Kutsanedzi: Kujiunga Simba ni fursa, heshima, ndoto zitatimia
Muktasari:
- Anasema hamu yake kubvwa ni kuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachocheza michuano ya CECAFA inayotarajiwa kufanyika Rwanda.
MIONGONI mwa wachezaji wapya waliosajiliwa na Simba Queens msimu huu basi ni beki wa kushoto, Hellen Kutsanedzi, aliyejiunga kwa mkataba wa miaka miwili akitokea FC Epiphany Warriors ya Ghana.
Safari yake hadi Tanzania si tukuhama klabu, bali kutimiza ndoto yake ya kukua na kufanikiwa kisoka Afrika.
Mwanaspoti lilifanya mahojiano na beki ambaye amezungumzia safari yake kisoka hadi kufika Tanzania.
“Nimekuwa nikiamini soka linaweza kunibadilishia maisha kama ilivyo kwa wanamichezo wengine, hata ilipotokea ofa ya Simba sikusita kwa sababu ni klabu inayojulikana Afrika,” anasema beki huyo na kuongeza wiki tatu alizokaa Dar es Salaam ameanza kuzoea mazingira mapya pamoja na wachezaji wenzake.
Anasema hamu yake kubvwa ni kuwa sehemu ya kikosi cha Simba kitakachocheza michuano ya CECAFA inayotarajiwa kufanyika Rwanda.
DILI LA SIMBA
Kutsanedzi anasema alipigiwa simu na mmoja wa viongozi wa Simba anahitajika kujiunga na timu hiyo, wakati huo alikuwa ameshamalizana na klabu yake ya Ghana.
“Nakumbuka nilikuwa nyumbani wakati simu inapigwa, nilivyozungumza na viongozi wa Simba nikagundua wana malengo makubwa, hivyo nikajisemea ninaweza kuwa sehemu ya mafanikio hayo. Sikuwahi kucheza nje ya nchi yangu ila nilikubali kutokana na ushawishi wa viongozi,”
TANZANIA NYUMBANI
Kutsanedzi anakiri kuhamia nchi nyingine si jambo rahisi, hasa kwa mchezaji anayelazimika kuanza kuzoea mazingira mapya, watu wapya na mfumo mpya wa soka.
“Unapotoka katika nchi moja kwenda nyingine, mambo yanabadilika. Si kama kuhama mkoa; hapa ni nchi tofauti. Lakini mazingira ni mazuri na najitahidi kuzoea mfumo haraka iwezekanavyo,” anasema na kuongeza;
“Watu wa hapa wana upendo sana ikiwemo wewe umenipokea vizuri sikutarajia, naamini kwa hiki nilichoonyeshwa kitanisaidia kukuza karia yangu na kunitimizia malengo niliyoyaweka kwenye soka na nje ya kazi yangu.”
KWA NINI SIMBA?
Kabla ya kukubali kujiunga Tanzania, anasema alifanya utafiti kuhusu Simba Queens na historia yake kwenye soka la wanawake na hapo ndipo alipofanya maamuzi yake.
“Ninahisi vizuri sana kujiunga na Simba Queens. Hii ni fursa kubwa na ni heshima kwangu kuwa hapa kusaidia kile ambacho tayari wanacho,” anasema Kutsanedzi.
Anaongeza: “Nilisoma mengi kuhusu Simba kabla ya kuja. Wanashinda ligi mara kwa mara. Nimekuja kuongeza nguvu ili tuendelee kushinda, kushinda na kushinda naamini kwa muendelezo huu nitatimiza na mimi ndoto yangu.”
CHANGAMOTO
Safari ya Kutsanedzi kwenye soka haikuwa rahisi, hasa kutokana na changamoto ambazo wanawake wanaocheza mchezo huo wamekuwa wakikabiliana nazo katika baadhi ya jamii.
“Changamoto ni nyingi. Kama mchezaji wa kike, ni vigumu sana ukilinganisha na wanaume. Fursa kwa wanaume zipo nyingi, lakini kwa wanawake watu husema, ‘Wewe ni mwanamke, unapaswa kuwa jikoni na mambo kama hayo’,” anasimulia.
Beki huyo anasema kauli hizo hazikumfanya arudi nyuma bali kuendelea kufanya zaidi na ziliendelea kumjenga na kumfanya aamini kwamba anaweza kufanikiwa.
Anaongeza moja ya kauli anayoichukia ni baadhi ya watu kuwaita wachezaji wa kike mwanaume kisa tu anacheza mpira na hali hiyo amekutana nayo mara kwa mara kwao Ghana.
“Wakati mwingine unakosa hata chakula, unapaswa kusawazisha masomo na mpira. Si rahisi hata kidogo. Lakini kwa neema ya Mungu, tumeweza kupenya na bado tunasonga mbele,” anaongeza.
KUJIWEKA KIUME
Anaeleza kwa baadhi ya wachezaji kuvaa mavazi ya michezo mara kwa mara kunawafanya kuzoea hali hiyo kiasi cha kutotambua tena namna wanavyopaswa kuonekana au kujiweka katika mazingira tofauti na ya uwanjani.
“Sidhani kama ni suala muhimu sana, nafikiri hata wachezaji wanakuwa na mazoea kwa sababu ya kuvaa jezi. Wakati mwingine wanajikuta wanaendelea na mazoea hayo hata wanapokuwa sehemu nyingine za nyumbani, kwa sababu wamezoea kuwa kwenye mazingira ya mpira na kuvaa mavazi ya timu.”
SIRI YA KROSI ZAKE
Ni mmoja wa mabeki wa kisasa wenye uwezo wa kucheza pembeni kwa kasi, umbo, maarifa na uwezo wa kutengeneza nafasi za kufunga.
Mbali na sifa hizo pia ana uwezo mkubwa wa kupanda kusaidia mashambulizi na kupiga krosi zenye macho ambazo kama zikimkuta mshambuliaji mzuri anaweza kufunga mabao mengi.
Anaamini mchezaji anapokuwa na utulivu wa akili, anaweza kufanya maamuzi sahihi hata akiwa kwenye presha kubwa ya mashabiki, wapinzani au mechi muhimu.
WAZAZI WAKE NGUZO
“Watu wengi wamekuwa wakinisapoti, ikiwemo marafiki zangu bora, na nawashukuru sana kwa hilo lakini wazazi wangu sina cha kuwaambia zaidi ya kuwashukuru kwa kuniamini na kunisapoti,” anasema.
NAFASI YAKE
Nafasi anayocheza Kutsanedzi yupo Mtanzania, Asha Omary ambaye huu ni msimu wake wa pili kujiunga na Wana Lunyasi hao wa kike akitokea kwa wapinzani wao Yanga Princess.
Beki huyo anasema anafahamu ugumu atakaoupata kupata nafasi kikosini hapo na anapenda ushindani kwa sababu anaamini humsaidia mchezaji kujiboresha zaidi.
“Mimi huwa napenda chalenji kwa sababu siku zote humsaidia mchezaji na kumfanya asibweteke apambane zaidi nafahamu hata kabla sijaja hapa kwamba lazima nitakutana na ushindani na nipo tayari.”
AHADI CECAFA
Miongoni mwa mashindano anayoyasubiri kwa hamu ni mashindano ya CECAFA ambayo anaamini yatamsaidia kupata chalenji mpya na kujiuza kwa sababu ni michuano inayokutanisha timu mbalimbali.
“Naamini kwenye michuano mikubwa kama hii itanisaidia kama nitaonyesha kiwango bora na kusaidia timu kutimiza lengo la kubeba taji la CECAFA.”