Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba, miaka tisini na dakika tisini bado hakijaeleweka

JICHO Pict (1)


MIAKA tisini ya Simba imetimizwa juzi. Kumbe Gen Z hawakujua kwamba Simba iimetimiza miaka 90 hapo juzi. Walidhani Simba ni timu ya juzi juzi tu. Hata hivyo, sidhani kama wamechelewa sana kuijua Simba. Hata wao wenyewe wanaweza wanaweza kuitengeza Simba mpya.


Wanaweza kuitengeneza Simba ambayo haijawahi kuwepo. Simba tofauti ya ndani na nje ya uwanja. Simba ilianzishwa mwaka 1936 lakini haijawahi kuwa na maajabu makubwa sana ambayo mashabiki wapya wa Simba hawawezi kufanya. Kuna mambo mengi kando yake.


Kwa mfano, katika miaka tisini ya Simba klabu hii haijawahi kumilliki uwanja wake. Hapa Bunju walikuja juzi juzi tu kutengeneza uwanja wa mazoezi lakini wao kama wao hawajawahi kumiliki uwanja wao wa mazoezi wala mechi kwa miaka yote hii. Afadhali huu wa mazoezi wamejikomboa lakini kitu kinachoitwa uwanja wao wa mechi za nyumbani hawajawahi kuwa nao.

JICH 01

Watani zao wamewahi kuwa na uwanja wao. Uwanja wa Kaunda. Sijui waliupataje na wakaupa jina la Rais wa kwanza wa Zambia, Kenneth Kaunda. Kiukweli haukuwa uwanja wa maana lakini tukubali tu kwamba walikuwa nao. Nasikia wanataka kujenga uwanja wa kisasa katika eneo hilo. Acha tusubiri kama kweli wanaweza kufanya hivyo.

Katika miaka tisini ya Simba bado wapo katika jengo ambalo lipo pale Msimbazi. Ni makao makuu ya timu yao lakini hadhi yake hailingani sana na ukubwa wa jina la timu. Pale hakuna vikao au kikao ambacho wanaweza kuendesha mambo yao ya kila siku. Ni ukweli mchungu lakini nitazungumza kitu hapo mbele kidogo. Ngoja kwanza tuendelee na mengine kwa sasa. Wanafanya vikao vyao katika ofisi ambayo ipo katikati ya mji.

Ndani ya uwanja, Simba inasuasua kwa sasa. Lakini kabla ya kusuasua kwa sasa, kitu ambacho ni kawaida kwa timu nyingi tu duniani, ukweli ni kwamba historia bado haipo vizuri sana. Kwa mujibu wa rekodi wamewahi kufika nusu fainali za ligi ya mabingwa mwaka 1974 wakiwa katika muundo ambao haulingani na huu wa leo. Walicheza na Mehalla El Kubra.

JICH 02

Vinginevyo Simba wamefika robo fainali za michuano ya ligi ya mabingwa mara nyingi mfululizo hapa katikati. Walifika fainali za michuano ya washindi ya CAF mwaka 1993 kabla ya kufika fainali za Shirikisho msimu mmoja nyuma. Wamefika robo fainali za ligi ya mabingwa mfululizo katika miaka ya karibuni. Bado hatuwezi sana kulinganisha umri wao na mafanikio yao ingawa katika hali ya kawaida unaweza kusema wanafanya vema.

Pamoja na yote haya bado unaweza kuwasifu Simba katika mengineyo mengi. Kwa mfano. Jina la Simba lipo lipo sana katika ramani ya mpira wa Afrika. Sawa, hauwezi kuwaweka katika viwango vya akina Al Ahly, Waydad Casablanca, Raja, Mamelodi Sundowns, TP Mazembe na wengineo lakini Simba wapo wapo sana. Haishangazi sana ukienda kuzurura Cairo au Casablanca halafu shabiki wa mpira wa huko akakwambia hajui lolote kuhusu Simba. Sio kweli.

Kuna alama nyingi anbazo Simba imeacha nyuma yake. Kufika hatua za mbele za michuano hii kama hii ya ligi ya mabingwa wa Afrika hauwezi kutoacha alama ya jina. Lakini sisahau namna ambavyo Simba walimtoa bingwa mtetezi wa ligi ya mabingwa wa Afrika Zamalek mwaka 2003 pale Cairo na wakatinga hatua ya mtoano.

JICH 03

Simba wapo wapo sana. Wao, kama ilivyo kwa watani zao ni watu ambao wanasikika sana. Simba unaweza kuwapeleka hatua kadhaa mbele ya mtani katika mafanikio ya michuano ya Afrika. Hata hivyo, ukilinganisha umri wao na mafanikio yao bado unahisi unawadai kwa kiasi kikubwa. Wakati mwingine ni namna ambavyo unaweza kuwalinganisha na timu ambazo zilizaliwa baada ya wao.

Watanzania wanapenda sana soka. Wamenyimwa mipango tu na watu ambao wanaongoza timu zao. Kuna timu nyingi ambazo zimezaliwa baada ya Simba na Yanga na tayari zimefanya mambo makubwa. Mifano ni mingi. Mamelodi Sundowns imeanzishwa mwaka 1970 na Simba imeanzishwa mwaka 1936. Kaizer Chiefs pia wameanzishwa mwaka 1970 wakati Simba imeanzishwa mwaka 1936.

Mifano ya timu ambazo zimechelewa kuzaliwa na  zimefanya makubwa mbele ya  wakubwa wetu katika mafanikio ni mingi. Kinachopaswa kufanyika kwa sasa ni kutumia ukubwa wetu katika kupata mafanikio ndani na nje ya dakika tisini. Miaka tisini ya Simba iendane na ukubwa wa klabu lakini pia na umri wa klabu yenyewe.

JICH 04

Kwa tulikotoka ukweli upo wazi kwamba Simba wamepiga hatua nyingi. Ni kweli kwamba Simba ya leo sio ile ya akina Marehemu Juma Salumu au Amri Bamchawi. Simba ya leo inasajili wachezaji mahiri kwa mabilioni ya pesa. Simba ya leo wachezaji na timu kwa ujumla wanalelewa vizuri.  Simba ya leo malezi yake ni tofauti ni zama za akina Abdalah Kibadeni au baadaye akina Zamoyoni Mogella kisha akina Clatous Chotta Chama.

Tatizo ni kwamba kuna tofauti kubwa ya kati ya rasilimali walizonazo dhidi ya maendeleo yenyewe. Tunazungumzia umri wao na idadi ya mashabiki walionao. Matazamio ni kwamba timu iende mbali zaidi na kwa kasi zaidi. Simba kama walivyo watani zao Yanga wana rasilimali kubwa ambayo klabu nyingi zingetamani kuwa nayo. Mashabiki.

Umri wa klabu sio tatizo sana. Kuna klabu ambazo zina umri mkubwa lakini zimetokea katika nchi ambazo hazina ushabiki mkubwa wa mpira. Haisaidii kuona timu ina umri mkubwa lakini inatoka India au China. Hawana mashabiki wengi wa mpira na ni vigumu kutumia kigezo cha umri wa klabu katika kupata mafanikio. Lakini Tanzania wakongwe wetu wana kila kitu.

JICH 05

Wakongwe wetu wanaweza kujivunia kuwa na klabu ambazo zina umri mkubwa lakini pia wamejikuta katika nchi ambayo ina mashabiki wenye wehu mkubwa wa ushabiki na mchezo wenyewe. Ni fursa nzuri kibiashara na kuifanya timu kuwa tishio ndani na nje ya uwanja. Na hili ndio jukumu ambalo watu wanaoiongoza Simba kwa sasa.

Kama ambao wanaiongoza Simba hawawezi kutimiza hilo basi sio mbaya wakiwapisisha vijana wa kizazi kipya wafanye kazi hiyo.  Simba imeng'ang'aniwa na watu wengi wa zamani ambao sidhani kama wanaweza kuipeleka katika mkondo mwingine wa maisha. Yanahitajika mawazo mapya na watu wapya kwa ajili ya kupambana na kasi ya dunia. Walichofanya sio kibaya lakini tunahitaji watu ambao wanaweza kupambana na kasi.

Miaka tisini ya Simba ni mingi. Hongera sana kwao kwa kuwepowepo katika ramani ya mpira wa Afrika. Wengi wameshindwa hapo njiani lakini miaka mingi peke yake haina maana yoyote kama haiendani na mafanikio ndani na nje ya uwanja hasa kwa nchi ambayo ina mashabiki walio wehu katika soka.

Hili pia nitalisema kwa watani wao. Yanga. Na wao hawawezi kusalimika katika hili kwa sababu ni mapacha. Hakuna ambacho huku kipo na kule hakipo. Wote tunawadai. Kuna mahala wametuangusha na inabidi waamke zaidi. Ni kweli hawapo kama zamani lakini inabidi waongeze kasi zaidi. Ni kweli kila siku tunaendelea kujivunia wao lakini waongeze kasi zaidi.