Defoe atimka baada ya miezi minne tu
Muktasari:
- Defoe alikiongoza kikosi hicho katika mechi sita rasmi na alikuwa tayari akiandaa timu kwa ajili ya msimu mpya kabla ya kuamua kujiuzulu ghafla.
LONDON, ENGLAND: NYOTA wa zamani wa England, Jermain Defoe, ameondoka katika klabu ya Woking inayoshiriki National League baada ya kukaa madarakani kwa miezi minne pekee.
Defoe alikiongoza kikosi hicho katika mechi sita rasmi na alikuwa tayari akiandaa timu kwa ajili ya msimu mpya kabla ya kuamua kujiuzulu ghafla.
Kwa mujibu wa taarifa, Defoe hakufika kuendesha mazoezi siku ya Alhamisi na baadaye aliipigia simu klabu hiyo kuwajulisha kuwa ameamua kuachia nafasi yake.
Chanzo kimoja kilieleza kuwa kulikuwa na mgogoro wa ndani kati ya Defoe na mmoja wa viongozi wa klabu hiyo, ingawa Woking imekataa kutoa maelezo zaidi.
Katika mechi sita alizoiongoza, Defoe alipoteza mchezo mmoja pekee huku timu ikimaliza nafasi ya 10 kwenye ligi hiyo.
Kupitia taarifa rasmi, Woking ilisema:
"Woking Football Club inathibitisha kuwa klabu na kocha wa timu ya kwanza Jermain Defoe wamekubaliana kuachana mara moja."
"Tunamshukuru kwa mchango wake na tunamtakia kila la heri katika maisha yake ya baadaye."
Kupitia Instagram, Defoe aliandika:
"Baada ya mazungumzo ya hivi karibuni, ninaweza kuthibitisha kuwa nimekubaliana na Woking kuondoka katika nafasi yangu ya ukocha. Kwa bahati mbaya mazingira yaliyopo yamefanya isiwezekane kuendelea."
"Najivunia kazi tuliyoifanya na niliamini tulikuwa tunajenga kitu maalumu."
"Nawashukuru viongozi, mashabiki na zaidi wachezaji ambao ninawaonea uchungu kwa sababu ni kundi bora sana."
"Nimevunjika moyo kuona safari imefika mwisho mapema lakini ninaondoka nikiwa na fahari kubwa kwa kile tulichokuwa tunakijenga."
"Uzoefu wangu Woking utanifanya kuwa kocha imara zaidi katika hatua inayofuata ya maisha yangu."