Afrika Kusini yatoka sare WAFCON
Muktasari:
- Mechi hiyo inakuwa ya pili kwa timu hizo, Banyana Banyana kwenye mechi ya kwanza ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania huku Ivory Coast ikiitandika Burkina Faso mabao 4-1.
AFRIKA Kusini imetoka sare ya 2-2 dhidi ya Ivory Coast kwenye mechi ya kundi B ya fainali za Kombe la Mataifa ya Afika kwa Wanawake WAFCON iliyopigwa Uwanja wa Rabat Olympic.
Mechi hiyo inakuwa ya pili kwa timu hizo, Banyana Banyana kwenye mechi ya kwanza ilipoteza kwa mabao 2-1 dhidi ya Tanzania huku Ivory Coast ikiitandika Burkina Faso mabao 4-1.
Ivory Coast ilitangulia kupata mabao yote mawili na hadi kipindi cha kwanza kinatamatika timu hiyo ilikuwa inaongoza kwa mabao 2-0.
Ivory Coast ilipata bao la kwanza kupitia kwa Grace Sery dakika ya 18 na 36 kabla ya baadae washambuliaji wa Banyana kufunga bao la kwanza kupitia kwa Thembi Kgatlana dakika ya 71 na lile la pili lililowapa pointi moja likifungwa na Hildah Magaia dakika ya 90.
Kabla ya Banyana kurudisha mabao hayo Ivory Coast ilikuwa iko vizuri kwenye kila eneo kuanzia pasi, kumiliki mpira hadi kwenye mashuti yaliyolenga lango.
Ivory Coast ilimiliki mpira kwa asilimia 63.5 dhidi ya 33.5 ya Afrika Kusini, Banyana ilipiga mashuti mawili yaliyolenga lango huku wapinzani wake wakipiga 11.
Kwa matokeo hayo sasa yanaifanya Ivory Coast iendele kusalia kileleni mwa kundi B ikiwa na pointi nne, Tanzania iliyocheza mechi moja ikiwa nafasi ya pili na pointi tatu, Afrika Kusini nafasi ya tatu na pointi moja.