Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Wakifunguliwa mlango wa kutokea Januari usishtuke!

Muktasari:


  • Mambo kama hayo ya kunasa mastaa wapya kwenye dirisha la Januari yanaweza kushuhudiwa pia kwenye vikosi vya Manchester United, Arsenal na pengine hata Liverpool, licha ya wakali hao wa Anfield kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi nne kwa sasa na bado wana mechi moja mkononi.

LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England imezidi kunoga kutokana na mchakamchaka wa kusaka ubingwa kuzidi kupamba moto. Manchester City mambo yao si mazuri kwa sasa, lakini bila ya shaka wakati dirisha la usajili la Januari litakapofunguliwa, miamba hiyo ya Etihad itaingia sokoni kunasa wakali wapya wa kuboresha kikosi.

Mambo kama hayo ya kunasa mastaa wapya kwenye dirisha la Januari yanaweza kushuhudiwa pia kwenye vikosi vya Manchester United, Arsenal na pengine hata Liverpool, licha ya wakali hao wa Anfield kuongoza ligi kwa tofauti ya pointi nne kwa sasa na bado wana mechi moja mkononi.

Hata hivyo, wakati dirisha la usajili la Januari likikaribia, kwenye timu 20 za Ligi Kuu England, kuna mchezaji mmoja ambaye atakuwa na bahati kubwa endapo kama ataendelea kubaki kikosini hadi dirisha la Januari litakapofungwa.

Kwa jinsi ya mambo yalivyo kwa wachezaji hao, endapo kama timu hizo zitahitaji kuondoa mchezaji mmoja kikosini ili kupata nafasi ya kuingiza mchezaji mpya, basi ishu ya kufunguliwa mlango wa kutokea inaweza kumhusu. Mchezaji wa kila timu kwenye Ligi Kuu England akipigwa bei Januari usishtuke.


Arsenal – Jakub Kiwior

Ni kawaida kwa timu inayofukuzia ubingwa, hakuna nafasi kwa mchezaji ambaye kiwango chake hakiwezi kuongeza kitu kwenye timu. Staa wa kimataifa wa Poland, Jakub Kiwior amejikuta hana nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza cha Arsenal kutokana na ujio wa mastaa wengine kwenye timu hiyo kama vile Riccardo Calafiori. Kutokana na hilo, kocha Mikel Arteta anaweza kufikiria mpango wa kumwondoa Kiwior kwenye dirisha la Januari ili kupunguza idadi ya wachezaji kwenye kikosi hicho kufungua milango ya kuja wengine. Haitakuwa kitu cha kushangaza Kiwior akipigwa bei kwenye dirisha la Januari.


Aston Villa – Emiliano Buendia

Kwenye mipango ya sasa ya kocha Unai Emery hakuonekani kuwa na nafasi tena kwa kiungo Emiliano Buendia. Mhispaniola Unai Emery mipango yake ya sasa ni kunyakua wachezaji ambao watakifanya kikosi chake kuwa na kiwango bora kabisa kwenye michuano mikubwa ikiwamo ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Staa huyo mzaliwa wa Mar del Plata amechezea mechi moja tu ya timu ya taifa ya Argentina na umri wake ni miaka 27 bado ana kitu cha kufanya kwenye Ligi Kuu England, lakini kwa hali ilivyo haonekani kuwa na maisha Villa Park. Haitashangaza akifunguliwa mlango wa kutokea kwenye dirisha la Januari.


Bournemouth – Philip Billing

Hakuna ubishi kwamba kikosi cha Bournemouth kilikuwa na mvuto mkubwa wa kukitazama chini ya kocha Andoni Iraola, lakini mtu mmoja ambaye haonekani kuwa kwenye mipango ya kocha huyo Mhispaniola ni Philip Billing, mchezaji ambaye Leeds United ilionyesha dhamira ya kuhitaji saini yake hadi katika dakika za mwisho za kufungwa kwa dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi. Bado kuna timu zinahitaji saini ya mchezaji huyo na huenda zikafanya kweli wakati dirisha la Januari litakapofunguliwa. Jambo hilo linafanya Bournemouth kuwa na nafasi nzuri ya kumuuza pale dirisha litakapofunguliwa.


Brentford – Ben Mee

Ni mchezaji mwenye uzoefu kwenye Ligi Kuu England, hivyo kubaki na huduma ya Ben Mee kutakuwa na faida kubwa kwenye kikosi cha Brentford. Lakini, umri wa mchezaji huyo unakuwa mkubwa, hivyo hata huduma yake ndani ya uwanja inapungua ubora wake, kitu ambacho kitaifanya timu yake kufikiria mpango wa kuachana naye kwenye dirisha la Januari. Mee amekuwa akihusishwa na Burnley na huenda akashawishika na mpango wa kurudi zake kuichezea miamba hiyo ya Turf Moor endapo kama atafunguliwa mlango wa kutokea na Brentford kwenye uhamisho wa Januari.


Brighton – Tariq Lamptey

Kuondoka Brighton & Hove Albion bila shaka ni kitu kinachotarajiwa kutokea kwa mchezaji Tariq Lamptey, ambaye huko nyuma uwezo wake wa uwanjani ulimfanya ahusishwe sana na timu za Big Six. Ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa cha soka, lakini tatizo linalomkabili ni kusumbuliwa sana na majeraha ya mara kwa mara na hilo ndilo litakalomfanya afunguliwe mlango wa kutokea wakati wa dirisha la Januari litakapofungulia ili akajaribu maisha kwingineko baada ya hapo Brighton kuonekana kuwa na bahati mbaya upande wake kutokana na kuwa majeruhi mara kwa mara.


Chelsea – Ben Chilwell

Maisha yake yametibuka huko Chelsea baada ya kuibuka kwa kiwango bora cha Marc Cucurella. Kwenye beki ya kushoto ya Chelsea, Ben Chilwell sasa haonekani kama ana umuhimu wowote licha ya kuwa mmoja wa mabeki wanaolipwa mshahara mkubwa kwenye Ligi Kuu England. Hakuna maana kwamba kiwango cha mkali huyo wa zamani wa Leicester City ni kibaya sana, lakini kinachoonekana ni kwamba kocha Enzo Maresca tayari amekuwa na machaguo yake katika upangaji wa kikosi chake huko Stamford Bridge, hivyo hakutakuwa na mshangao, Ben Chilwell akifunguliwa mlango wa kutokea Januari.


Crystal Palace – Rob Holding

Rob Holding uhamisho wake wa kwenda Crystal Palace ulionekana kama ni wa faida kwa pande zote mbili. Palace iliamini inanasa mchezaji mwenye uzoefu wa kutosha kwenye safu ya ulinzi ili kuwafanya kuwa imara zaidi kwenye eneo hilo. Lakini, mambo yamekuwa tofauti kabisa na beki huyo ameshindwa kabisa kwenda kufanya kitu cha kipekee katika kikosi hicho cha Selhurst Park na kujiweka kwenye orodha ya wachezaji ambao wanaweza kufunguliwa mlango wa kutokea kwenye dirisha la Januari ili wakajaribu maisha kwingineko.


Everton – Beto

Aliwasili kwenye kikosi cha Everton mwaka 2023 akitokea Udinese ya Italia, mchezaji Beto amekuwa hana maajabu sana kwenye kikosi hicho alipokuwa akicheza chini ya Sean Dyche. Mchezaji Dominic Calvert-Lewin, licha ya kupunguza makali yake kwenye kufunga mabao, lakini amekuwa akipewa nafasi ya kucheza mbele ya staa huyo wa kimataifa wa Guinea-Bissau. Beto amecheza dakika 180 tu kwenye Ligi Kuu England, jambo ambalo halionekani kama ana maisha mazuri kwenye kikosi hicho na huenda akafunguliwa mlango wa kutokea wakati wa dirisha la Januari litakapofunguliwa.


Fulham - Ryan Sessegnon

Thamani ya Ryan Sessegnon huko Fulham ni kubwa. Alikuwa miongoni mwa mastaa wa England kwa Under-19 ambao walishinda ubingwa wa Ulaya kwa timu za vijana Euro 2017. Lakini, staa huyo mzaliwa wa London bado hajafikia viwango vilivyotarajiwa baada ya kucheza kikosi cha wakubwa akitokea kwenye akademia ya Fulham. Uhamisho wake wa Tottenham, uliofuatia wa mkopo Hoffenheim haikuwa na matunda makubwa kabla ya kurudi Craven Cottage kwenye dirisha lililopita la uhamisho wa majira ya kiangazi. Msimu huu amecheza dakika nne tu kwenye ligi, hivyo Januari anaweza kubadili timu.


Ipswich Town - Harry Clarke

Baada ya kuwa na mechi yake ya kwanza ya hovyo wakati wa mchezo dhidi ya Brentford mwanzoni mwa msimu huu 2024/25, beki Harry Clarke huenda akawa ametibua maisha yake kuwamo kwenye mipango ya kocha Kieran McKenna. Umri wake bado mdogo na ana hamu kubwa ya kucheza soka, hivyo kuhama hapo na kwenda kupambania maisha kwingineko ni kitu ambacho kinaweza kuwa na maana kubwa kwa mchezaji huyo endapo kama ataamua kubadili timu kwenye dirisha la Januari na kuachana na Tractor Boys, mahali ambako amekuwa na wakati mgumu wa kumshawishi kocha kupata nafasi ya kucheza.


Leicester City - Patson Daka

Tangu iliporejea kwenye Ligi Kuu England, Leicester City imekuwa na nyakati ngumu sana na kushuhudia mambo yao mengi yakienda hovyo ndani ya uwanja. Kikosi hicho kwa sasa kipo chini ya kocha Ruud van Nistelrooy alipokuja kuchukua mikoba ya Steve Cooper. Kwenye kikosi hicho kuna mchezaji Patson Daka, maisha yake yametibuka sana kutokana na kusumbuliwa na majeraha, kitu ambacho kinaweza kumfungulia milango ya kutokea wakati dirisha la uhamisho wa Januari litakapofunguliwa. Kwa hali ilivyo, Daka anaweza kuwa mmoja wa mastaa watakaofunguliwa milango ya kutokea huko King Power.


Liverpool - Wataru Endo

Kocha, Arne Slot amewafanya wachezaji wa Liverpool kupandisha viwango vyao na kuifanya timu hiyo kucheza kwenye viwango bora kabisa, ikiwamo wachezaji Curtis Jones, Cody Gakpo na wengine kibao. Lakini, mchezaji mmoja ambaye amekuwa na bahati mbaya kutokana na ujio wa Mdachi huyo ni Wataru Endo. Kiungo huyo wa kati alipokuwa kwenye ubora wake asingekuwa mchezaji wa kumfikiria hatima yake kwenye kikosi cha Anfield. Lakini, kwa sasa mambo yalivyo kwa mchezaji huyo bila shaka haitakuwa inashangaza endapo Endo atafunguliwa milango ya kutokea Januari.


Man City - James McAtee

Kile ambacho kilitokea kwa Cole Palmer kuhama kutoka Manchester City kwenda Chelsea kinaweza kutokea pia kwa mchezaji James McAtee, 22, ambapo mchezaji huyo akaachana na miamba hiyo ya Etihad kwenda kujaribu maisha kwingineko. Kipaji cha mchezaji huyo hakina mjadala, lakini maisha hayaonekani kuwa na mwendelezo kwenye kikosi cha Man City na ndiyo maana kuna uwezekano mkubwa wa kufungulia mlango wa kutokea Januari.


Man Utd - Antony

Kuna wachezaji wengi sana watanufaika na ujio wa kocha Ruben Amorim kwenye kikosi cha Manchester United, ambaye amekuwa akitoa nafasi ya kucheza kwa kila mchezaji kuonyesha ubora wake, lakini mambo yanaweza kwenda kombo kwa Antony. Staa huyo mara zote alizopewa nafasi ya kucheza, kiwango chake kilikuwa hakina ushawishi na hilo linaweza kumponza kwa kipindi hiki ambacho dirisha la usajili wa Januari linatarajiwa kufunguliwa. Kocha huyo mpya wa United atahitaji kuleta nyota wapya kwenye timu na hilo kufanyika, kuna wachezaji watalazimika kuondoka na anaweza kuwa Antony.


Newcastle - Miguel Almiron

Kuna nyakati Miguel Almiron alikuwa kwenye kiwango bora sana Newcastle United, mfano msimu wa 2022/23 wakati alipofunga mabao 11 na kuasisti mara nne. Lakini, mambo yalibadilika na sasa mchezaji huyo si muhimu sana, akiwa hana uhakika wa nafasi ya kucheza kwenye kikosi hicho cha St James’ Park. Klabu ya Charlotte FC ya Marekani ilionyesha dhamira ya kuhitaji saini yake hivi karibuni, kitu ambacho kinawafanya Newcastle kufikiria mpango wa kumpiga bei na pengine hilo linaweza kufanyika kwenye dirisha la uhamisho wa Januari.


Nottingham Forest - Taiwo Awoniyi

Staa huyo mwenye kimo kirefu na kuzuia tishio kwenye Ligi Kuu England ni moja ya wachezaji muhimu ambao wamefunga mabao 17 katika mechi 64, lakini sasa anaweza kufunguliwa mlango wa kutokea. Kutokana na Chris Wood kuonyesha kiwango bora kabisa kwenye kufunga mabao, jambo hilo linamweka Taiwo Awoniyi, 27, kwenye wakati mgumu wa kupata nafasi ya kucheza kitu ambacho kinafungua mlango kwa mkali huyo kufikiria kubadili timu wakati dirisha la uhamisho wa majira ya baridi litakapofunguliwa mapema Januari.


Southampton - Paul Onuachu

Russell Martin alikuwa hapendi kumtumia Paul Onuachu na kumpanga straika huyo uwanjani kwa dakika 151 tu tangu mwanzoni mwa msimu. Kwa sasa matumaini ya mshambuliaji huyo yapo kwa kocha mpya Ivan Juric, lakini hakitakuwa kitu cha kushangaza kama ataamua kubadili timu kwenye dirisha la Januari. Southampton inaweza kuwa na tatizo kwenye safu yao ya ushambuliaji, lakini uwepo wa Cameron Archer na Adam Armstrong unaipa timu hiyo makali ya kutosha na hivyo kufanya uwezekano wa Onuachu kuondoka kwenye kikosi hicho cha St Mary’s.


Tottenham Hotspur – Sergio Reguilon

Uhamisho wa mkopo Manchester United ulionekana kufufua upya maisha ya soka ya beki huyo wa kushoto, lakini miamba hiyo ya Old Trafford haikutaka kuendelea na huduma yake na hivyo kumfanya Sergio Reguilon abaki kuwa njiapanda. Ameshindwa kumshawishi kocha Ange Postecoglou na hivyo kujikuta akisugua tu benchi huko Tottenham Hotspur. Mhitimu huyo wa akademia ya Real Madrid, hakuna ubishi kwamba ni mwenye kipaji kikubwa, lakini mambo yake hayaendi kwenye timu anayochezea kwa sasa na endapo ataamua kuhama Spurs kwenye dirisha la Januari halitakuwa jambo la kushtua watu.


West Ham United - Andy Irving

Kulikuwa na mpango wa kumpiga bei mchezaji wa safu ya ushambuliaji huku nyuma kama vile Danny Ings - kabla ya Michail Antonio kuumia, lakini sasa West Ham mambo yamebadilika na huenda kiungo wa Scotland, Andy Irving akahusika kwenye mastaa watakaofunguliwa mlango wa kutokea kwenye dirisha la Januari. Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 24 ameichezea timu yake mara sita tu tangu alipotua majira ya kiangazi 2023 na ameshindwa kupenya na kupata nafasi kwenye kikosi cha kwanza. Irving alikuwa kwenye mipango ya timu nyingi sana kwenye dirisha lililopita, hivyo isishangaze akiuzwa Januari.


Wolves - Sasa Kalajdzic

Staa huyo wa kimataifa wa Austria si tu ameshindwa kufanya kweli kwenye Ligi Kuu England akiwa na kikosi cha Wolves, lakini ni majeraha ndiyo yaliyomtibulia mkali huyo. Mambo yamekuwa hovyo kwa mkali huyo, ambapo kwa sasa amekumbwa na maumivu ya goti ambayo yanamfanya kuwa nje ya uwanja kwa muda mrefu baada ya kuichezea dakika 45 tu Wolves. Haifahamiki kama kocha mpya Ivan Juric atakuwa na mipango naye, lakini ni mmoja wa wachezaji ambao hadi dirisha la usajili wa Januari likifungwa na bado akiwa kwenye timu yake ya sasa, basi atakuwa mwenye bahati kubwa.