Mfungaji bora kupishana na Ahoua Singida
Muktasari:
- Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa kutoka ndani ya Singida zinabainisha kwamba, klabu hiyo ipo mbioni kumuuza mshambuliaji Mosi Nduwumwe ambaye aliibuka kinara wa ufungaji Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026 akipachika mabao 17 zikiwemo hat trick mbili.
NI suala la muda kwa Singida Black Stars, kumalizana na aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Jean Charles Ahoua ili kuwa sehemu ya kikosi hicho msimu ujao.
Wakati hali ikiwa hivyo, taarifa kutoka ndani ya Singida zinabainisha kwamba, klabu hiyo ipo mbioni kumuuza mshambuliaji Mosi Nduwumwe ambaye aliibuka kinara wa ufungaji Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026 akipachika mabao 17 zikiwemo hat trick mbili.
Ahoua aliyeichezea Simba msimu wa 2024-2025 ikiwa ni mara ya kwanza kushiriki Ligi Kuu ya NBC, naye alikuwa mfungaji bora alipomaliza na mabao 16 na asisti tisa, kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari 2026, aliondoka kwenda CR Belouizdad ya Algeria.
Taarifa kutoka kwa mmoja wa viongozi wa Singida BS, mchakato wa kukamilisha usajili wa Ahoua upo pazuri na kuna uwezekano nyota huyo akajiunga na timu hiyo nchini Rwanda ambako inacheza michuano ya Cecafa Kagame Cup 2026.
"Kuna wachezaji wengi wapya tuliowasajili, wataungana na timu Rwanda ambako tunakwenda kucheza kama bingwa mtetezi wa michuano ya Cecafa Kagame Cup, hivyo suala la Ahoua likikamilika basi atajiunga na timu huko," amesema kiongozi huyo.
Ahoua aliyezaliwa Februari 10, 2002 (umri wa miaka 24) nchini Ivory Coast, hakucheza kwa muda mrefu katika klabu ya Belouizdad, akidumu kwa takriani miezi sita tangu ajiunge nayo Januari 2026 akitokea Simba.
"Tunaamini kiwango cha Ahoua kitakuja kuongeza nguvu na timu kuwa na ushindani kila nafasi. Ukiangalia hata usajili wetu tunaleta wachezaji wa kuboresha kikosi, ndiyo maana tumeamua kumrejesha Jonathan Sowah ambaye licha ya kumsajili dirisha dogo msimu wake wa kwanza 2024-2025 alimaliza na mabao 13, alipoenda Simba 2025-2026 licha ya kukosa nafasi ya kucheza alikuwa na mabao matatu, hivyo tunaamini likikamilika suala la Ahoua tutakuwa timu ya ushindani."