Wakipatikana hawa Liverpool, maji mtaita ‘Mmma’
Muktasari:
- Kwenye dirisha hili, Liverpool imefanya usajili wa kibabe, akiwamo Florian Wirtz, ambaye uhamisho wake umevunja rekodi Uingereza, huku wengine Jeremie Frimpong na Milos Kerkez, nao wamenaswa kwa pesa nyingi.
LIVERPOOL, ENGLAND: HUU msimu patakwenda kuchimbika. Liverpool inaonekana kufungua pochi kuhakikisha kocha Arne Slot anafanya usajili kwenye dirisha lake la kwanza la majira ya kiangazi - na sasa kinachoonekana, miamba hiyo ya Anfield haijafunga hesabu.
Kwenye dirisha hili, Liverpool imefanya usajili wa kibabe, akiwamo Florian Wirtz, ambaye uhamisho wake umevunja rekodi Uingereza, huku wengine Jeremie Frimpong na Milos Kerkez, nao wamenaswa kwa pesa nyingi.
Na Liverpool haionekani kupunguza kasi kwenye kufungua pochi kufanya usajili kwenye dirisha hili la majira ya kiangazi. Kwenye kuanzia safu ya ushambuliaji, kocha Slot anahitaji huduma ya straika wa kiwango cha dunia, Alexander Isak.
Mchakato huo ulianza kufanywa ndani ya wiki hii, ambapo Liverpool inamtazama Isak kuwa na thamani ya Pauni 125 milioni. Lakini, Newcastle imesisitiza Isak, 25, hauzwi, huku ikimthaminisha mkali huo kuwa na thamani ya Pauni 150 milioni.
Kwenye safu ya ulinzi, Marc Guehi amewekwa kwenye mipango. Taarifa za hivi karibuni zinafichua kwamba mabingwa wa Ligi Kuu England wanahitaji huduma ya beki huyo wa kimataifa wa England, ambaye mkataba wake huko Crystal Palace utafika ukomo kwenye dirisha lijalo la uhamisho wa majira ya kiangazi.
Guehi naye hawezi kupatikana kwa bei ndogo hasa baada ya kuwaongoza Palace kucheza michuano ya Ulaya msimu ujao baada ya kushinda taji la Kombe la FA. Na sababu kubwa ya Liverpool kumtaka Guehi ni kwa kuwa inatia shaka na ubora wa Ibrahima Konate, ambaye anaweza kufunguliwa mlango wa kutokea huko Anfield.
Konate, mkataba wake unaelekea mwisho na kinachoonekana ni kama vile anataka kupita kwenye nyayo za Trent Alexander-Arnold kwenda kujiunga na Real Madrid kwa uhamisho wa bure mwaka 2026.
Kwenye hilo, baadhi ya mashabiki wa Liverpool wanashauri Konate auzwe sasa ili timu ipate pesa au imweke benchi kama itafanikiwa kunasa saini ya beki wa kati, Guehi.
Na sasa beki huyo wa zamani wa Chelsea, anaweza kwenda kuunda safu mpya ya ulinzi ya Liverpool sambamba na Frimpong na Kerkez wakicheza beki za pembeni, wakati pacha wake kwenye beki ya kati ni Virgil van Dijk.
Kikosi cha Liverpool, golini ataendelea kubaki Alisson Becker, licha ya kusajiliwa kwa Giorgi Mamardashvili, ambaye anatazamwa kama mbadala wa muda mrefu wa kipa huyo wa Kibrazili kwenye lango la wababe hao wa Anfield.
Kocha Slot ni mpenzi wa fomesheni ya 4-2-3-1, hivyo Ryan Gravenberch na Alexis Mac Allister wataendelea kupata nafasi kucheza kwenye “double pivot” kwenye kiuno cha safu ya kiungo, lakini juu yao hatakuwa tena Dominik Szoboszlai kama Wirtz atapangwa kwenye nafasi anayopenda kucheza.
Hata hivyo, staa huyo wa Kijerumani, Wirtz ni kiraka, anaweza pia kucheza kama winga wa kushoto au mshambuliaji wa kati, lakini Slot bila shaka atahitaji kupata huduma yake bora kwa kumpanga Namba 10.
Mo Salah nafasi yake kwenye timu haina mjadala, wakati Cody Gakpo au Luis Diaz mmoja ndiye atakayepewa nafasi kwenye timu, huku mwingine anaweza kufunguliwa mlango wa kutokea. Na kwenye nafasi ya mshambuliaji wa kati, hakuna shaka atapewa nafasi Isak, endapo kama saini yake itanaswa na miamba hiyo ya Anfield.
Kama Slot atafanikiwa kunasa kikosi hicho, je kuna timu itaweza kuizuia Liverpool kwenye ubingwa wa Ligi Kuu England msimu ujao?
Mwezi mmoja umebaki kabla ya Liverpool kutupa kete yake ya kwanza kwenye Ligi Kuu England, ambapo Ijumaa ya Agosti 15, itakipiga na Bournemouth. Lakini, mechi ya kwanza ya ushindani ya Liverpool itapigwa siku sita kabla ya hapo, ambapo itakipiga na Palace kwenye kipute cha Ngao ya Jamii.
Mambo yakibaki kama ilivyo kwa sasa, Guehi atakuwa kwenye safu ya ulinzi ya Palace. Baadaye mwezi ujao, Slot na jeshi lake litakwenda kukipiga na Newcastle, ambapo safu yake ya mabeki itakuwa na kazi ya kumkabili Isak endapo kama itashindwa kufanikiwa usajili wake ambao utavunja rekodi ya uhamisho England.
Kikosi kinachotarajiwa Liverpool: Alisson; Frimpong, Guehi, Van Dijk, Kerkez; Mac Allister, Gravenberch; Salah, Wirtz, Gakpo; Isak