Prime
Vinicius Jr ametupotezea muda, jikumbushe kumpuuza
Muktasari:
- Kuna huyu mwingine anaitwa Ricardo Kaka naye hakuwahi kucheza Ligi Kuu England. Nitahesabu wangapi wengine? Kina Roberto Carlos na Cafu hawakuwahi kucheza Ligi Kuu England. Subiri kidogo. Neymar hakuwahi kucheza Ligi Kuu Brazil na hana nafasi nyingine ya kufanya hivyo.
RONALDO di Lima hakuwahi kucheza Ligi Kuu England. Ronaldinho Gaucho hakuwahi kucheza Ligi Kuu England. Romario de Souza hakuwahi kucheza Ligi Kuu England. Rivaldo hakuwahi kucheza Ligi Kuu England.
Kuna huyu mwingine anaitwa Ricardo Kaka naye hakuwahi kucheza Ligi Kuu England. Nitahesabu wangapi wengine? Kina Roberto Carlos na Cafu hawakuwahi kucheza Ligi Kuu England. Subiri kidogo. Neymar hakuwahi kucheza Ligi Kuu Brazil na hana nafasi nyingine ya kufanya hivyo.
Nitahesabu wangapi wengine? Huwa haiji kwa bahati mbaya. Nilikuwa nawahesabu watoto watukutu wa Kibrizl ndani ya miaka 20 iliyopita. Siyo kwa bahati mbaya hawakwenda katika majiji ya London, Manchester au Liverpool kucheza mpira katika upande ule wa mfalme Charles. Kuna sababu.
Kucheza kwa Mfalme Charles sio jambo lao sana. Wanapenda kucheza Hispania. Kule kuna miji kama miji yao ya Brazil. Wanapenda kukaa katika fukwe za Barcelona, Ibiza, Mallorca na kwingineko. Fukwe ambazo zinawakumbusha kwao Brazil. Kule wana fukwe za Copacabana, Ipanema na nyinginezo.
Sio Wabrazil tu. Wachezaji wengi wa Amerika Kusini wanapenda kucheza Hispania. Na kama utawapa chaguo jingine la moyoni basi wanapenda pia kucheza Italia au Ufaransa. Kwa Mfalme Charles hawapendi kucheza. Lugha zinagongana na hali ya hewa sio ile ambayo wanaipenda. Wanakwenda kucheza basi tu kwa sababu ya noti.
Nilikuwa natazama tu namna Vinicius Junior alivyokuwa anajizungusha kusaini mkataba mpya. Angeenda wapi? Arsenal? Hapana. Niliandika hapa wiki mbili zilizopita sikumwona Vinicius akicheza Arsenal ambayo ni timu yangu. Sababu zilikuwa lukuki. Sababu ya kwanza ni hii hapa, watoto wa Amerika Kusini wanapenda kucheza Hispania. Wabrazil wanapenda kucheza Hispania.
Kuna mambo mengine mawili. Jambo la kwanza ni inawezekana kuna ukweli Arsenal walijaribu bahati yao kwa Vinicius. Pesa hiyo wanayo. Stan Kroenke ni mtu na pesa zake. Na sasa ameiingiza Arsenal katika Kundi la timu zinazotumia noti.
Mfano amelipa Pauni 75 milioni kwa ajili ya kuinasa saini ya Bruno Guimares. Ni kiasi kikubwa cha pesa kwa mchezaji mwenye umri wa miaka 28. Arsene Wenger katika ubora wake wa ubahili asingetoa kiasi hicho cha pesa.
Inawezekana kweli Kroenke alimtaka Vinicius. Lakini kuna asilimia kubwa Vinicius alitumia mwanya huo kupata dili nzuri pale Madrid. Sikumwona akiondoka Santiago Bernabeu kwenda Arsenal.
Kama angehusishwa na PSG ningeweza kudhania ingetokea. Angeweza kwenda kuishi Paris kama ambavyo iliwahi kutokea kwa Neymar kisha ikatokea kwa Lionel Messi. Kwa nyakati tofauti waliwahi kuondoka Catalunya wakaenda zao kuishi Paris.
Kama dili la Vinicius kwenda Arsenal lingetokea basi lingenishangaza sana. Sababu nyingine ya kushangaa kwangu ni ukweli wachezaji wakubwa wa Hispania huwa hawaendi kucheza England.
Wachezaji wa viwango vya dunia ambao wanatamba Hispania ni ngumu kwao kwenda England. Sio wale wa Amerika Kusini tu. Hata wa Ulaya wanaotamba Hispania huwa wanakuwa wazito kwenda England. Mfano ni kama kina Zinedine Zidane. Waliishia pale pale Hispania.
Wachezaji wanaotamba England ndio ambao huwa wanatimkia Hispania. Mfano ni Cristiano Ronaldo. Akiwa katika ubora wake wa hali ya juu kabisa katika Lgi Kuu England na jezi ya Manchester United ndugu zangu Real Madrid wakapita naye.
Thierry Henry pia baada ya kuwa bora Arsenal aliamua kutimkia Barcelona. Orodha ya wachezaji wa aina hii ni ndefu. Kina Phillipe Coutinho baada ya kuonyesha ubora mkubwa England wakaamua kusaliti kambi na kutimkia Hispania.
Ni nadra kwa wachezaji walio bora pale Hispania kutimkia England. Iliwahi kutokea kwa mchezaji kama Mesut Ozil lakini hakuwa katika Daraja la Ronaldo au Karim Benzema pale Real Madrid.
Kumleta Kylian Mbappe, Vinicius Junior au Lamine Yamal katika ligi kuu ya Mfalme Charles ni jambo gumu. Wangekuwa wao wanacheza England ungeweza kuona wakiondoka zao na kutimkia Hispania.
Vinicius alikuwa anatupotezea muda tu. Sikuona kama angeweza kuondoka zake jiji la Madrid na kwenda London. Sikuona. Ukitaka kujua hakuwa na mpango wa kuondoka Madrid angalia namna alivyosaini mkataba mrefu. Miaka sita.
Kwa pale yupo yupo sana. Labda baadaye kidogo PSG wanaweza kuingilia kati lakini sioni wakifanya hivyo kwa sababu wameunda timu ambayo inacheza kitimu zaidi kuliko kumtegemea mchezaji mmoja. Luis Enrique amefanya kazi nzuri pale Paris.
Kwingine ambako Vinicus anaweza kwenda baadaye ni labda AC Milan au Inter Milan. Hili litakuja pale ambapo umri utakuwa umesogea sana na uwezo utakuwa umepungua. Siku hizi Italia hakuna pesa. Ni sehemu ya wastaafu waliochoka au Watoto wa Kiingereza ambao wametemwa na timu kubwa za England.
Vinginevyo kila la kheri kwake. Kama angeenda Arsenal nadhani angepoteza pia nafasi ya kuchaguliwa kuwa mwanasoka bora wa dunia. Siku hizi wanasoka bora wa dunia huwa wanatoka Hispania. Baada ya miaka mingi ni Rodri tu ndiye ameweza kupenya kutoka katika Ligi Kuu England.
Kila la kheri kwa Vinicius. Kama Pele hakucheza England. Diego Maradona hakucheza England. Romario de Souza hakucheza England. Kwa nini yeye akajaribu kucheza England. Alikuwa anatupotezea muda tu wa kufuatilia habari zake. Alikuwa anataka kuitumia Arsenal kupata noti nyingi za Florentino Petez. Wala hakuwa na mpango na Arsenal.