Viungo wa pauni 150 milioni kuibeba man united
Muktasari:
- Ingawa safu hiyo mpya huenda isiwafanye mashabiki wengi wa Manchester United kusisimka mara moja, viongozi wa klabu hiyo wanaamini wamefanya biashara nzuri katika soko la usajili, hasa kutokana na gharama kubwa za viungo bora katika kipindi hiki.
LONDON, ENGLAND: MANCHESTER United imefanya maboresho makubwa katika eneo la kiungo msimu huu, ikikamilisha mpango wa kuingiza wachezaji wapya watatu kwa gharama ya zaidi ya pauni150 milioni, huku kocha Michael Carrick akitarajia kuanza kibarua chake leo ugenini dhidi ya Hull mechi ya kwanza ya Ligi Kuu England.
Ingawa safu hiyo mpya huenda isiwafanye mashabiki wengi wa Manchester United kusisimka mara moja, viongozi wa klabu hiyo wanaamini wamefanya biashara nzuri katika soko la usajili, hasa kutokana na gharama kubwa za viungo bora katika kipindi hiki.
Man United ilikuwa ikimuwania Elliot Anderson, lakini kiungo huyo alihamia Manchester City kwa ada ya pauni 116milioni. Pia, ilimfuatilia Mateus Fernandes na Sandro Tonali, ambao baadaye walijiunga na Tottenham kwa jumla ya karibu pauni 185milioni.
Kwa upande mwingine, mabingwa Arsenal wamefanikiwa kumsajili Bruno Guimaraes kwa pauni75 milioni.
Hivyo, Manchester United kukamilisha ujenzi upya wa kiungo kwa wachezaji watatu kwa kiasi kinachozidi kidogo tu gharama ambayo ingetumia kumsajili Anderson, kunaonekana kuwa uamuzi wa busara.
Swali kubwa sasa ni kama Andrey Santos, Youri Tielemans na Carlos Baleba wa Brighton wataweza kuipa United ubora na kina kinachohitajika katika eneo hilo.
Baada ya kukamilisha usajili wa wachezaji wawili wa kwanza mapema, kwa wiki kadhaa kulikuwa na sintofahamu kuhusu kama United ingemalizia usajili wa kiungo wa tatu.
Majina kadhaa yalihusishwa na klabu hiyo, yakiwamo Aurelien Tchouameni, Alex Scott, Sander Berge, Manu Kone na Tyler Adams. Kwa wakati mmoja, ilionekana huenda United ikaamua kutosajili mchezaji mwingine au kumtafuta chaguo la gharama nafuu.
Hivyo, kuwa katika hatua za mwisho za kumsajili Baleba ni habari njema kwa Carrick, hasa ikizingatiwa kuwa Brighton waliwahi kumthaminisha kiungo huyo kwa karibu pauni112 milioni msimu uliopita.
Carrick, ambaye alitumia miaka 12 katika eneo la kiungo la Manchester United akiwa mchezaji, anatarajiwa kuwa na uwezo wa kutambua ubora wa kiungo anayemhitaji kwenye kikosi chake.
Kwa Tielemans, mwenye umri wa miaka 29, United inapata mchezaji mwenye uzoefu wa Ligi Kuu England, baada ya kucheza nchini humo kwa miaka saba.
Matumaini ya Carrick ni kwamba kiungo huyo raia wa Ubelgiji atatumia uzoefu na uwezo wake wa kiufundi kupunguza mzigo kwa nahodha Bruno Fernandes, ambaye mara nyingi amekuwa tegemeo kubwa la timu hiyo.
Man United pia itakuwa na mechi zisizopungua nane zaidi msimu huu, na huenda zikawa nyingi zaidi, kutokana na ushiriki wake katika mashindano mbalimbali baada ya msimu uliopita kufanya vibaya kwenye makombe ya ndani.
Hivyo, haitakuwa busara kuendelea kumtegemea Fernandes kila wiki kama ilivyokuwa katika nyakati kadhaa msimu uliopita.
Katika Baleba na Santos, ambao wote wana umri wa miaka 22, United imechagua wachezaji vijana wanaoweza kuwa sehemu muhimu ya kikosi kwa miaka mingi ijayo.
Ingawa wawili hao hawakuwa na misimu mzuri katika klabu zao msimu uliopita, Carrick bado ana chaguo jingine ndani ya kikosi.
Kobbie Mainoo, ambaye sasa amesaini mkataba wa muda mrefu na kurejea kwenye mipango ya timu baada ya kuonekana kama angeondoka mwanzoni mwa mwaka, anaongeza nguvu na nguvu kazi katika eneo hilo.
Manuel Ugarte, kwa upande mwingine, atakaa nje kwa miezi kadhaa baada ya kupata jeraha la mishipa ya goti wakati wa Kombe la Dunia. Hata hivyo, akirejea fiti, huenda United ikamruhusu kuondoka.
Pia, kuna Mason Mount, ambaye changamoto yake kubwa imekuwa kukaa fiti, pamoja na kinda wa Scotland, Tyler Fletcher, ambao wanaweza kuongeza chaguo zaidi kwenye safu hiyo.
Msimu uliopita, Manchester United ilitumia sehemu kubwa ya bajeti yake ya usajili kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Bryan Mbuemo, Matheus Cunha na Benjamin Sesko hawakuwa katika kiwango kilekile kila wiki, huku kila mmoja akiwa na vipindi vya kufanya vizuri na vingine vya kutokuwa bora.
Hata hivyo, kwa ujumla dirisha hilo la usajili lilionekana kuwa na mafanikio kwa United na lilisaidia timu hiyo kumaliza katika nafasi nne za juu ikiwa na nafasi nzuri.
Ikiwa wachezaji watatu wapya wa kiungo watafanya vizuri kama ilivyofanya safu ya usajili wa majira ya kiangazi iliyopita, Manchester United inaweza kuwa imepiga hatua nyingine muhimu katika ujenzi wa kikosi chake.
Huenda kikosi hicho bado kisiwe na nguvu ya kuipa changamoto Arsenal, ambayo kwa sasa inaonekana kuwa na moja ya safu bora zaidi za viungo barani Ulaya.
Lakini Manchester United inatumai maboresho hayo yatakuwa hatua nyingine muhimu kuelekea kutimiza mpango wa ‘Project 150’ na lengo la kurejesha ubingwa wa Ligi Kuu England ifikapo mwaka 2028.