu ambapo Ufaransa ilifungwa na England.
Akizungumza akiwa kwenye Kombe la Dunia, Saliba alikiri kuwa alikuwa akivumilia maumivu kwa muda mrefu.
"Nimekuwa nikisumbuliwa na majeraha madogo kwa miezi kadhaa. Nilivumilia kwa sababu kulikuwa na Ligi ya Mabingwa, Ligi Kuu England na baadaye Kombe la Dunia, ambalo hufanyika mara moja tu kila baada ya miaka minne," amesema Saliba.
Msimu uliopita, Saliba alicheza mechi 50 katika mashindano yote akiwa na Arsenal, akichangia klabu hiyo kutwaa taji la Ligi Kuu England kwa mara ya kwanza baada ya miaka 22, pamoja na kufika fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Kutokuwepo kwake ni pigo kubwa kwa kocha Mikel Arteta, ambaye anajiandaa kuanza msimu mpya kwa mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Manchester City kabla ya Arsenal kuanza utetezi wa taji la Ligi Kuu dhidi ya Coventry City.