Prime
Hatma ya nyota wazawa Simba, Yanga
TUWAOMBEE! Ni kauli za baadhi ya wadau wa soka hapa nchini kuhusu wazawa wanaocheza timu za Yanga na Simba kuelekea msimu ujao wa 2026-2027 baada ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) kuruhusu timu kusajili wachezaji 40.
Ruhusa hiyo imekuja ili kuendana na kasi ya msimu wa 2026-2027 wa Ligi Kuu ya NBC unaotakiwa kuanza Agosti 14, 2026 na kumalizika Mei 15, 2027 kwani ratiba inaonekana mechi moja kwenda nyingine zipo karibu zaidi na hakutakuwa na sababu ya kuweka viporo.
Hii yote inatokana na kwamba, Tanzania ni mwenyeji wa AFCON 2027, michuano itakayoanza Juni 19, 2027 hadi Julai 17, 2027 kwa ushirikiano wa Kenya na Uganda.
Kabla ya ruhusa hiyo, imekuwa ni kawaida kwa timu za Ligi Kuu ya NBC kusajili wachezaji 30 kila moja, hata hivyo, kwa Simba na Yanga wazawa wengi imekuwa changamoto kupenya kikosi cha kwanza kutokana na uwepo wa wageni 12 wanaoruhusiwa kikanuni, hivyo kufanya kuishia benchi au kukaa jukwaani kabisa wakati walipotoka walikuwa wakipata nafasi ya kucheza.
Kukosa nafasi huko kunawarudisha nyuma kiuwezo, hivyo kuja kurudi tena katika kiwango kile kile cha awali, labda waondoke hapo.
Katika kikosi cha Simba msimu wa 2025-2026, wazawa waliokuwa wanapata nafasi kubwa ya kucheza ni Shomari Kapombe, Yusuph Kagoma na Nickson Kibabage, huku wengi wao wakiishia benchi. Seleman Mwalimu alianza vizuri, baadaye akawa anatokea benchi.
Miongoni mwa nyota ambao licha ya walikotoka walikuwa wanacheza vizuri lakini baada ya kujiunga na Simba walikutana na ushindani mkali na kupata nafasi ndogo ya kucheza ni Antony Mligo, Hussein Semfuko, David Kameta na Morice Abraham, huku Ladack Chasambi naye akikosa nafasi hadi kufikia hatua ya kuuzwa kwenda Singida Black Stars. Salehe Karabaka alitolewa kwa mkopo Namungo, JKT Tanzania na sasa ameelekea Pamba Jiji, wakati Awesu Awesu alipelekwa Kenya Police kwa mkopo, mkataba umeisha ameagwa na kutimkia Namungo. Valentino Mashaka akapelekwa kwa mkopo JKT Tanzania.
Kwa upande wa magolikipa, isingekuwa kuumia kwa Yakoub Suleiman aliyesajiliwa kutoka JKT Tanzania ambapo msimu wa 2024-2025 alimaliza na cleansheets nane, basi ingekuwa ngumu kwa Hussein Abel kuendelea kusalia hapo.
Pia mabeki Wilson Nangu na Abdulazak Hamza majeraha yamewakwamisha, kwani walishaanza kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosini, walipoumia wakakosa takribani msimu mzima.
Vivyo hivyo kwa Yanga kuna wachezaji wachache wazawa ambao wamekuwa na uhakika wa namba kikosi cha kwanza kama Dickson Job kabla ya kuumia, Ibrahim Hamad 'Bacca', Mohamed Hussein na Bakari Mwamnyeto anayeingia na kutoka kama ilivyo kwa Mudathir Yahya.
Lakini nyota wengine wazawa wamekosa nafasi kama Offen Chikola alitolewa kwa mkopo kwenda Singida Black Stars, lakini wakati yupo Tabora United na sasa TRA United msimu wa 2024-2025 alifanya vizuri na kumaliza akifunga mabao saba. Faridi Mussa amemaliza mkataba na kuna tetesi anaweza akaachwa, Denis Nkane alitolewa kwa mkopo msimu uliyopita kwenda TRA United.
Wengine ni Aziz Andabwile anayetajwa huenda akaachwa, kiungo mkabaji Abdulnassir Mohammed 'Casemiro' na kiungo mshambuliaji Shekhan Ibrahim Khamis ambaye imeelezwa katolewa kwa mkopo kwenda Singida Black Stars. Pia Nizar Abubakar 'Ninju', Salum Abubakar 'Sure Boy', Emmanuel Mwanengo na Kibwana Shomari.
Kwa upande wa magolikipa, Khomeiny Abubakar, Abuutwalib Mshery na Hussein Masalanga uwepo wa Djigui Diarra unawafanya wawe na nafasi finyu ya kucheza.
Kuelekea msimu ujao, Yanga imetambulisha wachezaji wazawa watano ambao ni kiungo mshambuliaji Juma Issa Abushiri, winga Erick Mwijage, mshambuliaji Hussein Mihambo na mabeki Abdulnasir Mohamed na Mohamed Mussa.
Kwa upande wa Simba, imewatambulisha wazawa beki wa kulia Nathaniel Chilambo, kiungo mkabaji Kelvin Nashon na kiungo mshambuliaji Bakari Msimu.
KAULI ZA WADAU
Kocha wa Singida BS, Muhibu Kanu, amesema: "Kutokana na ratiba ya msimu unaokuja kitendo cha TFF na TPLB kuruhusu timu zisajili wachezaji 40, inaturahisishia makocha kuwa na uwanja mpana wa kuwatumia wachezaji."
Nyota wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, amesema: "Kocha ambaye alikuwa na uthubutu wa kubadilisha kikosi na ilikuwa ngumu kuzisoma mbinu zake alikuwa Nasreddine Nabi wa Yanga ndiyo maana kina Farid, Salum Abubakar 'Sure Boy', Nkane, Clement Mzize walikuwa wanacheza, ila wengine ni ngumu sana kukabiliana na hilo. Tuwaombee hali iwe tofauti kwa sasa ili wapate nafasi, lakini wanapaswa kujituma kwani nafasi haiji kirahisi."
Ameongeza: "Kusajili wachezaji 40 siyo ishu ila kuwatumia ni kitu kingine kabisa. Kujituma na kuonesha bidii uwanja wa mazoezi ndiyo silaha ya kupata nafasi."
Mwingine aliyechangia hilo ni muasisi wa klabu ya mpira ya Friends Rangers, Heri Mzozo amesema: "Endapo kama wachezaji wazawa wataiona kama fursa hasa kwa Simba na Yanga ambako wengi wao ndiko wanakobadilishia maisha yao kiuchumi, itawasaidia kuonyesha uwezo wao, vinginevyo tutaendelea kuwaona wageni kupata nafasi zaidi. Wapambane."
Mshambuliaji wa zamani wa Simba, Moses Phiri kwa sasa anacheza Nkana FC ya nchini kwao Zambia, amesema: "Kwa muda niliocheza Tanzania sijaona tofauti sana ya kiwango kati ya wazawa na wageni, wageni wanakuwa wanapambana zaidi kwani wanajua wapo ugenini."
Ameongeza: "Wakati huo nacheza Simba walikuwepo kina John Bocco, Kapombe, Mohemed Hussein 'Tshabalala' viwango vyao vilikuwa juu, hivyo kupata nafasi ni mchezaji mwenyewe kujituma kwa bidii."