Vinicius JR onyesha kidevu chake
Muktasari:
- Real Madrid iliifunga Deportivo La Coruna bao 1-0 katika mchezo huo wa kirafiki uliochezwa dhidi ya timu hiyo ya LaLiga, huku Brahim Diaz akifunga bao la ushindi katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza.
MADRID, HSPANIA: Vinicius Jr amecheza mechi yake ya kwanza kwa Real Madrid katika maandalizi ya msimu mpya, ikiwa pia ni mara yake ya kwanza kuonekana uwanjani tangu kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha umbo la kidevu.
Real Madrid iliifunga Deportivo La Coruna bao 1-0 katika mchezo huo wa kirafiki uliochezwa dhidi ya timu hiyo ya LaLiga, huku Brahim Diaz akifunga bao la ushindi katika muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza.
Vinicius Jr alianza mchezo huo kabla ya kutolewa dakika ya 71 na nafasi yake kuchukuliwa na Jorge Cestero, katika mchezo ambao ulikuwa wa kwanza kwake chini ya kocha mpya Jose Mourinho.
Licha ya kuonekana akiwa na sura mpya baada ya kufanyiwa upasuaji, Vinicius aliweza kufurahia ushindi huo uliowapa Real Madrid taji la Teresa Herrera Trophy.
Upasuaji wa mchezaji huyo wa Brazil ulifanyika wiki chache baada ya timu yake ya taifa kutolewa katika hatua ya 16 bora ya Kombe la Dunia na Norway.
Kwa mujibu wa chombo cha habari cha Brazil, TMC, Vinicius alielekea moja kwa moja kwa daktari bingwa wa ngozi mjini Goiania baada ya kurejea nchini humo kufuatia likizo fupi aliyotumia Ulaya pamoja na mpenzi wake wa mara kwa mara, Virginia Fonseca.
Picha kadhaa za Vinicius, mwenye umri wa miaka 26, zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii baada ya upasuaji zilionyesha mabadiliko makubwa ya sura yake na kuwashangaza mashabiki.
Katika picha nyingine iliyosambaa mtandaoni, Vinicius alionekana akiwa pamoja na Dk Alessandro Alarcao, aliyefanya upasuaji huo mjini Goiania.
Vinicius alifanyiwa utaratibu huo wa kitabibu unaotumia vijazaji maalumu (fillers) kurekebisha umbo la uso, kwa lengo la kufanya kidevu chake kionekane chenye umbo na uwazi zaidi baada ya kufanyiwa kejeli kuhusu muonekano wake wakati wa Kombe la Dunia.
Msimu huu wa kiangazi umekuwa wenye matukio mengi kwa Vinicius, ambaye awali alihusishwa na uwezekano wa kuondoka Real Madrid, huku Arsenal ikitajwa kuwa moja ya klabu zilizokuwa zikimuwania kutokana na kubakiwa na mwaka mmoja kwenye mkataba wake.
Hata hivyo, uwezekano wa kuhamia Ligi Kuu England ulifutika mapema mwezi huu baada ya Vinicius kusaini mkataba mpya wa miaka sita na Real Madrid, utakaomfanya aendelee kubaki Santiago Bernabeu hadi mwaka 2032.