Don Carlo: Hii ndo Brazil mpya
Muktasari:
- Moja ya mada alizozizungumzia ni kulinganisha Brazil na Hispania, mabingwa wa sasa wa dunia akikiri kwamba Wahispaniola wamefanikiwa kutokana na kuwa na kizazi bora cha viungo wa kati akiwataja Rodri, Pedri, Fabian Ruiz, Dani Olmo, Martín Zubimendi, Mikel Merino na Gavi.
BRASILIA, BRAZIL: KOCHA wa timu ya taifa ya Brazil, Carlo Ancelotti ametumia fursa ya kurejea nchini humo baada ya mapumziko mafupi kufuatia kuondolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia kueleza dira anayotaka waifuate miaka ijayo.
Akizungumza kupitia mahojiano na Jornal Nacional ya TV Globo, ESPN na AP, kocha huyo Muitaliano ambaye atabaki kuinoa Brazil hadi 2030 baada ya kukataa ofa ya kuifundisha Italia, amesema kipigo dhidi ya Norway kilichowaondoa katika fainali za Kombe la Dunia 2026 kinaashiria mwisho wa kizazi kimoja na mwanzo wa mchakato wa kujenga kikosi kipya kinachotegemea vijana.
Moja ya mada alizozizungumzia ni kulinganisha Brazil na Hispania, mabingwa wa sasa wa dunia akikiri kwamba Wahispaniola wamefanikiwa kutokana na kuwa na kizazi bora cha viungo wa kati akiwataja Rodri, Pedri, Fabian Ruiz, Dani Olmo, Martín Zubimendi, Mikel Merino na Gavi.
Hata hivyo, aliweka wazi kuwa Brazil haina haja ya kuiga mfumo wa Hispania wala Ufaransa na badala yake timu hiyo inapaswa kutambua maeneo ambayo yanahitaji kuboreshwa akisisitiza kwamba kiungo ndilo linalohitaji kazi zaidi, huku akiamini safu ya ulinzi na ushambuliaji kuna ubora wa kutosha.
Kutokana na hali hiyo amesema michezo ya Olimpiki ya Los Angeles 2028 ni sehemu muhimu ya mradi wake wa kuijenga upya Brazil.
Alikumbusha kuwa wachezaji wanane walioipa Hispania medali ya dhahabu katika Olimpiki za Tokyo 2020 kwa kuifunga Brazil katika fainali, hivi sasa ni sehemu ya kikosi kilichotwaa Kombe la Dunia mwaka huu.
Kwa upande wa Brazil, ni Bruno Guimaraes na Matheus Cunha pekee kati ya kikosi hicho cha Olimpiki waliocheza kwenye Kombe la Dunia 2026.
Kwa mujibu wa Ancelotti, tofauti hiyo inaonyesha umuhimu wa kufanya kazi kwa karibu na timu za vijana za chini ya umri wa miaka 15, 17 na 20, ambazo tayari zimetoa vipaji kama Rayan, Endrick, Estevao na Vitor Reis.
"Baada ya kushindwa ni muhimu kutafakari kilichotokea na kuangalia kwa makini siku zijazo. Tutaunda kikosi kipya chenye wachezaji vijana," amesema Ancelotti.
Kocha huyo pia amesema anataka kuondoa utamaduni wa Brazil kutegemea mchezaji mmoja nyota, badala yake kujenga timu inayocheza kwa ushirikiano, huku ikiendelea kutumia kasi na uwezo wa kubadili mchezo wa wachezaji kama Vincius Junior, Endrick, Estevao na Raphinha ili kuifanya icheze soka la kushambulia kwa kasi zaidi.
Katika mchakato huo wa mabadiliko, Ancelotti alithibitisha kuwa safari ya Neymar katika timu ya taifa imefikia mwisho akimpongeza kwa kujitolea licha ya majeraha yaliyomzuia kucheza kwa kiwango alichotamani kwenye Kombe la Dunia.
Kwa upande wake amesema kuondolewa kwenye fainali za Kombe la Dunia kulimuumiza zaidi kuliko kushindwa alikowahi kupitia akiwa kocha wa klabu, kwa sababu safari hii hana nafasi ya kulipiza kisasi haraka kupitia mechi inayofuata.