Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Vijana wa Chelsea waidhalilisha Ajax

Muktasari:

  • Marc Guiu, mwenye umri wa miaka 19, alikuwa wa kwanza kufunga na kwa muda mfupi akawa mchezaji mchanga zaidi wa Chelsea kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa, katika dakika moja na sekunde 17 baada ya nahodha wa Ajax, Kenneth Taylor kutolewa kwa kadi nyekundu.

LONDON, ENGLAND: Chelsea imekuwa timu ya kwanza kwenye historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kuwa na wachezaji watatu vijana wenye umri chini ya miaka 20 waliofunga mabao katika mechi moja, baada ya kushinda 5–1 dhidi ya Ajax iliyokuwa dhaifu kwenye Uwanja wa Stamford Bridge, Oktoba 22, 2025.

Marc Guiu, mwenye umri wa miaka 19, alikuwa wa kwanza kufunga na kwa muda mfupi akawa mchezaji mchanga zaidi wa Chelsea kufunga bao katika Ligi ya Mabingwa, katika dakika moja na sekunde 17 baada ya nahodha wa Ajax, Kenneth Taylor kutolewa kwa kadi nyekundu.

Hata hivyo, rekodi ya Guiu ilivunjwa dakika 33 baadaye pale Estevão Willian, mwenye umri wa miaka 18, alipofunga penalti ya tatu kati ya tatu baada ya penalti za awali kufungwa na Enzo Fernández na Wout Weghorst, huku Moisés Caicedo akifunga shuti la mbali katika kipindi cha kwanza kilichokuwa na purukushani nyingi.

Chelsea ilifanya mabadiliko matatu wakati wa mapumziko, ikiwemo kumuingiza mshambuliaji Tyrique George, ambaye alifunga bao dakika tatu tu baada ya kuingia, na kuwa kijana wa tatu kufunga katika mechi hiyo.

Kiungo Reggie Walsh, mwenye umri wa miaka 17, naye alitokea benchi na kuwa mchezaji mdogo zaidi kuchezea Chelsea katika Ligi ya Mabingwa, na Muingereza wa pili mwenye umri mdogo zaidi baada ya Jack Wilshere alipokuwa Arsenal.

Ajax, waliowahi kuwa vigogo wa soka la Ulaya na kushinda taji hili mara nne, walicheza vibaya mno, huku kadi nyekundu ya Taylor kutokana na rafu ya juu na kuchelewa ikifungua milango ya maafa hayo.

Nidhamu mbaya iliendelea kuwaangusha. Weghorst, aliyekuwa amefunga penalti ya kwanza baada ya Tosin Adarabioyo kufanya madhambi, alifanya rafu nyingine mbaya dhidi ya Fernández ambaye alifunga penalti iliyofuata dakika ya 45.

Cha kushangaza zaidi, Ajax walitoa penalti nyingine baada ya Youri Baas kumkanyaga Estevão, na kijana huyo akafunga dakika ya sita ya muda wa nyongeza wa kipindi cha kwanza.

Baada ya George kufunga bao la tano, mechi ilipungua kasi kwa pande zote mbili ambapo kocha wa Chelsea, Enzo Maresca alianza kuwapumzisha wachezaji wake muhimu kama Caicedo, Fernández na Adarabioyo, na kufanya mabadiliko yote matano kufikia dakika ya 65.

Ajax, waliokuwa wababe wa zamani barani Ulaya, sasa wamepoteza mechi zote tatu za Ligi ya Mabingwa na wapo mkiani mwa jedwali la timu 36. Pia hawajapata ushindi katika mechi nne mfululizo kwenye michuano yote.

Kwa upande mwingine, Chelsea wamepata ushindi wa pili mfululizo barani Ulaya baada ya kupoteza mchezo wa kwanza dhidi ya Bayern Munich, na sasa wanajiandaa kusafiri kwenda Azerbaijan kumenyana na Qarabag.