Usajili: Ni mwendo wa kupiga pesa tu!
Muktasari:
- Aston Villa, Manchester City na Newcastle United tayari zimeingia kwenye orodha ya timu sita zilizowahi kupata mapato makubwa zaidi kupitia mauzo ya nyota wake katika dirisha moja la usajili.
LONDON, ENGLAND: KLABU za Ligi Kuu England zimezoeleka kwa matumizi makubwa katika usajili, lakini dirisha hili zimeonyesha upande mwingine kwa kufanya biashara kubwa kupitia mauzo ya wachezaji.
Aston Villa, Manchester City na Newcastle United tayari zimeingia kwenye orodha ya timu sita zilizowahi kupata mapato makubwa zaidi kupitia mauzo ya nyota wake katika dirisha moja la usajili.
Kwa mujibu wa takwimu za Transfermarkt wiki hii, Villa imeingiza euro293.1 milioni (Sh251 bilioni) kutokana na mauzo ya wachezaji, huku City ikiwa imekusanya euro278.6 milioni na Newcastle euro275.5 milioni.
Timu hizo sasa zinakaribia kuvunja rekodi ya AS Monaco iliyoweka euro360 milioni katika msimu wa 2018/19.
Rekodi hiyo ya Monaco ilijengwa na mauzo makubwa kadhaa, likiwamo la Kylian Mbappe kwenda Paris Saint-Germain kwa euro180 milioni. Thomas Lemar alijiunga na Atletico Madrid kwa euro72 milioni, huku Fabinho akihamia Liverpool kwa euro45 milioni.
Kwa sasa, Monaco ndiyo inayoongoza, ikifuatiwa na Chelsea iliyokusanya euro321 milioni msimu wa 2025/26 na Atletico Madrid iliyofikisha euro314 milioni msimu wa 2019/20.
Hata hivyo, kwa kuwa bado zimesalia siku kadhaa kabla ya dirisha kufungwa, rekodi hiyo inaweza kuvunjwa.
VILLA YAONGOZA
Villa ndiyo iliyo karibu zaidi na rekodi ya Monaco, huku uhamisho wa Morgan Rogers kwenda Chelsea kwa Pauni117 milioni ukiwa umechangia sehemu kubwa ya mapato hayo.
Ezri Konsa, Youri Tielemans na Lucas Digne pia ni miongoni mwa wachezaji walioondoka Villa katika dirisha hili.
Biashara hiyo imeifanya Villa kuwa na faida kubwa zaidi ya usajili miongoni mwa klabu za Ligi Kuu England kwa sasa.
Villa imetumia euro160.5 milioni katika usajili, hivyo ikiwa na faida ya euro132.6 milioni baada ya kujumlisha mapato ya mauzo.
Hata hivyo, biashara hiyo imefanyika wakati klabu hiyo ikikabiliwa na shinikizo la kifedha.
Mwezi Juni, UEFA ilipiga Villa faini ya euro22.5 milioni kutokana na kukiuka kwa kiasi kikubwa kanuni ya gharama za kikosi kwa mwaka 2025. Kati ya kiasi hicho, euro15 milioni zimesitishwa kutekelezwa kwa sharti la klabu kuendelea kupunguza uwiano wa gharama za kikosi mwaka 2026.
Athari za kuondoka kwa baadhi ya wachezaji wakubwa zilionekana mwanzoni mwa msimu, Villa ilipofungwa 4-0 na Brighton.
Baada ya mchezo huo, mchambuzi Gary Neville amesema Villa ilionekana kana kwamba “imevuliwa moyo”, akielekeza zaidi kwenye uzoefu uliopotea baada ya kuondoka kwa Rogers, Tielemans na Konsa.
Villa bado inaweza kusogea zaidi kuelekea rekodi hiyo, hasa ikiwa Ollie Watkins ataondoka.
Klabu ya Saudi Arabia, Al-Hilal, imefanya majaribio kadhaa kumsajili Watkins, huku Villa ikiripotiwa kukataa ofa ya takribani euro 52milioni.
Kocha Unai Emery tayari amekiri kuwa mshambuliaji huyo wa England anaweza kuondoka, ingawa klabu hizo mbili bado hazijafikia makubaliano kuhusu thamani yake.
MAN CITY KUIPIKU VILLA
Msimamo wa Manchester City umebadilika baada ya kusajili Ayyoub Bouaddi.
City imeingiza takribani euro 278.5milioni kutokana na mauzo ya wachezaji, akiwamo Savio, Tijjani Reijnders, Rodri, James Trafford, Manuel Akanji na Nathan Ake.
Baada ya kumsajili Bouaddi, matumizi ya City yamefikia euro273.7 milioni, hivyo kubaki na faida ya euro4.8 milioni kwenye biashara ya usajili.
Mauzo mengine yanaweza kubadili picha hiyo kwa haraka.
Tottenham tayari imekubaliana kumsajili Omar Marmoush kwa mkopo, ikiwa na sharti la kumsajili moja kwa moja kwa euro58 milioni msimu ujao. Hivyo, fedha hizo zitahesabiwa kwenye mapato ya City ya msimu wa 2027/28, si msimu huu.
Nico Gonzalez pia anatarajiwa kuondoka, huku Jack Grealish akiwa bado anaweza kuuzwa kabla ya dirisha kufungwa.
Grealish alicheza kwa mkopo Everton msimu uliopita, huku klabu hiyo ikiendelea kumtaka. Hata hivyo, mchezaji huyo anaamini kuondoka kwa Pep Guardiola na kuwasili kwa Enzo Maresca kama kocha kunaweza kumpa mwanzo mpya City. Mkataba wake unamalizika Juni 2027.
Iwapo Gonzalez na huenda Grealish watauzwa, mapato ya City msimu huu yanaweza kuongezeka kwa kiasi kikubwa.
Uwezo wa City kuuza wachezaji kwa thamani kubwa ni muhimu hasa kutokana na ujenzi upya wa safu yake ya kiungo. Tayari imefanikiwa kumsajili Elliot Anderson kutoka Nottingham Forest kwa euro135 milioni na bado inamfuatilia kiungo wa Chelsea, Enzo Fernandez.
NEWCASTLE USIPIME
Newcastle imefikisha euro275.5 milioni katika mapato ya mauzo tu, huku sehemu kubwa ya fedha hizo ikitokana na kuondoka kwa wachezaji watatu muhimu.
Sandro Tonali amejiunga na Tottenham kwa euro 108milioni, Bruno Guimaraes amehamia Arsenal kwa euro87.5 milioni, huku Anthony Gordon akijiunga na Barcelona kwa euro 80milioni.
Mauzo hayo matatu yameibadilisha kwa kiasi kikubwa hali ya kifedha ya Newcastle katika dirisha hili.
Klabu hiyo imetumia euro197 milioni katika usajili, hivyo kubaki na faida ya euro78.5 milioni.
Kwa sasa, ni Villa na Nottingham Forest pekee zilizo na faida kubwa zaidi ya Newcastle katika biashara ya usajili miongoni mwa klabu za Ligi Kuu.
KLABU SITA ZIKO KWENYE FAIDA
Kiasi kikubwa cha mauzo katika Ligi Kuu pia kimeonekana kwenye mizania ya jumla ya usajili.
Kwa mujibu wa Transfermarkt, klabu sita za Ligi Kuu England kwa sasa ziko kwenye faida baada ya kuzingatia fedha zilizotumika kusajili wachezaji na zilizopatikana kupitia mauzo.
Kwa upande mwingine, Chelsea ina hasara kubwa zaidi, ikiwa imetumia euro407.95 milioni na kupata euro165.65 milioni kupitia mauzo, hivyo kuwa na tofauti hasi ya euro 242.3milioni.
Tottenham inafuata ikiwa na hasara ya euro189.15 milioni, huku Arsenal ikiwa na hasara ya euro180.95 milioni, huku zikiwa zimesalia siku saa tu kabla ya dirisha kufungwa Septemba 1.
BRIGHTON BADO KINARA WA BIASHARA
Takwimu za Brighton zinaonyesha mfumo tofauti wa kufanya biashara ya wachezaji.
Katika misimu mitano iliyopita, Brighton & Hove Albion imetumia euro665.4 milioni kusajili wachezaji na kupata euro715.4 milioni kupitia mauzo, ikiwa na faida ya takribani euro50 milioni.
Kwa mujibu wa Transfermarkt, Brighton ndiyo klabu pekee ya Ligi Kuu ambayo imepata faida ya jumla katika biashara ya usajili kwa kipindi hicho cha misimu mitano.
Aston Villa inafuata ikiwa karibu kufikia usawa, ikiwa na tofauti hasi ya euro 10.02milioni.
Takwimu hizo zinaonyesha namna Brighton ilivyofanikiwa kwa muda mrefu kuuza wachezaji kwa fedha nyingi huku ikiendelea kuwekeza kwenye usajili, badala ya kutegemea dirisha moja pekee lenye mauzo.