Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Man City yakataa ofa ya Barcelona kwa Rodri

FUNUNU Pict

Muktasari:

  • Rodri, mwenye umri wa miaka 30, ameingia katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na City, lakini bado hajakubaliana na klabu hiyo kuhusu mkataba mpya.

MANCHESTER, ENGLAND: MANCHESTER City imekataa ofa ya awali ya Pauni38.5 milioni kutoka Barcelona kwa ajili ya kiungo wake wa kimataifa wa Hispania, Rodri, huku mabingwa hao wa England wakisisitiza kuwa hawatamuuza mchezaji huyo kwa chini ya Pauni60 milioni.

Rodri, mwenye umri wa miaka 30, ameingia katika mwaka wa mwisho wa mkataba wake na City, lakini bado hajakubaliana na klabu hiyo kuhusu mkataba mpya.

Hali hiyo imeongeza uvumi kuhusu mustakabali wake msimu huu wa kiangazi, huku klabu kadhaa zikifuatilia kwa karibu kinachoendelea Uwanja wa Etihad.

Awali ilionekana Real Madrid ndiyo iliyokuwa na nafasi kubwa ya kumsajili Rodri, lakini sasa Barcelona imeibuka kuwa kinara katika mbio za kumpata kiungo huyo.

Barcelona tayari imepata ridhaa ya Rodri kuanza mazungumzo na Manchester City kuhusu uhamisho wake.

Siku iliyofuata, Barcelona iliwasilisha ofa yake ya kwanza ya pauni38.5 milioni, lakini City ikaikataa kwa madai kuwa haitoshelezi thamani wanayomuwekea mchezaji huyo.

Taarifa zinaeleza kuwa Barcelona bado inaendelea na mazungumzo na wawakilishi wa Rodri, huku klabu hiyo ikiwa na matumaini ya kufikia makubaliano.

Manchester City sasa iko kwenye wakati muhimu kuhusu mustakabali wa Rodri.

Klabu hiyo inaweza kumuuza kwa zaidi ya pauni60 milioni katika dirisha hili na kupata fedha kubwa, hasa ikizingatiwa kuwa mkataba wake unamalizika.

Kwa upande mwingine, Barcelona inaonekana kuwa tayari imeanza harakati za kumsogeza Rodri Camp Nou, huku uamuzi wa mwisho ukitegemea iwapo itakuwa tayari kuongeza ofa yake hadi kufikia kiwango ambacho City inakitaka.


ENDRICK

Wawakilishi wa mshambuliaji wa Real Madrid, Endrick, wamewasiliana na Chelsea kuhusu uwezekano wa mchezaji huyo kuhamia Stamford Bridge.

Kwa mujibu wa TeamTalk, mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Brazil mwenye umri wa miaka 20 ana wasiwasi kuhusu nafasi yake katika kikosi cha Real Madrid chini ya kocha mpya, Jose Mourinho. Wasiwasi huo umeongezeka baada ya Real Madrid kumsajili Carlos Espi pamoja na Yan Diomande, jambo linaloweza kuongeza ushindani katika safu ya ushambuliaji ya kikosi hicho.

Chelsea inatajwa kuwa imekuwa ikimfuatilia Endrick kwa muda mrefu na inaendelea kuvutiwa na uwezo wa mshambuliaji huyo.


GERONIMO RULLI

MANCHESTER City imefikia makubaliano ya kumsajili kipa wa Argentina, Geronimo Rulli, kutoka Marseille kwa ada ya pauni 1.7 milioni.

Rulli, mwenye umri wa miaka 34, anarejea Etihad ambako aliwahi kuwa sehemu ya kikosi cha City msimu wa 2016/17, ingawa hakupata nafasi ya kucheza mechi yoyote katika kikosi cha kwanza.

Kipa huyo amesaini mkataba wa miaka miwili na miamba hao wa England na sasa anatarajiwa kuwa msaidizi wa kipa namba moja, Gianluigi Donnarumma.


CONOR GALLAGHER

Klabu ya Besiktas ya Uturuki imewasilisha ofa ya kutaka kumsajili kwa mkopo kiungo wa Tottenham, Conor Gallagher, ikiwa ni miezi michache tu baada ya mchezaji huyo kujiunga na Spurs. Gallagher alijiunga na Tottenham akitokea Atletico Madrid mwezi Januari mwaka huu na amecheza mechi 18 tangu kuwasili kwake.

Hata hivyo, mustakabali wake katika kikosi hicho umeanza kuwa shakani baada ya Tottenham kuongeza nguvu katika safu ya kiungo kwa kumsajili Sandro Tonali na Mateus Fernandes.


AYYOUB BOUADDI

Manchester City iko hatua za mwisho kukamilisha usajili wa kiungo wa Lille, Ayyoub Bouaddi, katika dili linalotajwa kuwa karibu kukamilika.

Bouaddi, raia wa Morocco, ameonekana kuwa mmoja wa wachezaji wanaolengwa na City kama mbadala wa kiungo wake Rodri, ambaye anahusishwa na uwezekano wa kuhamia Barcelona.

Kwa mujibu wa taarifa za Fabrizio Romano, mazungumzo kati ya Manchester City na Lille yamefikia hatua za mwisho, huku makubaliano kati ya klabu hizo yakitarajiwa kupatikana muda wowote.

Usajili wa Bouaddi ukikamilika, utakuwa hatua nyingine ya City kujiandaa kwa uwezekano wa kuondoka kwa Rodri, ambaye amekuwa mhimili muhimu katika safu ya kiungo ya kikosi hicho.



RONALD ARAUJO

Liverpool imeendelea kufanya usajili wa nguvu katika dirisha hili la usajili baada ya kufikia makubaliano ya kumchukua kwa mkopo beki wa kati wa Barcelona, Ronald Araujo.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa Fabrizio Romano, Liverpool imekubali kugharamia mshahara wote wa beki huyo raia wa Uruguay katika kipindi cha mkopo. Dili hilo pia limeweka kipengele cha Liverpool kuwa na fursa ya kumsajili moja kwa moja Araujo kwa ada ya euro55 milioni baada ya kumalizika kwa kipindi cha mkopo.

Usajili huo unaendelea kuonyesha nia ya Liverpool kuimarisha kikosi chake kwa wachezaji wenye uwezo mkubwa kuelekea msimu ujao.


JOAO PALHINHA

Aston Villa imeingia kwenye mazungumzo na Bayern Munich kuhusu kumsajili kiungo wa kimataifa wa Ureno, Joao Palhinha, katika dirisha hili la usajili. Mkurugenzi wa masuala ya usajili wa Aston Villa, Damian Vidagany, amethibitisha kuwa klabu hiyo ipo kwenye mazungumzo na Bayern Munich kuhusu uwezekano wa kumsajili Palhinha.

Palhinha, 30, alitumia msimu uliopita kwa mkopo katika klabu ya Tottenham Hotspur, lakini sasa anaonekana kuwa njiani kuachana na Bayern Munich.


ROMELU LUKAKU

Fenerbahce iko kwenye hatua za mwisho kukamilisha usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa Ubelgiji, Romelu Lukaku, kutoka Napoli. Lukaku, mwenye umri wa miaka 33, anatarajiwa kujiunga na Fenerbahce katika uhamisho wa moja kwa moja baada ya klabu hiyo ya Uturuki kufikia hatua ya mwisho ya mazungumzo na Napoli.

Uhamisho huo pia utaigusa Chelsea, ambayo inatarajiwa kunufaika kwa kupata sehemu ya fedha kutokana na kipengele cha mgao wa mauzo kilichowekwa kwenye mkataba wa awali wa Lukaku.


TIMOTHEE PEMBELE

Beki wa pembeni wa Sunderland, Timothee Pembele, ameondoka katika klabu hiyo na kujiunga na Le Havre ya Ufaransa kwa uhamisho wa moja kwa moja. Pembele, mwenye umri wa miaka 23, alijiunga na Sunderland akitokea Paris Saint-Germain (PSG) Septemba 2023, lakini alikumbwa na changamoto za utimamu wa mwili zilizomfanya ashindwe kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza.

Katika kipindi chake Sunderland, beki huyo aliichezea timu hiyo mechi nane pekee za kikosi cha kwanza.


FERRAN TORRES

Mshambuliaji wa Barcelona, Ferran Torres, amekubaliana kwa mdomo masharti binafsi ya kujiunga na Paris Saint-Germain (PSG), hatua inayomweka karibu na kuhamia miamba hiyo ya Ligue 1.

Torres, ambaye amewahi kuhusishwa na uhamisho kwenda Arsenal pamoja na klabu nyingine kadhaa, sasa anaonekana kuwa kwenye njia ya kuachana na Barcelona na kujiunga na mabingwa hao wa Ufaransa.

PSG pia imeifahamisha Barcelona kuwa inatarajia kuwasilisha ofa rasmi ya kumsajili Torres hivi karibuni, huku mazungumzo ya moja kwa moja kati ya klabu hizo yakitarajiwa kushika kasi katika siku chache zijazo.