Mchezaji afariki dunia baada ya kuanguka uwanjani
Muktasari:
- Ozor alianguka wakati wa mchezo wa Gusau/Ahlan Pre-season Cup uliokuwa ukifanyika katika Uwanja wa Muhammadu Dikko, Katsina, na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
MCHEZAJI wa Katsina United, Chinedu Ozor, amefariki dunia baada ya kuanguka ghafla uwanjani wakati wa mchezo wa maandalizi ya msimu dhidi ya Niger Tornadoes uliochezwa Jumanne mjini Katsina, Nigeria.
Ozor alianguka wakati wa mchezo wa Gusau/Ahlan Pre-season Cup uliokuwa ukifanyika katika Uwanja wa Muhammadu Dikko, Katsina, na kukimbizwa hospitalini kwa ajili ya matibabu.
Ofisa Habari wa Katsina United, Nasir Gide, amethibitisha tukio hilo, akisema mchezaji huyo alipelekwa katika hospitali iliyokuwa karibu ambako daktari alitangaza kuwa amefariki.
Gide alisema baada ya kupata taarifa ya polisi, mwili wa Ozor ulipelekwa katika Hospitali Kuu ya Katsina, ambako pia alitangazwa kuwa amefariki na baadaye kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
Hata hivyo, baadaye familia ilihitaji uthibitisho zaidi wa kitabibu kabla ya mwili kuendelea na taratibu za kuhifadhiwa, huku wahudumu wa afya wakiripoti kuona harakati kwenye mwili wake. Ozor alirudishwa katika kitengo cha uangalizi maalumu (ICU).
Taarifa hiyo ilisababisha kuibuka kwa madai kwamba mchezaji huyo alikuwa amerejea katika hali ya kawaida, lakini Katsina United imekanusha taarifa hizo.
Katika taarifa yake ya baadaye, klabu hiyo imesema licha ya juhudi zilizofanyika baada ya tukio hilo, Ozor alifariki dunia na kwamba taarifa zilizodai alikuwa amepata fahamu si za kweli.
Klabu hiyo imesema familia ya Ozor, ikiwa katika hali ya mshtuko na kutotaka kukata tamaa, iliomba uthibitisho zaidi wa kitabibu kabla ya mwili wake kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti.
“Tunajua jinsi ilivyo vigumu kukubali hili. Wachezaji wenzake wanaomboleza, marafiki zake wanaomboleza na klabu inaomboleza,” Katsina United imeeleza katika taarifa yake.
Heartland FC ya Owerri aliyowahi kuitumikia Ozor, pia imetoa salamu za rambirambi, ikisema mchezaji huyo amepigana vita nzuri lakini amefariki akiwa bado katika umri mdogo.
Tukio hilo pia limeibua mjadala kuhusu maandalizi ya kitabibu katika viwanja vya michezo nchini Nigeria.
Barau FC, ambayo ilikuwa miongoni mwa timu zilizoshiriki mashindano hayo ya maandalizi, imetangaza kujiondoa ikilalamikia kile ilichokiita kutokuwa na maandalizi mazuri kwa waandaaji na uamuzi wa kuendelea na mashindano licha ya tukio hilo.
Kifo cha Ozor kimekumbusha matukio mengine ya wachezaji na viongozi wa soka waliopoteza maisha wakiwa katika shughuli za mpira nchini Nigeria.
Tukio hilo limetokea karibu mwaka mmoja baada ya kifo cha aliyekuwa kocha msaidizi wa Shooting Stars, Akin Olowokere, aliyefariki dunia Agosti 11, 2025 baada ya kuanguka wakati wa mazoezi.
Mwaka 2020, Nasarawa United ilipoteza beki wake, Chineme Martins, aliyefariki dunia baada ya kuanguka wakati wa mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Katsina United.
Baada ya kifo cha Martins, Shirikisho la Soka Nigeria (NFF) liliagiza mechi za ligi zisichezwe katika maeneo ambayo hayakuwa na vifaa na wataalamu muhimu wa huduma za kwanza.
Pia, makamishna wa mechi na waandaaji wa mashindano waliagizwa kukagua na kuthibitisha uwepo wa huduma za kitabibu kabla ya mchezo kuruhusiwa kufanyika.
Tukio la Ozor sasa limeongeza tena maswali kuhusu usalama wa kiafya wa wachezaji, maandalizi ya huduma za dharura na kama viwanja vinapaswa kuwa na vifaa maalumu vya kuokoa maisha kabla ya kuruhusu mechi kuchezwa.