Ule mzigo wa Kombe la Dunia la Klabu unaanza

Muktasari:
- Timu 32 kutoka mashirikisho sita yatachuana vikali kusaka taji hilo la ubingwa wa dunia na Al-Ahly na Inter Miami zitakazokata utepe zimepangwa kwenye Kundi A sambamba na timu za FC Porto na Palmeiras.
MIAMI, MAREKANI: ILE siku imefika. Mambo ni moto huku kwenye fainali za Kombe la Dunia la Klabu na utepe utakatwa uwanjani Hard Rock, Florida wakati chama la supastaa Lionel Messi, Inter Miami litakapomenyana na miamba ya soka ya Misri, Al-Ahly alfajiri ya Jumapili kwa saa za Afrika Mashariki.
Timu 32 kutoka mashirikisho sita yatachuana vikali kusaka taji hilo la ubingwa wa dunia na Al-Ahly na Inter Miami zitakazokata utepe zimepangwa kwenye Kundi A sambamba na timu za FC Porto na Palmeiras.
Al Ahly ni moja ya silaha muhimu za Afrika kwenye michuano hiyo, lakini imepangwa kwenye Kundi A lenye timu nyingi za kibabe. Hata hivyo, Al Ahly inakwenda kwenye michuano hiyo ikiwa na rekodi ya kubeba ubingwa wa Misri mara 45, huku ikifuzu Kombe la Dunia la Klabu mara 10 kwenye historia na misimu ya karibuni ilibeba ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Afrika katika msimu wa 2020-21, 2022-23 na 2023-24.
Ni Real Madrid (15) na Auckland City (13) ndizo timu zilizoshinda ubingwa wa mabara yao mara nyingi kuzidi Al Ahly (12) na inashika nafasi za juu kwa timu zilizofanya vizuri kwenye michuano hiyo ya ubingwa wa dunia na ilimaliza nafasi ya tatu kwenye awamu ilizocheza katika muongo huu. Mtihani wao wa safari hii utaanza kwa kukabiliana na jeshi la Messi na wenzake, wakiwamo mastaa wa zamani wa Barcelona, Luis Suarez, Sergio Busquets na Jordi Alba. Al Ahly ilikuwa na wasiwasi juu ya afya ya staa wake, Emam Ashour, lakini kiungo alionekana kuwa vizuri. Timu zote mbili zinaonekana kuwa na mastaa wake mahiri kabisa na kikosi cha Inter Miami, kinachonolewa na Javier Mascherano kinatarajia kutumia fomesheni ya 4-4-2 na Messi na Suarez - waliofunga mabao 23 kwa pamoja mwaka huu, watarajia kuanza mbele kwenye fowadi.
Mechi nyingine zitakazopigwa Jumapili, mabingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, Paris Saint-Germain itarusha kete yake ya kwanza kwa kumenyana na Atletico Madrid kwenye Kundi B, wakati kipute hicho kitazishuhudia pia, Bayern Munich ya straika Harry Kane ikiwa na kazi kubwa mbele ya Auckland City Fc katika mchezo wa Kundi C.
Mashabiki wa soka wanasubiri kuona kama PSG itaweza kuonyesha ubabe wake wa Ulaya kwa kukabiliana na Atletico, moja ya timu ngumu kabisa inayocheza La Liga.
Vikosi vinavyotarajiwa;
Al Ahly: El Shenawy; Hany, Rabia, Ibrahim, Debes; El Solia, Ashour, Ateya; Mohamed, Trezeguet; Abou Ali
Inter Miami: Ustari; Weigandt, Falcon, Lujan, Allen; Allende, Cremaschi, Busquets, Segovia; Messi, Suarez