Utabiri…! Manchester United haitoboi nane bora Ulaya
Muktasari:
- Kwa mujibu wa utabiri huo, Man United inatarajiwa kumaliza katika nafasi ya tisa, ikiwa ni nafasi moja nyuma ya nane bora ambayo inatoa tiketi ya moja kwa moja kwenda hatua ya 16 bora.
LONDON, ENGLAND: MWAKA wa tabu. Manchester United imetabiriwa kumaliza nje ya nane bora katika hatua ya ligi ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu, jambo litakalowalazimisha kucheza mchujo wa kuwania nafasi 16 bora.
Kwa mujibu wa utabiri huo, Man United inatarajiwa kumaliza katika nafasi ya tisa, ikiwa ni nafasi moja nyuma ya nane bora ambayo inatoa tiketi ya moja kwa moja kwenda hatua ya 16 bora.
Utabiri huo umefanywa na wataalamu wa takwimu kutoka Football Ranked, ambao wamefanyia uchambuzi ratiba ya mechi baada ya droo ya hatua ya ligi kufanyika Monaco, Ufaransa, chini ya usimamizi wa UEFA.
Manchester United imepangwa kukutana na vigogo Bayern Munich na Atletico Madrid, huku pia ikiwa na michezo dhidi ya Sporting CP, Roma, RB Leipzig, Villarreal, Como na Sabah.
Kwa mujibu wa makadirio ya Football Ranked, kikosi cha Michael Carrick kinatarajiwa kukusanya wastani wa pointi 14.1 katika michezo hiyo, ambazo zitatosha kuwapa nafasi ya tisa.
Katika misimu miwili iliyopita tangu mfumo wa Ligi ya Mabingwa ubadilishwe, timu ilihitaji angalau pointi 16 ili kumaliza ndani ya nane bora.
Iwapo United itamaliza nafasi ya tisa, italazimika kucheza mechi za mchujo za hatua ya 16 bora dhidi ya timu itakayomaliza nafasi ya 23 au 24.
Katika simulizi ya Football Ranked, United inaweza kukutana na Lens au Lille katika mchujo huo wa mechi mbili, hali ambayo inaweza kuwalazimisha kusafiri kwenda kaskazini mwa Ufaransa.
Aston Villa nayo imetabiriwa kumaliza nafasi ya 10, licha ya kupitia kipindi kigumu katika majira haya ya kiangazi.
Hilo litafanya Villa kucheza dhidi ya timu nyingine kati ya Lens au Lille katika hatua ya mchujo.
ARSENAL, MAN CITY, LIVERPOOL SALAMA
Timu nyingine tatu za England zinatabiriwa kufuzu moja kwa moja hatua ya 16 bora.
Arsenal, ambayo ina mechi dhidi ya Real Madrid na Bayern Munich, inatarajiwa kumaliza nafasi ya pili ikiwa na pointi 17.6 za makadirio, nyuma ya Bayern Munich pekee.
Mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, Paris Saint-Germain, wanatarajiwa kumaliza nafasi ya tatu, huku Manchester City ikishika nafasi ya nne ikiwa na pointi 16.9 za makadirio.
Real Madrid inatarajiwa kumaliza nafasi ya tano, ikifuatiwa na Inter Milan, Liverpool ikiwa nafasi ya saba na Barcelona nafasi ya nane.
Miongoni mwa vigogo vinavyotabiriwa kukosa nane bora ni Borussia Dortmund, Napoli na Atletico Madrid, ambao wanakadiriwa kumaliza hadi nafasi ya 19.
VIGOGO WAINGIA HATARINI KUTOLEWA
Timu zinazotabiriwa kuondolewa kabisa kwenye mashindano hayo ni Real Betis na Villarreal za Hispania, Fenerbahce na Galatasaray za Istanbul, pamoja na Shakhtar Donetsk ya Ukraine. Shakhtar Donetsk italazimika kutumia Uwanja wa Stamford Bridge, London, kama uwanja wake wa nyumbani katika michezo ya Ligi ya Mabingwa.
WAPINZANI WA TIMU ZA LIGI KUU ENGLAND
Arsenal: Real Madrid (nyumbani), Bayern Munich (ugenini), Borussia Dortmund (nyumbani), Real Betis (ugenini), Lille (nyumbani), Napoli (ugenini), Sabah (nyumbani), Slavia Prague (ugenini).
Aston Villa: PSG (nyumbani), Barcelona (ugenini), Borussia Dortmund (nyumbani), Club Brugge (ugenini), Fenerbahce (nyumbani), Galatasaray (ugenini), Viking (nyumbani), Slavia Prague (ugenini).
Liverpool: Atletico Madrid (nyumbani), Inter Milan (ugenini), Porto (nyumbani), Club Brugge (ugenini), Villarreal (nyumbani), Fenerbahce (ugenini), Lens (nyumbani), LASK (ugenini).
Manchester City: PSG (nyumbani), Barcelona (ugenini), Sporting (nyumbani), Porto (ugenini), Napoli (nyumbani), RB Leipzig (ugenini), AEK Athens (nyumbani), Lens (ugenini).
Manchester United: Bayern Munich (nyumbani), Atletico Madrid (ugenini), Roma (nyumbani), Sporting (ugenini), RB Leipzig (nyumbani), Villarreal (ugenini), Sabah (nyumbani), Como (ugenini).