Vigogo Manchester City wamng’ang’ania Guehi
Muktasari:
- Hata hivyo, mabosi wa Man City hawapo tayari kutoa kiasi cha pesa kinachoweza kufikia Pauni 35 milioni ambacho Palace inakitaka ili kumuuza. Licha ya kuonyesha nia ya kutaka kumsajili hadi sasa taarifa zinadai Guehi hataki kujiunga na Man City badala yake anataka kwenda ama Liverpool au Arsenal ambazo pia zinamtaka.
MANCHESTER CITY inajiandaa kuwasilisha ofa ili kumsajili beki wa kati wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Marc Guehi, 25, kabla ya kufungwa dirisha la usajili la Januari.
Hata hivyo, mabosi wa Man City hawapo tayari kutoa kiasi cha pesa kinachoweza kufikia Pauni 35 milioni ambacho Palace inakitaka ili kumuuza. Licha ya kuonyesha nia ya kutaka kumsajili hadi sasa taarifa zinadai Guehi hataki kujiunga na Man City badala yake anataka kwenda ama Liverpool au Arsenal ambazo pia zinamtaka.
Wakati Man City ikionekana kuwekeza nguvu kwa ajili ya kumsajili, inadaiwa mkurugenzi wa michezo wa Bayern Munich, Max Eberl, amekuwa akifanya mawasiliano ya moja kwa moja na wawakilishi wa Guehi katika siku za karibuni, akijaribu kumshawishi ajiunge na mabingwa hao wa Ujerumani dirisha la kiangazi.
Ushindani wa timu hizo unaonekana kuwa unaweza kusababisha kuongezeka kwa bei ya Guehi tofauti na ile ya sasa ya Pauni 35 milioni.
Tangu kuanza msimu huu, Guehi amecheza mechi 33 za michuano yote na kufunga mabao matatu na asisti tatu.
Marcus Rashford
LICHA ya kuondoka kwa kocha Ruben Amorim, taarifa zinadai Manchester United haina mpango wa kumrudisha mshambuliaji wa kimataifa wa England, Marcus Rashford, 28, mwisho wa msimu huu, baada ya mkataba wake wa mkopo na Barcelona kumalizika.
Rashford aliondoka Old Trafford baada ya kupoteza nafasi ya mara kwa mara katika kikosi cha kwanza.Uongozi wa Man United unaamini ni bora kuendelea kujenga kikosi kipya bila Rashford.
Marcus Tavernier
NOTTINGHAM Forest imefanya mawasiliano ya awali kwa ajili ya kumsajili winga wa Bournemouth, Marcus Tavernier, 26, lakini klabu yake imeweka wazi kuwa haina mpango wa kumuuza kwa sasa.
Tavernier amekuwa mhimili muhimu katika kikosi cha Bournemouth kutokana na uwezo wake wa kucheza winga ya kulia na kushoto.
Hata hivyo, Forest haijakata tamaa na inataka kuweka mezani zaidi ya Pauni 30 milioni ambazo inaamini zinaweza kuishawishi Bournemouth kuwauzia fundi huyo.
Mathys Tel
TOTTENHAM Hotspur imezuia mawasiliano yote kuhusu mshambuliaji raia wa Ufaransa, Mathys Tel, 20, licha ya kuwepo kwa timu zinazotaka kumsajili kwa mkopo kama Paris FC.
Licha ya kutopata nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza cha Spurs, mabosi wa timu hiyo wanaamini Tel ni sehemu ya msingi wa mipango ya baadaye, hivyo hawapo tayari hata kusikiliza timu zinazomtaka. Mkataba wa Tel unamalizika 2031.
Alex Toth
BOURNEMOUTH inaendelea na mazungumzo na Ferencvaros kuhusu kumsajili kiungo wa klabu hiyo na Hungary, Alex Toth, 20, baada ya ofa ya awali ya Pauni 8.6 milioni kukataliwa.
Toth ana uwezo mkubwa wa kupandisha mashambulizi, na mara kadhaa maskauti wa timu kubwa wamekuwa wakimtazama katika Ligi Kuu Hungary.
Kwa sasa mazungumzo yanaendelea huku Bournemouth ikifikiria kuwasilisha ofa nyingine.
Tino Livramento
NEWCASTLE UNITED inataka kusajili beki wa kulia katika dirisha hili baada ya Tino Livramento, 23, kupata jeraha la msuli wa nyuma ya paja litakalomuweka nje ya uwanja wiki nane, lakini kuna timu zinazomtaka pia.
Jeraha hilo limeacha pengo kubwa katika safu ya ulinzi ya Newcastle, na mabosi wameanza kuchuja majina ya mabeki wanaoweza kupatikana kwa mkopo au uhamisho wa kudumu. Mkataba wake unamalizika 2028.
Joe Gomez
LIVERPOOL haina mpango wa kumuuza beki raia wa England, Joe Gomez, 28, katika dirisha hili la Januari baada ya beki wa kulia wa kimataifa wa Ireland Kaskazini, Conor Bradley, 22, kupata jeraha la goti litakalomuweka nje ya uwanja kwa msimu mzima.
Gomez, ambaye anaweza kucheza kama beki wa kati au pembeni awali alikuwa akihusishwa kuondoka kwa sababu hachezi kila mara.
Ben White
ARSENAL imesisitiza kuwa haina mpango na haitaki kumuuza beki wa kimataifa wa England, Ben White, 28, licha ya kukosa muda mwingi wa kucheza msimu huu.
Beki huyo ameingia katika rada za Everton na Manchester City ambazo zinahitaji kusajili kuziba mapengo baada ya mastaa wao kupata majeraha.
White ni mmoja wa mabeki wenye uwezo wa kucheza nafasi nyingi, jambo linalomfanya awe muhimu.