Wachezaji 46, Alonso ana kazi nzito Chelsea
Muktasari:
- Tangu atue Chelsea mwanzoni mwa Julai, Alonso tayari ameongoza usajili wa nyota kadhaa akiwemo Morgan Rogers aliyenunuliwa kwa ada ya Pauni117 milioni, pamoja na Marco Palestra, Danny Welbeck, Maxence Lacroix na Jordan Henderson.
LONDON, England: KOCHA mpya wa Chelsea, Xabi Alonso, anakabiliwa na moja ya changamoto kubwa zaidi tangu aanze kazi Stamford Bridge baada ya kujikuta akisuka kikosi chenye jumla ya wachezaji 46 wa timu ya kwanza, huku idadi hiyo ikitarajiwa kuongezeka kutokana na usajili mpya.
Tangu atue Chelsea mwanzoni mwa Julai, Alonso tayari ameongoza usajili wa nyota kadhaa akiwemo Morgan Rogers aliyenunuliwa kwa ada ya Pauni117 milioni, pamoja na Marco Palestra, Danny Welbeck, Maxence Lacroix na Jordan Henderson.
Hata hivyo, tofauti na kasi ya usajili, idadi ya walioondoka klabuni ni ndogo. Hadi sasa, Marc Cucurella amehamia Real Madrid moja kwa moja, Tyrique George ameuzwa Everton, huku Alejandro Garnacho, Jesse Derry na Kendry Paez wakitolewa kwa mkopo.
ALONSO AANZA KAZI YA KUPUNGUZA KIKOSI
Kutokana na msongamano huo, Alonso atalazimika kupunguza idadi ya wachezaji kabla ya kuanza kwa msimu wa Ligi Kuu England.
Kocha huyo Mhispania anatakiwa kufanya maamuzi magumu ili kuepuka kurejea kwa kile kilichoitwa 'bomb squad', mfumo uliotumiwa na aliyekuwa kocha wa Chelsea, Enzo Maresca.
Chini ya Maresca, wachezaji waliokuwa hawapo kwenye mipango ya benchi la ufundi walitengwa na kikosi cha kwanza, wakifanya mazoezi tofauti na hata kutumia vyumba tofauti vya kubadilishia nguo.
Miongoni mwa nyota waliowahi kutengwa ni Raheem Sterling, Axel Disasi, Joao Felix na Ben Chilwell.
USHINDANI MKALI KILA NAFASI
Chelsea inatarajiwa kuanza kampeni ya Ligi Kuu Agosti 24, lakini kabla ya hapo uongozi wa klabu unapaswa kuharakisha mikopo na mauzo ya baadhi ya wachezaji.
Katika baadhi ya nafasi, hadi wachezaji wanane wanashindania nafasi moja ya kuanza kikosini.
Safu ya ushambuliaji ndiyo iliyojaa zaidi baada ya kurejea kwa Nicolas Jackson kutoka mkopo Bayern Munich, huku mshambuliaji chipukizi wa Kazakhstan, Dastan Satpayev akijiunga rasmi mwezi huu baada ya kusajiliwa mwaka 2025.
Aidha, Emmanuel Emegha, aliyesajiliwa kutoka Strasbourg, atachuana na Danny Welbeck, Marc Guiu, Liam Delap na Joao Pedro katika kutafuta nafasi ya kucheza.
VIJANA NAO WAONGEZWA KIKOSINI
Mbali na usajili mpya, Alonso pia amewapa nafasi vijana kadhaa wa akademi wakati wa ziara ya maandalizi ya msimu nchini Australia na Asia.
Miongoni mwao ni Reggie Watson, Reggie Walsh, Ryan Kavuma-McQueen, Calvin Diakite, Olutaro Subuloye, Mahdi Nicoll-Jazuli, Landon Emenalo na Ted Curd, waliopata nafasi ya kujionyesha kutokana na baadhi ya nyota wa kikosi cha kwanza kuwa walikuwa kwenye majukumu ya Kombe la Dunia.
MUDRYK AREJEA, MAAMUZI YAZIDI KUWA MAGUMU
Changamoto nyingine kwa Alonso ni kurejea kwa Mykhailo Mudryk, ambaye ameruhusiwa tena kucheza baada ya kesi yake ya matumizi ya dawa zilizokatazwa kufungwa.
Hata hivyo, Chelsea tayari imeanza kupokea ofa kwa baadhi ya wachezaji wake.
Klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo na Como kuhusu Trevoh Chalobah, huku Crystal Palace na West Ham zikimwania Axel Disasi. Naye Benoit Badiashile amevutia Napoli.
Kwa upande wa kiungo Enzo Fernandez, Chelsea haina mpango wa kumuachia kirahisi na imeweka dau la Pauni milioni 120, licha ya Real Madrid kuendelea kufuatilia hali yake.
Mudryk pia anatajwa kuvutia klabu tatu za Ligi Kuu England baada ya kurejea rasmi uwanjani.
Kwa idadi kubwa ya wachezaji na ushindani mkali ndani ya kikosi, Alonso sasa ana kazi ya kufanya maamuzi magumu ya nani abaki, nani aondoke na nani apewe nafasi ya kuiongoza Chelsea kuelekea msimu mpya.