Waache wauwane! Vita kali ya Arsenal, Man City msimamo EPL
Muktasari:
- Lakini, kitu kitamu zaidi, Arsenal na Man City zinaweza kujikuta zikicheza zenyewe mara tano ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, huku wapinzani hao wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England wakichuana kuwania mataji mbalimbali.
LONDON, ENGLAND: NDO hivyo. Arsenal na Manchester City weka niweke. Miamba hiyo imetofautiana pointi sita tu kwenye msimamo wa Ligi Kuu England, jambo linaloashiria kuwapo kwa vita kali katika kusaka ubingwa wa ligi hiyo kwa msimu huu.
Lakini, kitu kitamu zaidi, Arsenal na Man City zinaweza kujikuta zikicheza zenyewe mara tano ndani ya kipindi cha mwezi mmoja, huku wapinzani hao wa mbio za ubingwa wa Ligi Kuu England wakichuana kuwania mataji mbalimbali.
Arsenal inaongoza msimamo wa Ligi Kuu England kwa tofauti ya pointi sita tu, kufuatia ushindi wa kusisimua wa Man City wa mabao 2-1 dhidi ya Liverpool, Jumapili usiku uwanjani Anfield.
Kikosi cha Mikel Arteta kiko kwenye mkondo wa kukutana na Man City, kikijua kuwa kitakabiliana na ufundi wa kocha Pep Guardiola angalau mara mbili msimu huu.
Kwanza, Arsenal itacheza na Man City kwenye fainali ya Kombe la Carabao, Machi 22, ambapo taji la kwanza la msimu litakuwa linapigiwa hesabu. Baada ya hapo, Arsenal itasafiri hadi Uwanja wa Etihad, Aprili 18 katika mechi muhimu sana ya kuamua mbio za ubingwa wa ligi.
Hata hivyo, kuna uwezekano timu hizo zikakutana kabla ya hapo, kwani raundi ya tano ya Kombe la FA itachezwa mwishoni mwa wiki ya Machi 7/8. Timu zote mbili bado zipo kwenye michuano hiyo, huku Arsenal ikiwakaribisha Wigan na Man City ikisafiri kwenda kucheza dhidi ya Salford. Robo fainali za Kombe la FA zitafanyika Aprili 4/5, nusu fainali Aprili 25/26 na fainali ni Mei 16.
Timu hizi pia zinaweza kukutana kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, kwani zote zilifuzu moja kwa moja hadi hatua ya 16 bora.
Hazitakutana kwenye raundi inayofuata, lakini zinaweza kukutana kwenye robo fainali ya mikondo miwili itakayochezwa Aprili 7/8 na Aprili 14/15. Pia kuna uwezekano mkubwa zikatenganishwa hadi fainali za Kombe la FA au Ligi ya Mabingwa, iwapo zote zitaendelea kusonga mbele kwenye michuano hiyo.
Kocha wa Man City, Guardiola, alizungumza kuhusu uwezekano wa kukutana na Arsenal mara kadhaa kabla ya mwisho wa msimu, wakati aliposema: “Inaweza kutokea. Sijui kitakachotokea kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, huku kwenye Ligi Kuu, ratiba ipo wazi.
“Wakati timu bora zinapofika hatua za mwisho, unaweza kukutana nazo. Napenda hilo, hasa unapocheza fainali.”
Arsenal ina kiu kubwa ya kukomesha ukame wa miaka 22 bila kutwaa taji la Ligi Kuu England, ikipambana na jambo hilo huku ikitambua mtihani unaowakabili kukabiliana na wapinzani wao wakubwa Man City.
Man City waliinyima Arsenal ubingwa mara mbili katika misimu mitatu iliyopita, kwanza msimu wa 2022–23, ambapo Arsenal ilikuwa ikiongoza ligi kwa pointi nane. Hata hivyo, kikosi cha Guardiola kilifanikiwa kutwaa taji hilo kwa tofauti ya pointi nne, kabla ya kuwashinda tena Arsenal kwa tofauti ya pointi mbili msimu wa 2023–24.
Arsenal kisha ilipambana na Liverpool katika mbio za ubingwa msimu uliopita, lakini ilimaliza na pointi 74, pointi kumi nyuma ya miamba ya Anfield, ambayo ilibeba taji la Ligi Kuu England ikiwa ni msimu wa kwanza wa kocha Arne Slot na taji lao la pili katika miaka 36.