Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Ufaransa, Ujerumani zilikuwa na mfumo kama wa FFP -3

KWENYE toleo lililopita tuliona namna Ligi Kuu England, Serie A na La Liga timu zao zilivyoathiriwa kwa madeni makubwa katika kujiendeesha baada ya kufanya matumizi makubwa kuliko mapato yao na kufanya msukumo huo wa uanzishwaji wa sera ya Financial Fair Play kuwa na ulazima mkubwa katika kuzinusuru timu hizo kwenye hatari ya kufa.

Kuna timu kama Valencia zilikumbwa na wakati mgumu kabla ya uanzishwaji wa sera hiyo ya udhibiti wa matumizi ya pesa kwenye soka la Ulaya kiasi cha kuwasukuma kuuza wachezaji wao muhimu kabisa kama Juan Mata, David Silva na David Villa kwa kuwataja kwa uchache ili kupunguza makali ya uchumi.

Baada ya ligi kubwa kama za England, Italia na Hispania kuwa kwenye hali mbaya hivyo, je mambo yalikuwaje kwenye ligi nyingine za Ulaya?

Ligi ya Ufaransa na Ujerumani
Kwa miaka mingi, klabu kwenye ligi hizi nyingine kubwa Ulaya, Ligue 1 ya Ufaransa na Bundesliga ya Ujerumani, zilikuwa na utaratibu wake wa udhibiti, lakini haukuwa na sheria kama za FFP.

Ligue 1
Huko Ufaransa, kulikuwa na taasis iliyofahamika kama Direction Nationale du Contrôle de Gestion (DNCG) ambayo ilikuwa inawajibu kwenye kuongoza, kusimamia na kufuatilia akaunti zote za klabu za kulipwa kuhakikisha wamiliki wake wanakuwa na pesa za kutosha kuendeesha klabu zao. Adhabu zao kwa timu ambayo zilikumbwa na tatizo la udhibiti zilihusisha pia zuio la kusajili, kuwapunguzia wachezaji kwenye kikosi ay hata kushushwa kwenye ligi. Kutokana na hilo, licha ya kuwa na mapato madogo, klabu za Ufaransa hazikuwa na madeni makubwa kwa kulinganisha na England, Italia na Hispania. Klabu kadhaa za Ufaransa zilikuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza faida jambo ndogo kwa miaka kadhaa, ambapo ziliwekeza zaidi katika kuendeleza wachezaji vijana kwenye akademia zao za kisasa na hapo zilipata mapato zaidi zilipoamua kuwauza wachezaji hao iliowazalisha.

Kwa mfano, kwa miaka minne hadi kufikia 2009, wachezaji waliuzwa na Lille, moja ya klabu hiyo iliyokuwa ikiuza mastaa wengi, waliingiza zaidi ya faida Euro 164 milioni.
OL Group, kampuni iliyokuwa ikifahamiika kwa jina la Olympique Lyonnais, ilitangaza faida ya Euro 5.1 milioni taslimu katika msimu wa 2008–09.

Bundesliga
Katika mwisho wa kila msimu, taratibu wa Bundesliga zilikuwa zinahitaji klabu kuomba kwenye Chama cha Soka (DFB) kupata kibali cha ushiriki wa ligi kwa mwaka unaofuata na kwamba DFB ni wao walikuwa na ruhusa ya kufuatilia taarifa zote za usajili kwenye akauti ya timu hizo ili kuondoa kama kuna hatari yoyote ya udanganyifu kwenye ishu ya usajili. Kwa timu iliyokutwa na hatia ya kufanya udanganyifu kwenye suala hilo, adhabu yake ni kutoza faini na kupokwa pointi na kwamba timu itawekwa kwenye masharti makali kwamba hawataruhusiwa kusajili mchezaji mwingine kama hawatakuwa wameuza huku gharama waliyomsajili mchezaji mpya isizidi ile ambayo walivuna kwenye mauzo ya mchezaji mwingine. Na kingine ni kwamba hakukuwa na ruhusa ya mmiliki mmoja wa klabu kumiliza zaidi ya asilimia 49 kwenye Bundesliga.

Licha ya kuwapo na uongozi bora wa kiuchumi kwenye Ligi Kuu Ujerumani, bado kuna klabu zilikumbana na wakati mgumu. Mwaka 2004, Borussia Dortmund iliripotiwa kuwa na deni la Euro 118.8 milioni. baada ya kushinda ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1997 na mataji ya Bundesliga, Dortmund ilijaribu kutengeneza mazingira ya kutafuta mafanikio kwa kufanya usajili mkubwa wa wachezaji wa kigeni kabla ya baadaye kushindwa kuwamudu vyema kwenye gharama zao. Baadaye, timu hiyo iliamua kuwekeza kwenye wachezaji wa ndani na kuzalisha wachezaji wao jambo lililoifanya timu hiyo kuwa na nguvu kiuchumi. Mwaka 2004, Hertha BSC iliripotiwa kuwa na deni la Pauni 24.7 milioni, lakini iliendelea kubaki kwenye ligi baada ya akaunti zao kuonyesha kuwa bado ina kiwango cha kutosha cha pesa.

Bayern Munich ilitengeneza faida ya Euro 2.5 milioni katika msimu wa 2008–09, wakati Schalke 04 ilipata hasara ya Euro 30.4 milioni mwaka 2009. Borussia Dortmund GmbH & Co. KGaA ilitengeneza hasara ya Euro 2.9 milioni msimu wa 2008–09.

Hali kwenye ligi nyingine
Kwenye ligi nyingine za Ulaya ikiwamo ya Ureno Primeira Liga, Eredivisie ya Uholanzi na Ligi Kuu Uskochi. Kutokana kutoka kwenye maeneo yenye idadi ndogo ya watu na uchumi mdogo, ligi hizo na hizi nyingine kama za Ubelgiji na nchi za Scandinavia zilikuwa na mapato kidogo ukilinganisha na mataifa makubwa na ndiyo maana hawakuwa na timu yoyote kwenye orodha ya klabu 20 za Deloitte. Lakini, hilo halikuzizuia klabu za Ureno kufanya vuzri kwenye michuano ya Ulaya, wakiwamo FC Porto, ambapo walibeba taji la Ulaya mara mbili msimu wa 1986–87 na 2003–04. Porto ilitengeneza mfumo wa kujitanua na kampuni za uwakala huko Amerika Kusini, ambapo ilikuwa inawasaidia kusajili wachezaji kwa pesa ndogo na kisha inakuja kuwauza kwa gharama kubwa kama ilivyotokea kwa mastaa kadhaa akiwamo James Rodriguez.

Tangu mwaka 2004, Porto iliingiza Euro 190 milioni kwenye mauzo ya wachezaji na kufidia hasara kwenye klabu yao.
Klabu tatu za Uholanzi, Ajax, PSV na Feyenoord, nazo zilifanikiwa kushinda ubingwa wa Ulaya walau mara moja. Katika miaka ya karibuni, kuliibuka na klabu nyingine kama FC Twente, wakiwa na mfumo mzuri wa kimapato kuliko kusubiri pesa za mgawo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Dili za televisheni ziliingiza faida ya Euro 64 milioni msimu wa 2007–08, lakini ilipata hasara ya Euro 90 milioni katika msimu wa 2009–10. Baada ya kuwa na wakati mzuri kwa miaka 11 kwenye michuano ya Ulaya, wakifika hadi nusu fainali mwaka 2005, PSV ilijikuta ikiingia kwenye hasara kubwa na kulazimika kuuza wachezaji wake bora kama vile Heurelho Gomes (Tottenham Hotspur), Mark van Bommel (Barcelona), Park Ji-sung (Manchester United), Johann Vogel (Milan), Alex (Chelsea) na Jan Vennegoor of Hesselink (Celtic). Kwa kuweza kupata mapato kidogo, timu hiyo ililazimika kuchukua mkopo wa Euro 10 milioni kutoka katika kampuni ya Phillips na Aprili 2012 ililazimika kuuza haki zake za uwanja wa mechi na mazoezi kwa Euro 49 milioni. Mambo kama hayo ndiyo yaliyosukuma kutoka kwa FFP ili kuziokoa klabu kutoka kwenye hatari ya kujikusanyia madeni makubwa na kujiweka pabaya.

Katika kuokoa klabu zao, mamlaka za serikali za Uholanzi ziliwekeza zaidi ya Euro 300 milioni kwenye soka kati yam waka 2006 na 2011 na kutoa mikoba kwa klabu kama FC Utrecht, FC Groningen, FC Twente, Vitesse na ADO Den Haag, licha ya jambo hilo lilidaiwa kuwa ni kosa kwenye taratibu za Umoja wa Ulaya.
Kwa ujumla wake, klabu nyingi za nchi mbalim bali za Ulaya zilikuwa kwenye changamoto kubwa ya kujisimamia kiuchumi na kujikuta zikiingia kwenye madeni makubwa kiuendaaji kabla ya kuibuka kwa kundi kubwa la wawekezaji binafsi, ambao walikuja kutibua zaidi kwa kutumia pesa za biashara zao nyingine kwenye mchezo wa soka na hivyo kuwafanya Uefa kuja na mpango huo wa FFP ili kudhibiti usawa kwenye matumizi ya klabu hizo kwa maana ya matumizi yasizidi kipato.
Je, Financial Fair Play Rule ina mambo gani ya msingi katika utekelezaji wake? Itaendelea kesho.