Nashon aanza mikwara Simba
Muktasari:
- Nyota huyo ambaye ni miongoni mwa usajili mpya wa Simba, alisema anafahamu ukubwa wa klabu hiyo na ushindani uliopo, lakini hilo halimtishi badala yake, alisema ndilo lililomvutia zaidi kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.
WAKATI usajili mkubwa wa Simba kuelekea msimu wa 2026/27 ukiibua mjadala kuhusu nani ataanza kikosini, kiungo mpya wa timu hiyo Kelvin Nashon amesema yupo tayari kupigania nafasi kwenye kikosi hicho.
Nyota huyo ambaye ni miongoni mwa usajili mpya wa Simba, alisema anafahamu ukubwa wa klabu hiyo na ushindani uliopo, lakini hilo halimtishi badala yake, alisema ndilo lililomvutia zaidi kujiunga na Wekundu wa Msimbazi.
“Nimekuja kupigania beji ya Simba, mimi ni mshindani, nilipokubali kusaini Simba nilijua nakwenda sehemu ambayo hakuna namba ya bure, kila mmoja anatakiwa kuonyesha anastahili kucheza,” alisema Nashon.
Kiungo huyo alisema hana presha ya kuwaza nani ataanza kikosini, akisisitiza jukumu lake ni kufanya kila analoweza mazoezini na uwanjani huku maamuzi ya mwisho yakibaki kwa kocha Steve Barker. “Nitafanya sehemu yangu, nitampa mwalimu wakati mgumu wa kuchagua kikosi. Nikicheza ni vizuri, nisipocheza nitaendelea kufanya kazi kwa sababu naamini ushindani ndio unaijenga timu kubwa.”
Kauli hiyo imekuja wakati Simba ikiwa imeongeza ushindani mkubwa eneo la kiungo baada ya kusajili wachezaji kadhaa wapya akiwemo Ibraheem Jabaar.
Nashon amesema maisha yake ya soka yamemfundisha kutokata tamaa, akiwa na JKT Tanzania, Geita Gold, Singida BS, Mtibwa Sugar na Pamba Jiji.
Kwa sasa Nashon ni sehemu ya kikosi cha Simba kilichopo Kigali.