Farid Mussa ataja kitakachombeba
Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, winga huyo ambaye ametumika Yanga kwa muda mrefu alisema baada ya kutua Coastal Union, aliomba kukaa nje kwanza ili afanye mazoezi zaidi awe fiti na sasa anajiona yu-ko tayari kuanza kuipigania timu hiyo aliyojiunga nayo msimu huu.
WINGA wa Coastal Union, Farid Mussa amefunguka namna anavyojipanga kuibeba timu hiyo Ligi Kuu Bara na atatumia uzoefu wake wa kuzichezea klabu kubwa kufanikisha hilo.
Akizungumza na Mwanaspoti, winga huyo ambaye ametumika Yanga kwa muda mrefu alisema baada ya kutua Coastal Union, aliomba kukaa nje kwanza ili afanye mazoezi zaidi awe fiti na sasa anajiona yu-ko tayari kuanza kuipigania timu hiyo aliyojiunga nayo msimu huu.
“Wakati nafika hapa niliongea na kocha nikamuomba anipe muda kidogo nijipange sawasawa, namshukuru sana alinielewa, nilitaka niwe fiti kwa kiwango kikubwa na sasa najiona naweza kuanza kuipigania Coastal Union uwanjani,” alisema Farid.
“Nilipochagua kuja hapa nilijua ni kitu gani nataka nikifanye ndani ya klabu hii, kuna uzoefu mkubwa ambao naweza kuutumia hapa nikishirikiana na wachezaji wenzangu ili tuipandishe timu ipate matokeo mazuri." Aliongeza anataka kuona wanautafuta ushindi wa kwanza msimu huu kwenye mechi yao ya tano.
“Ukilitazama benchi la ufundi tuna mwalimu ambaye anajua kuishi na wachezaji, kikosi nacho kina vija-na wenye mchanganyiko ambao tutasaidiana kuongozana tufikie malengo, kwa sasa kitu muhimu ni kuanza kutafuta ushindi.”
Winga huyo ametua Coastal akitokea Yanga alipodumu kwa misimu sita. Kabla ya hapo alicheza CD Tenerife B ya Hispania na Azam FC.