Vigogo Chelsea wapania kumng’oa Vinicius Madrid
Muktasari:
- Vinicius ni miongoni mwa wachezaji wanaodaiwa kutaka kuondoka Madrid mwisho wa msimu huu kwa sababu hawaridhishwi na namna wanavyochezeshwa chini ya kocha Xabi Alonso.
CHELSEA imeingia katika vita ya kuiwania saini ya mshambuliaji wa Real Madrid na timu ya taifa ya Brazl ili kumsajili dirisha lijalo la majira ya kiangazi.
Vinicius ni miongoni mwa wachezaji wanaodaiwa kutaka kuondoka Madrid mwisho wa msimu huu kwa sababu hawaridhishwi na namna wanavyochezeshwa chini ya kocha Xabi Alonso.
Mara kadhaa imekuwa ikiripotiwa kwamba Viniciua hayupo katika maelewano mazuri na kocha huyo na amewahi kusikika akitamka hadharani kwamba ni bora aondoke.
Hata hivyo, Chelsea itatakiwa kushinda vita dhidi ya vigogo wengine wa Ulaya ambao wapo tayari kutoa kiasi kikubwa cha pesa kuhakikisha zinamsajili Vinicius na miongoni mwa timu hizo ni PSG.
Vinicius ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwakani, amewaambia mabosi wa Madrid ili asaini mkataba mpya anahitaji apewe mshahara sawa na ule ambao Kylian Mbappe wa Euro 600,000 kwa wiki.
Marcus Rashford
BARCELONA imepanga kufanya kila linalowezekana kuhakikisha inambakisha mshambuliaji wa Manchester United na timu ya taifa ya England, Marcus Rashford, 28, ambaye anacheza kwa mkopo katika kikosi chao.
Awali baada ya Ruben Amorim kufukuzwa Man United baadhi ya vyombo vya habari viliripoti kuna uwezekano mkubwa Rashford akarudi katika kikosi hicho kwa msimu ujao, lakini sasa Barca inadaiwa kutaka kujitahidi kadri itakavyoweza ili kumpa mkataba wa moja kwa moja.
Tammy Abraham
ASTON Villa inaangalia uwezekano wa kumsajili mshambuliaji wa England, Tammy Abraham, mwenye umri wa miaka 28, ambaye kwa sasa yupo kwa mkopo Besiktas akitokea Roma.
Abraham anatajwa kuvutia mabosi wa Villa kutokana na uzoefu wake wa Ligi Kuu England, Serie A na mashindano ya Ulaya.
Kocha Unai Emery anaamini mshambuliaji huyo anaweza kuongeza nguvu na kumpa chaguo nyingi katika safu yake ya ushambuliaji ya kikosi chake.
Igor Tyjon
MANCHESTER United inapambana na Arsenal kuwania saini ya kinda wa Blackburn Rovers na timu ya taifa ya vijana ya England, Igor Tyjon, mwenye umri wa miaka 17.
Tyjon anasikifika kwa ubora mkubwa aliouonyesha tangu kuanza kwa msimu huu. Mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwaka 2026. Man United inaona usajili wake kama uwekezaji wa muda mrefu kwa ajili ya kumtumia siku za usoni.
Giorgio Scalvini
NEWCASTLE United inaendelea kumtathmini beki wa kati wa Atalanta, Giorgio Scalvini, 22,ikiwa inaweza kumsajili dirisha hili ili akawe mbadala wa beki wao raia wa Uswiss, Fabian Schar, 34, ambaye amepata majeraha yanayotarajiwa kumweka nje kwa muda mrefu.
Scalvini anasifiwa kwa uwezo wake wa kusoma mchezo, nguvu za kimwili na utulivu akiwa na mpira, jambo linalomfanya kuwa chaguo muhimu kwa Newcastle.
Kobbie Mainoo
KIUNGO wa Manchester United, Kobbie Mainoo, 20, mshambuliaji wa timu hiyo, Joshua Zirkzee, 24, na kiungo, Manuel Ugarte, 24, wote walikuwa wanapanga kuondoka dirisha hili la majira ya baridi ikiwa Ruben Amorim angeendelea kusalia katika kikosi hicho.
Inaelezwa mastaa hawa walichoshwa na namna Amorim alivyokuwa akiwachukulia kwa kuwaweka nje muda mwingi akidai kuwa hawaendani na mifumo yake.
Federico Chiesa
JUVENTUS imeendelea kufanya mazungumzo na Liverpool ili kumsajili kwa mkopo mshambuliaji wa timu hiyo na Italia, Federico Chiesa, 28.
Chiesa ameonyesha nia ya kutaka kurejea Juventus aliyoitumikia mwaka 2022 hadi 2024 kwa sababu hapati nafasi ya kutosha kikosi cha kwanza cha Liverpool.
Yupo tayari hata kupunguza mshahara wake wa sasa ili kuhakikisha dilo hilo linafanikiwa.
Jamie Leweling
MABOSI wa Stuttgart wameendelea kushikilia msimamo wao wa kuhitaji kiasi kisichopungua Euro 50 milioni ili kumuuza winga wao, Jamie Leweling.
Awali Bournemouth ilijipanga kulipa Euro 40 milioni kwa ajilinya kumsajili staa huyu ili akawe mbadala wa winga wao wa kimataifa wa Ghana mwenye umri wa miaka 25, Antoine Semenyo ambaye amejiunga na Manchester City.