Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Real Madrid mzigoni ikiulizwa mara tano

Muktasari:

Msimu mpya wa La Liga ulianza mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, Real Madrid hawakuanza pamoja na wengine, wakitarajiwa kuanza Jumamosi ijayo, Agosti 22.

MADRID, HISPANIA: JOSE Mourinho amerejea Real Madrid, Vinicius Junior amejifunga na klabu hiyo kwa mkataba mpya, huku Kylian Mbappe akitoka kushinda Kiatu cha Dhahabu katika Kombe la Dunia. Kuna maswali matano muhimu yanayopaswa kuulizwa kuhusu Real Madrid kuelekea msimu wa 2026/27.

Msimu mpya wa La Liga ulianza mwishoni mwa wiki iliyopita. Hata hivyo, Real Madrid hawakuanza pamoja na wengine, wakitarajiwa kuanza Jumamosi ijayo, Agosti 22.

Mchezo wao wa kwanza dhidi ya Espanyol uliahirishwa kama ilivyo kwa Barcelona, Athletic Club na Real Sociedad, kutokana na ushiriki wa wachezaji wao katika hatua za mwisho za Kombe la Dunia 2026 zilizopita.

Los Blancos watataka kuanza kwa kasi wakilenga kurejea kileleni mwa soka la Hispania. Kwa klabu ambayo haijawahi kuwa na aibu kujitangaza yenyewe, haikuwa picha nzuri kumaliza nyuma ya wapinzani wao wakubwa Barcelona katika mbio za ubingwa wa ligi kwa misimu miwili mfululizo. Ndiyo maana Mourinho amerejeshwa Santiago Bernabeu.

Mourinho yupo kwenye kiti cha ukocha kwa mara ya pili jijini Madrid, akiwa na jukumu la kuinyang’anya Barcelona ya Hansi Flick ubingwa na kuifanya Real Madrid kuwa mshindani wa kuaminika zaidi katika Ligi ya Mabingwa Ulaya kuliko ilivyokuwa katika misimu michache iliyopita. Pia kuna wachezaji wapya akiwemo Yan Diomande aliyesajiliwa kutoka RB Leipzig kwa ada ya mabilioni ya shilingi pamoja na beki wa kushoto kutoka Chelsea aliyeshinda Kombe la Dunia 2026 akiwa na Hispania na aliyewahi kupita akademi ya Barcelona, Marc Cucurella.

Real Madrid wanaweza kutarajia kufanikisha nini? Kama ilivyo kila msimu watataka kushinda kila kitu. Lakini, wana uwezekano upi wa kufanya hivyo? Kuna maswali matano kuhusu Real Madrid ambayo majibu yake yanaweza kuamua mashabiki watakuwa na furaha kiasi gani ifikapo mwishoni mwa Mei 2027.


MOURINHO ATAREJESHA MIUJIZA?

Amerejea! Mourinho aliondoka Real Madrid 2013, lakini miaka 13 baadaye klabu hiyo imemrejesha kocha huyo kutoka Ureno katika jaribio la kurejea kwenye mafanikio yake ya zamani. Lakini je, kocha huyo wa zamani wa Chelsea na Manchester United ataweza kuifanya Madrid kuwa mshindani katika ligi na Ligi ya Mabingwa msimu huu? Kipindi chake cha kwanza hakikuwa na mafanikio makubwa sana. Katika misimu yake mitatu alishinda Copa del Rey msimu wa kwanza, La Liga msimu wa pili na Supercopa de Espana pekee katika msimu wake wa tatu.

Hata hivyo, ubingwa wa msimu wa 2011/12 ulikuwa wa kuvutia sana. Real Madrid hawakuwa wameshinda La Liga tangu 2007/08, lakini walikusanya pointi 100 wakishinda michezo 32 ya La Liga, rekodi ya mashindano wakati huo ambayo Barcelona waliifikia msimu uliofuata. Pia walishinda michezo 16 ugenini, rekodi ambayo haijavunjwa. Baada ya kujijengea sifa kuwa miongoni mwa makocha bora wa kizazi chake katika vipindi vyake Porto, Chelsea mara mbili, Inter Milan, Real Madrid na Man United, kiwango chake kilishuka kwa kiasi katika vipindi vya Tottenham Hotspur, Roma, Fenerbahce na Benfica. Hata hivyo, akiwa Roma alishinda ubingwa wa kwanza wa timu hiuo wa UEFA Conference League.

Mambo hayakwenda vizuri kwa Real Madrid chini ya Xabi Alonso msimu uliopita baada ya miaka kadhaa ya mafanikio chini ya Carlo Ancelotti. Mara nyingi klabu hiyo imekuwa ikifanya vizuri zaidi inapokuwa na kocha ambaye huwaweka wachezaji wake bora katika hali nzuri na asiyeingilia sana mambo ya kiufundi.

Mourinho alionyesha kwamba bado ana uwezo wa kufanya makubwa pale inapohitajika. Benfica yake ilishinda mchezo wa kusisimua wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Madrid mjini Lisbon msimu uliopita kwa mabao 4-2, huku bao la nne la kuchelewa kutoka kwa kipa Anatoliy Trubin likiwapa nafasi ya kufuzu hatua ya mchujo. Hata hivyo, hawakuweza kurudia mafanikio hayo dhidi ya Los Blancos katika hatua hiyo, wakipoteza 3-1.

Lililo wazi ni kwamba timu alizofundisha ni ngumu kuzifunga. Benfica ilimaliza bila kupoteza mchezo katika msimu wa Primeira Liga 2025/26. Hata hivyo, hawakuwa wakali vya kutosha katika kushinda mechi. Sare 11 ziliwagharimu, kwani walilazimika kumaliza nafasi ya tatu nyuma ya Porto na Sporting CP. Labda kuwa na baadhi ya washambuliaji bora zaidi duniani kutamsaidia, jambo ambalo linatupeleka kwenye swali linalofuata.


ATAPATA UWIANO BORA SAFU YA USHAMBULIAJI?

Unapokuwa na safu ya ushambuliaji yenye Vinicius Junior na Kylian Mbappe, unafikiri, “tuna washambuliaji wawili bora zaidi duniani, tuna bahati kiasi gani?” Hapana. Unafikiri, “tunahitaji wa tatu!” Rodrygo akiwa majeruhi, Franco Mastantuono keshaenda Fiorentina kwa mkopo na Arda Güler kwa kiasi kikubwa akibadilishwa kuwa kiungo wa kati, kulikuwa na nafasi upande wa kulia wa safu ya ushambuliaji ya Real Madrid. Wameijaza kwa kumvuta Yan Diomande kutoka RB Leipzig.

Winga huyo wa Ivory Coast anaweza kukamilisha moja ya safu hatari zaidi za washambuliaji ambazo soka limeziona katika kipindi cha hivi karibuni. Vinícius hatimaye alibaki Madrid licha ya wiki kadhaa za kuvutiwa na Arsenal. Mbappe ametoka kufunga mabao 10 akiwa na Ufaransa katika Kombe la Dunia la 2026. Inawezekanaje watatu hawa wasiharibu kila kitu kitakachokuwa mbele yao msimu huu?

Hata hivyo, wakati Vinicius na Mbappe hawakuwa na tatizo la kufunga mabao msimu uliopita wakifunga 22 na 42 mtawalia katika mashindano yote kulikuwa na imani kwamba hawakufanya kazi pamoja vizuri kama walivyoweza. Pia iliaminika ukosefu wa mataji na kiwango cha kukatisha tamaa katika michezo mikubwa vinaweza kwa kiasi fulani kulaumiwa kutokana na safu ya ushambuliaji kutofanya vizuri wakati muhimu.

Kuongezwa kwa Diomande ambaye ni hodari wa kupiga chenga na akifunga mabao 13 na kutoa pasi za mabao tisa kwa Leipzig mashindano yote msimu uliopita matumaini ni kwamba timu pinzani zitakuwa na kazi ngumu.

Mourinho anaweza kuwa na sifa ya kuwa kocha anayesisitiza zaidi ulinzi wakati mwingine, lakini Real Madrid yake ilifunga mabao 121 katika michezo 38 ya ligi 2011/12, idadi kubwa zaidi iliyowahi kufungwa na timu katika msimu mmoja wa La Liga tangu 1929.

Katika msimu huo, Mourinho alipata kiwango bora kutoka kwa Cristiano Ronaldo, Gonzalo Higuain na Karim Benzema. Labda safari hii atafanya jambo kama hilo akiwa na Vinicius, Mbappe na Diomande.


BELLINGHAM AMERUDI KATIKA KIWANGO BORA?

Bellingham hakuwa mbaya msimu uliopita, lakini alikuwa chini ya kiwango chake cha juu sana cha awali. Mchezaji huyo wa zamani wa Borussia Dortmund alifunga mabao manane na kutoa asisti tano katika michezo 40 kwa Madrid msimu uliopita, bao moja tu zaidi ya aliyofunga katika mechi nane za Kombe la Dunia. Katika msimu wake wa kwanza Hispania, Bellingham alifunga mara 23 na kutoa asisti 13 akifuatiwa na mabao 14 na asisti 13 msimu wake wa pili. Hivyo, msimu uliopita ulikuwa na upungufu mkubwa wa uzalishaji wake.

Chini ya Thomas Tuchel, Bellingham alicheza kama namba 10 nyuma ya Harry Kane, na mfumo huo ulifanya kazi vizuri sana. Labda Mourinho atafikiria kumrudisha katika namba 10 msimu huu. Katika msimu wa 2025/26, alicheza dakika nyingi zaidi akiwa kiungo wa kati, huku akipanda karibu na mshambuliaji kwa asilimia 28 tu ya dakika zake za La Liga, ikilinganishwa na asilimia 71 wakati wa Kombe la Dunia. Je ni vyema kuwa na Bellingham aliye katika ubora akicheza nyuma ya Vinícius, Mbappe na Diomande?

USAJILI MPYA UTABAMBA?

Tayari tumezungumzia Yan Diomande. Ni Lamine Yamal pekee aliyekamilisha chenga 133 katika ligi tano bora za Ulaya msimu uliopita, aliyemzidi Diomande aliyekuwa nazo 118. Pia anafanya kazi kwa bidii bila mpira. Ni wachezaji tisa pekee kutoka ligi tano bora za Ulaya waliofikisha mpira katika theluthi ya mwisho ya eneo la wapinzani mara nyingi zaidi ya Diomande, aliyefanya hivyo mara 27.

Pia, kuna Marc Cucurella aliyesajiliwa muda mfupi kabla ya kwenda kushinda Kombe la Dunia. Denzel Dumfries ameongeza chaguo upande wa kulia baada ya kusajiliwa kutoka Inter Milan, huku Bernardo Silva na Ibrahima Konate wakitua kutoka Ligi Kuu England.

Diomande ni mchezaji anayesisimua, lakini kama kuna aina ya mchezaji ambaye Mourinho anampenda ni yule mwenye uzoefu, uelewa wa mchezo na ubora. Na ana kila kitu hicho kupitia usajili wa wachezaji hao wanne. Ni Moises Caicedo pekee aliyefanya takolingi 87 ndiye aliyemzidi Cucurella aliyekuwa nazo 55 kwa Chelsea katika EPL msimu uliopita. Wakati huohuo, Enzo Fernandez (61) na Pedro Neto (43) pekee ndio waliotengeneza nafasi nyingi zaidi za wazi kuliko beki huyo wa kushoto aliyefanya hivyo mara 37.

Dumfries ulikuwa usajili wa kuvutia. Kwa kweli, ingekuwa rahisi sana kuweka swali katika makala hii kuhusu jinsi Mourinho atakavyopata kiwango bora kutoka kwa Trent Alexander-Arnold, ambaye alikuwa na msimu wa kwanza wa kukatisha tamaa nchini Hispania. Lakini kuwasili kwa Mholanzi huyo anayependa kupanda mbele haijulikani kama mchezaji huyo wa zamani wa Liverpool atakuwa chaguo la mara kwa mara katika kikosi cha kwanza msimu huu.

Silva anawasili akiwa ameshinda mataji sita EPL akiwa na Manchester City, huku Konate akiwa pia bingwa wa England msimu mmoja uliopita akiwa Liverpool. Beki huyo wa kati wa Ufaransa alikuwa na msimu mbaya uliopita, lakini bado ni mchezaji mwenye nguvu katika mipambano ya ana kwa ana, hasa mipira ya juu. Ni Virgil van Dijk pekee aliyekuwa mshirika wake katika safu ya ulinzi aliyeshinda asilimia kubwa zaidi ya mipira ya juu EPL kuliko Konate msimu uliopita.

Pia kuna usajili wa Carlos Espi kutoka Levante aliyetua kuchukua nafasi ya Gonzalo Garcia kama mshambuliaji wa akiba wa Mbappe. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 alifunga mabao 11 katika michezo 25 La Liga msimu uliopita, manne kati yake yakiwa kwa kichwa. Miongoni mwa wachezaji waliofunga angalau mabao 10 katika La Liga 2025/26, ni Alexander Sorloth wa Atletico Madrid pekee aliyekuwa na asilimia kubwa zaidi ya mabao ya kichwa. Mourinho atakuwa na wachezaji wengi wa kufanya nao kazi, lakini je, ataweza kuwaunganisha vizuri na kuifanya timu iwe mshindani katika mashindano yote?


JE, ANAHITAJIKA MBADALA WA RODRI?

Usajili mmoja ambao unaonekana kuwakwepa Real Madrid ni wa kiungo wa Manchester City, Rodri, anayeonekana kwenda Barcelona. Ikiwa hilo litatokea, litakuwa pigo mara mbili kwa Madrid. Hata hivyo, haijulikani kama hilo linamaanisha Madrid watahitaji kutafuta chaguo jingine.

Tukubali ukweli, Real Madrid tayari wana baadhi ya viungo bora zaidi duniani. Bellingham anaweza kutumika juu zaidi, lakini Aurelien Tchouameni, Federico Valverde, Bernardo Silva, Arda Guler na Eduardo Camavinga ni kundi la kuvutia, huku mengi yakitarajiwa kutoka kwa kipaji chipukizi Thiago Pitarch. Je, Rodri anaweza kutengenezwa upya? Hapana. Lakini kuna wachezaji waliofanana naye zaidi msimu uliopita kwa kuzingatia viwango vya uzalishaji wao. Mchezaji kutoka ligi tano bora za Ulaya aliyefanana zaidi na Rodri msimu uliopita alikuwa Elliot Anderson, aliyejiunga na Manchester City. Wa pili aliyekuwa karibu zaidi? Tchouameni. Pia kuna Manuel Locatelli wa Juventus na Nico Gonzalez aliyekuwa msaidizi wa Rodri Manchester City. Kwa hiyo, unaweza kusema Madrid tayari wana Rodri nyumbani. Mpe Tchouameni imani kisha mzunguke na vipaji vikubwa vya Valverde, Silva, Guler, Camavinga na Pitarch. Kuna maswali mengi kuliko majibu Real Madrid kwa sasa, lakini kwa Mourinho kurejea kwenye usukani, jambo moja ambalo siyo rahisi kutokea ni msimu wa kuchosha.