Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

USAJILI: Siri ya dili za Pauni 100 milioni

USAJILI Pict

Muktasari:

  • Dirisha hili la usajili pekee limevunja rekodi kadhaa. Chelsea imekubali kumchukua Morgan Rogers kutoka Aston Villa kwa pauni 117 milioni, Manchester City ikalipa pauni116 milioni kumsajili Elliot Anderson kutoka Nottingham Forest, huku Tottenham ikivunja rekodi yake kwa kutoa pauni100 milioni kwa Sandro Tonali.

LONDON, ENGLAND: MIAKA 34 iliyopita, usajili wa pauni milioni 13 ulimtikisa kila mtu nchini Italia.

Mwaka 1992, AC Milan ilipomsajili Gianluigi Lentini kutoka Torino kwa ada iliyokuwa rekodi ya dunia wakati huo, magazeti yaliuita mkataba huo "aibu", huku gazeti rasmi la Vatican likisema ulikuwa "kashfa dhidi ya heshima ya kazi."

Lakini leo, kiasi hicho kingekuwa kidogo sana ukilinganisha na soko la sasa la Ligi Kuu England.

Dirisha hili la usajili pekee limevunja rekodi kadhaa. Chelsea imekubali kumchukua Morgan Rogers kutoka Aston Villa kwa pauni 117 milioni, Manchester City ikalipa pauni116 milioni kumsajili Elliot Anderson kutoka Nottingham Forest, huku Tottenham ikivunja rekodi yake kwa kutoa pauni100 milioni kwa Sandro Tonali.

Mbali na dili hizo, Tottenham pia imemsajili Mateus Fernandes kwa pauni85 milioni kutoka West Ham, Barcelona ikamnasa Anthony Gordon kutoka Newcastle kwa pauni69 milioni, wakati Manchester United ikitoa pauni50 milioni kwa Andrey Santos wa Chelsea.

Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Ligi Kuu England kushuhudia sajili tatu wa zaidi ya pauni100 milioni ndani ya dirisha moja la usajili, huku muda ukiwa bado haujaisha kabla ya kufungwa Septemba 1.

Msimu uliopita wa usajili wa majira ya kiangazi, klabu za Ligi Kuu England zilitumia rekodi ya pauni3 bilioni kununua wachezaji.

ROGERS Pict

KWA NINI ADA ZINAENDELEA KUPANDA?

Usajili wa Morgan Rogers unaonyesha namna soko la sasa linavyofanya gumu.

Chelsea imenunua mchezaji kutoka Aston Villa, timu iliyomaliza juu yao katika misimu mitatu kati ya minne iliyopita. Zamani, klabu nyingi zingeona ni hatari kuimarisha mpinzani wa moja kwa moja, lakini safari hii Chelsea ilikubali tu bei iliyowekwa na Villa.

Mtaalamu wa masuala ya fedha za soka, Kieran Maguire, anasema kila usajili unaovunja rekodi huweka kiwango kipya cha bei.

"Unapoweka rekodi mpya, unabadilisha thamani ya soko. Forest waliona Elliot Anderson ni mchezaji muhimu, hivyo walitaka ada yake iwe karibu na rekodi. Baadaye Villa wakatumia kiwango hicho kumuuza Morgan Rogers kwa bei kubwa zaidi," alisema.

Baada ya City kulipa pauni 116milioni kwa Anderson, Villa iliweka wazi kuwa yeyote anayemtaka Rogers atalazimika kutoa zaidi ya kiwango hicho. Chelsea ikafanya hivyo kwa kukubali pauni117 milioni.

Arsenal pia ilimhitaji Rogers, lakini ilikataa kufikia thamani iliyotakiwa na Villa.

Mfano huo unaonyesha jinsi bei za soko zinavyopanda haraka pindi rekodi mpya inapowekwa.

ROGE 03

KWA NINI WACHEZAJI WA ENGLAND NI GHALI ZAIDI?

Sababu kubwa ni mahitaji makubwa kuliko idadi iliyopo.

Sheria za Ligi Kuu zinazitaka klabu kuwa na angalau wachezaji wanane waliokulia nchini England katika kikosi cha watu 25. Pia, klabu zinazoshiriki mashindano ya UEFA zinapaswa kutimiza masharti hayo ya wachezaji wa nyumbani.

Kutokana na hilo, ushindani wa kuwapata wachezaji bora wa Kiingereza umekuwa mkubwa.

Maguire anawataja wachezaji wa Ligi Kuu kuwa ni "tayari kwa matumizi", akimaanisha hawahitaji muda wa kuzoea mazingira mapya.

Klabu tayari zinawajua uwezo wao dhidi ya wapinzani wa kiwango cha juu, zinafahamu wanaweza kuhimili kasi na nguvu za ligi ya hapa, hivyo zinapunguza hatari ya usajili kutoka nje ya England.

Zaidi ya hayo, mapato makubwa ya haki za matangazo yanaipa klabu za England uwezo mkubwa wa kifedha, jambo linalowapa wauzaji nafasi ya kudai ada kubwa zaidi.

ROGE 05

KWA NINI KLABU ZINAUZA MASTAA WAO?

Jambo la kushangaza zaidi ni kuona klabu zikikubali kuwauza wachezaji wao muhimu.

Aston Villa imemuuza Rogers licha ya kuwa nguzo muhimu kwa kocha Unai Emery. Nottingham Forest imekubali ofa ya City kwa Anderson, huku Newcastle ikimruhusu Anthony Gordon kuondoka licha ya kuwa mmoja wa wachezaji muhimu wa Eddie Howe.

Kwa sasa, klabu nyingi zinaona kuuza nyota mmoja kunaweza kuzipatia fedha za kuboresha maeneo kadhaa ya kikosi badala ya kutegemea mchezaji mmoja pekee.

Aidha, mauzo hayo yamechochea mjadala kuhusu kanuni za kifedha za Ligi Kuu, ambazo baadhi wanaamini zinazilazimisha klabu za ukubwa wa kati kuuza mastaa wao ili kuendana na masharti ya matumizi.

Maguire anasema kanuni hizo zinaweza kuwa sababu ya uamuzi wa usajili, lakini si lazima ziwe sababu kuu.

"Kwa kuwa klabu nyingi hazilazimiki kuuza kutokana na matatizo ya kifedha, zinaweza kusubiri hadi zipate thamani kubwa zaidi kwa mchezaji wao," alisema.

ROGE 01

SHERIA MPYA ZA KIFEDHA

Ligi Kuu pia imeanza kuondoka kwenye mfumo wa Kanuni za Faida na Uendelevu wa Kifedha (PSR) na kuelekea mfumo mpya unaozingatia uwiano wa matumizi ya kikosi (SCR) pamoja na Mfumo wa Uendelevu na Uhimilivu wa Kifedha(SSR).

Mfumo huo unazingatia zaidi uwiano kati ya matumizi ya soka na mapato ya klabu.

Mishahara ya wachezaji, ada za mawakala na namna gharama za usajili zinavyogawanywa kwa kipindi cha mkataba sasa vitakuwa vitu muhimu zaidi katika kupanga matumizi.

Kwa klabu zinazoshiriki mashindano ya Ulaya, sheria za UEFA nazo zinaendelea kuweka mipaka ya matumizi.

Maguire anasema mashabiki mara nyingi huangalia ada ya jumla, wakati klabu huangalia gharama za kila mwaka.

"Ukimsajili mchezaji kwa pauni milioni 115 kwa mkataba wa miaka mitano, gharama ya uhasibu ni takribani pauni milioni 23 kwa mwaka kabla ya mshahara. Ukifikia Ligi ya Mabingwa, unaweza kupata mapato makubwa zaidi kuliko gharama hiyo," alisema.

Anakadiria kushiriki Ligi ya Mabingwa kunaweza kuingizia klabu kati ya euro 180 hadi 200 milioni kupitia zawadi, mapato ya mechi na mikataba ya kibiashara.

MATES 04

SOKO LINAENDELEA KUKUA

Tangu mwaka 2016, matumizi ya usajili katika dirisha la majira ya kiangazi yameongezeka kutoka pauni 1.16bilioni hadi rekodi ya pauni3.19 bilioni mwaka 2025.

Hata hivyo, utafiti wa Maguire na Chuo Kikuu cha Liverpool unaonyesha baadhi ya usajili wa zamani ulikuwa na uzito mkubwa zaidi ukilinganisha na uwezo wa kifedha wa klabu wakati huo.

Kwa kutumia mapato ya matangazo kama kipimo, usajili wa Alan Shearer kutoka Blackburn kwenda Newcastle mwaka 1996 kwa pauni15 milioni bado unaonekana kuwa mkubwa zaidi katika historia ya Ligi Kuu. Vivyo hivyo, usajili wa Rio Ferdinand kwenda Manchester United mwaka 2002 na Juan Sebastian Veron mwaka 2001 ulikuwa na thamani kubwa zaidi kwa mazingira ya kipindi hicho kuliko dili nyingi za sasa.

Utafiti huo pia unaonyesha kuwa usajili wa kwanza wa pauni milioni moja nchini England, Trevor Francis kwenda Nottingham Forest mwaka 1979, ungekuwa na thamani ya takribani pauni173 milioni katika soko la leo.

Hilo linaonyesha si kwamba ada za Rogers, Anderson au Tonali ni ndogo, bali ni kwamba mapato ya Ligi Kuu yamekua kwa kiwango kikubwa kiasi cha kufanya matumizi hayo yaonekane ya kawaida.

Jack Grealish alipokuwa mchezaji wa kwanza wa Uingereza kugharimu pauni100 milioni mwaka 2021, wengi waliona ni hatua kubwa katika historia ya soka.

Miaka mitano baadaye, usajili wa zaidi ya pauni100 milioni si jambo la kushangaza tena.

Na kwa mwenendo wa sasa, usajili wa kwanza wa pauni200 milioni unaweza kutokea mapema kuliko wengi wanavyotarajia.