Bernardo Silva akaribia kutua katika kikosi cha Juventus
Muktasari:
- Silva amekuwa mhimili muhimu katika mafanikio ya Man City kwa miaka ya karibuni, lakini anaonekana kutaka changamoto mpya baada ya kuhudumu katika timu hiyo kwa muda mrefu.
JUVENTUS inaongoza mbio za kuwania saini ya kiungo wa Manchester City na timu ya taifa ya Ureno, Bernardo Silva, 31, ambaye mkataba wake wa sasa unatarajiwa kumalizika mwisho wa msimu huu.
Silva amekuwa mhimili muhimu katika mafanikio ya Man City kwa miaka ya karibuni, lakini anaonekana kutaka changamoto mpya baada ya kuhudumu katika timu hiyo kwa muda mrefu.
Vigogo kadhaa vya Ulaya pia vinaendelea kumfuatilia, lakini Juventus inaonekana kuwa mbele na Silva mwenyewe ameonyesha kuvutiwa na mpango kazi wao.
Mabingwa wa Uturuki, Galatasaray ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kumsajili ingawa hadi sasa hawajafikia mwafaka na wawakilishi wake.
Kuna uwezekano mkubwa Man City ikakubali kumuuza katika dirisha hili ili kupata pesa walau kidogo badala ya kumwacha aondoke bure.Silva anadaiwa kuwaambia wawakilishi wake anataka kumaliza msimu.
Tino Livramento
ARSENAL imeanza kumfuatilia kwa karibu beki wa Newcastle United na timu ya taifa ya England, Tino Livramento, mwenye umri wa miaka 23, kwa lengo la usajili wa majira ya kiangazi.
Livramento amekuwa akionyesha kiwango bora katika Ligi Kuu England tangu msimu uliopita.
Mkataba wake wa sasa unatarajiwa unatarajiwa kumalizika 2028 na tangu kuanza kwa msimu huu amecheza mechi 18 za michuano yote.
Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta anamwona kama chaguo la kuongeza ushindani.
Conor Gallagher
ASTON Villa ipo katika mazungumzo ya awali kutaka kumsajili kiungo wa Atletico Madrid na timu ya taifa ya England, Conor Gallagher, 25.
Staa huyu ambaye awali aliwahi kucheza Ligi Kuu England akiwa na Chelsea amekuwa akihusishwa kuondoka Atletico tangu mwaka jana kwa sababu hapati nafasi ya kutosha katika kikosi cha kwanza.
Kocha Unai Emery anaamini uzoefu wa Gallagher unaweza kuongeza nguvu zaidi katika safu ya kiungo. Mkataba wa Gallagher unamalizika 2029.
Kaye Furo
BRENTFORD imekubali kulipa Pauni 8.7 milioni kwenda Club Brugge kwa ajili ya kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya vijana ya Ubelgiji, Kaye Furo, 18.
Furo anatajwa kuwa miongoni mwa vipaji vinavyochipukia kwa kasi Ulaya kutokana na uwezo wa kufunga mabao, kasi na ufundi akiwa ndani ya boksi.
Usajili wake unaonekana kuwa sehemu ya mpango wa muda mrefu wa Brentford kuwekeza kwa vijana.
Dominik Szoboszlai
KIUNGO wa kimataifa wa Hungary, Dominik Szoboszlai mwenye umri wa miaka 25 amefikia makubaliano ya awali ya kuongeza mkataba na Liverpool.
Szoboszlai amekataa ofa nono kutoka Real Madrid na Bayern Munich ambazo zinahitaji kumsajili katika dirisha hili.
Kiungo huyo anaamini bado anahitaji zaidi kuendelea kusalia katika viunga vya Anfield na inaelezwa anaweza kusaini mkataba wa miaka mitatu.
Leon Bailey
MSHAMBULIAJI wa ASTON Villa na timu ya taifa ya Jamaica, Leon Bailey, 28, anaweza kujiunga na Girona kwa mkopo hadi mwisho wa msimu baada ya mkopo wa sasa Roma kusitishwa.
Bailey amekuwa akipata wakati mgumu kupata nafasi ya kudumu Roma, hali inayofanya uwezekano wa kumpeleka La Liga uonekane kuwa chaguo bora kwake ili kufufua kiwango chake. Girona ipo tayari kumsajili na kulipa mshahara wake kila wiki.
Othmane Maamma
LIVERPOOL, Manchester United na Newcastle United zinaendelea kumfuatilia kwa karibu mshambuliaji wa Watford na timu ya taifa ya Morocco chini ya umri wa miaka 20, Othmane Maamma, 20.
Staa huyu chipukizi amevutia macho ya maskauti wengi wa vigogo hao ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa muda mrefu. Watford inatajwa kuwa tayari kumuuza kwa klabu yenye ofa nono.
Taty Castellanos
MABOSI wa West Ham United wapo kwenye mazungumzo na Lazio ili kumsajili mshambuliaji wa klabu hiyo na timu ya taifa ya Argentina, Taty Castellanos, 27, katika dirisha hili kwa dau linalokadiriwa kufikia Pauni 25 milioni.
Kocha wa West Ham United anataka kuongeza nguvu katika safu ya ushambuliaji baada ya kuona changamoto ya upachikaji mabao msimu huu.