JKT yaongeza nguvu kwenye ushambuliaji
Muktasari:
- Mshambuliaji huyo aliwahi kuwa mfungaji bora wa michuano ya CECAFA chini ya miaka 17, hatua iliyomuweka kwenye ramani ya soka la wanawake na kuonyesha mapema uwezo wake wa kufunga katika mashindano ya ushindani.
INAELEZWA JKT Queens iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji kinda wa Bunda Queens, Bahati Steven kwa mkataba wa miaka miwili.
Bahati anajiunga na JKT Queens akiwa mmoja wa wachezaji vijana walioonyesha uwezo mkubwa katika misimu ya hivi karibuni.
Mshambuliaji huyo aliwahi kuwa mfungaji bora wa michuano ya CECAFA chini ya miaka 17, hatua iliyomuweka kwenye ramani ya soka la wanawake na kuonyesha mapema uwezo wake wa kufunga katika mashindano ya ushindani.
Mbali na mafanikio yake katika ngazi ya vijana, Bahati amekuwa na msimu mzuri akiwa na Bunda Queens, akitumia nafasi hiyo kujitengenezea uzoefu katika Ligi Kuu Wanawake Tanzania Bara.
Bahati ambaye alikuwa nchini Morocco kwenye michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwaka huu, akicheza katika mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi dhidi ya Ivory Coast.
Chanzo kililiambia Mwanaspoti ipo kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji huyo kinda ambaye inaamini atakuwa na msimu mzuri.
"Eneo la ushambuliaji kuna wachezaji wengi lakini kama ilivyo kawaida ya JKT kuchukua wachezaji vijana ambao wamecheza ligi na kuwaamini na kuwapa nafasi zaidi," kilisema chanzo hiko na kuongeza;
"Mambo yakikamilika Bahati atakuwa sehemu ya kikosi chetu kwa sababu ni mchezaji mzuri bado mdogo na tuna imani hapa atakuwa salama na sehemu sahihi ya kuendeleza kipaji chake."
Bahati anajiunga na JKT wakati ambao eneo hilo lina wachezaji kama Winifrida Gerald, Stumai Abdallah, Jamila Rajabu ambao wamekuwa na kiwango bora dani ya misimu mfululizo.