Como inamtaka Silva, Juve, Galatasaray bado zipo
Muktasari:
- Hata hivyo, Silva ambaye msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote, huduma yake pia inahitajika sana na Juventus na Galatasaray ambazo tayari zimeshaanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili na zinataka kukamilisha dili Januari hii.
KIUNGO wa Manchester City na timu ya taifa ya Ureno, Bernardo Silva, 31, anadaiwa huenda akatimkia Italia kujiunga na Como katika dirisha la majira ya kiangazi mwaka huu.
Hata hivyo, Silva ambaye msimu huu amecheza mechi 28 za michuano yote, huduma yake pia inahitajika sana na Juventus na Galatasaray ambazo tayari zimeshaanza mazungumzo kwa ajili ya kumsajili na zinataka kukamilisha dili Januari hii.
Kiungo huyo ni mmoja wa wachezaji wenye uzoefu mkubwa Ulaya akiwa ameshinda mataji mengi Ligi Kuu England, lakini mkataba wake unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu na hadi sasa bado Man City haijafanya naye mazungumzo yoyote ya kumsainisha dili jipya hali inayoonyesha kuwa haina mpango wa kuendelea kuwa naye.
Licha ya kuwepo kwa timu za Saudi Arabia zinazohitaji kumpa mshahara mnono, inaelezwa Bernardo anaweza kujiunga na Como.
Elliot Anderson
MANCHESTER CITY imeanza mawasiliano kuhusu uwezekano wa kumsajili kiungo wa Nottingham Forest na timu ya taifa ya England, Elliot Anderson, mwenye umri wa miaka 23.
Anderson amekuwa mmoja kati ya viungo wanaokua kwa kasi katika Ligi Kuu England na timu nyingi kubwa zimekuwa zikihitaji saini yake tangu dirisha lililopita la majira ya kiangazi. Hata hivyo, Nottingham Forest haiko tayari kumuuza kirahisi kwa sababu yupo katika mipango yake hivyo inahitaji ofa nono.
Marc Guehi
BAYERN MUNICH bado haijakata tamaa katika harakati za kumsajili beki wa Crystal Palace na timu ya taifa ya England, Marc Guehi, mwenye umri wa miaka 25.
Guehi amekuwa akionyesha kiwango cha juu akiwa na Palace na timu ya taifa ya England na mbali ya Bayern, staa huyo pia anahitajika na timu za ndani ya England ambazo ni Manchester City, Arsenal na Liverpool.
Hata hivyo, hivi karibuni taarifa zinaeleza kwamba hataki kwenda Man City badala yake anataka kwenda ama Arsenal au Liverool.
Donyell Malen
ROMA imefikia makubaliano ya kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa Aston Villa na timu ya taifa ya Uholanzi, Donyell Malen, mwenye umri wa miaka 26, kwa mkataba wenye kipengele cha kumnunua moja kwa moja kwa Euro 28 milioni mwisho wa msimu huu ikiwa itaridhishwa na kiwango chake.
Malen alijiunga na Aston Villa akiwa na matarajio makubwa, lakini amekuwa akikosa nafasi ya kucheza mara kwa mara kikosini.
Uhamisho huu unaonekana kumfurahisha sana Malen ambaye anaamini atapata nafasi kubwa sana ya kucheza tofauti na ilivyo katika kikosi cha Villa kwa sasa.
Marcos Llorente
ATLETICO MADRID inatafakari ofa ya Euro 35 milioni kutoka Manchester United kwa ajili ya kumsajili mchezaji kiraka Marcos Llorente, 30.
Llorente ni mchezaji anayeweza kucheza katika nafasi mbalimbali za kiungo na ulinzi, jambo linalomfanya kuwa chaguo linalovutia Man United ambayo kwa sasa haina kocha wa kudumu baada ya kuoachana na Ruben Amorim. Atletico haina haraka ya kumuuza, lakini kiasi hicho cha pesa kinaweza kuishawishi.
Tarik Muharemovic
MANCHESTER UNITED, Tottenham Hotspur na Newcastle United zimeanza kumfuatilia beki wa kati wa Sassuolo, Tarik Muharemovic, 22.
Muharemovic amekuwa akifuatiliwa na maskauti wa timu nyingi Ulaya ambao wamekuwa wakisafiri kwenda Italia kumtazama akicheza Serie A.
Sassuolo haina mpango wa kumzuia staa huyo kirahisi, lakini inahitaji ofa ya kuvutia ili kumwachia kwa sababu ni miongoni mwa mastaa muhimu kikosini.
Tammy Abraham
MSHAMBULIAJI wa England na Roma, Tammy Abraham, 28, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo Besiktas, anaonyesha nia ya kurejea katika Ligi Kuu England.
Aston Villa inatajwa kuwa miongoni mwa timu zinazomfuatilia kwa karibu ikiwa ni katika mipango ya kuongeza nguvu safu ya ushambuliaji. Abraham amekuwa akipambana kurejesha kiwango bora baada ya majeraha.
Arda Guler
KIUNGO wa Real Madrid, Arda Guler, 20, hana mapango wa kuondoka katika kikosi hicho licha ya kuhusishwa na baadhi ya timu kubwa Ulaya ikiwemo Arsenal na PSG.
Guler ambaye alidaiwa kuwa anaweza akaondoka kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza, amepanga kuendelea kusalia kuhakikisha anapambania nambaa kwani anaamini bado anaweza kutoboa.