Sheria mpya tatu za Jose Mourinho Real Madrid
Muktasari:
- Msimu uliopita hali ya nidhamu ilishuka zaidi kiasi kwamba mastaa wa timu hiyo walikuwa wakiamua lolote wanalotaka kufanya ikiwamo kufika au kutofika mazoezini ama kuchelewa, kujibizana na kocha au wasaidizi wake na hata kurushia maneno wao kwa wao, huku wakifikia hatua ya kuzichapa ambapo Aurelien Tchouameni na Federico Valverde walizipiga lakini wakaishia kutozwa faini na uongozi ya Pauni 500,000 kila mmoja.
MADRID, HISPANIA: KOCHA mpya wa Real Madrid, Jose Mourinho ameanzisha sheria mpya tatu ili kuimarisha nidhamu, ambapo zitamgusa kila mtu aliyepo kwenye kikosi hicho wakiwamo wasaidizi wake wa benchi la ufundi, ingawa zaidi zinawalenga wachezaji.
Taarifa zinaeleza kwamba Mourinho hajapoteza muda kuanza kuonyesha msimamo wake mpya ndani ya kikosi hicho ambacho misimu miwili iliyopita kilionekana kushuka kiwango kutokana na kile kilichoelezwa kwamba ni udhaifu wa usimamizi wa nidhamu kutoka kwa watangulizi wake, Xabi Alonso na Alvaro Albeloa, ambao wakati flani waliwahi kuitumikia timu hiyo miaka ya nyuma.
Msimu uliopita hali ya nidhamu ilishuka zaidi kiasi kwamba mastaa wa timu hiyo walikuwa wakiamua lolote wanalotaka kufanya ikiwamo kufika au kutofika mazoezini ama kuchelewa, kujibizana na kocha au wasaidizi wake na hata kurushia maneno wao kwa wao, huku wakifikia hatua ya kuzichapa ambapo Aurelien Tchouameni na Federico Valverde walizipiga lakini wakaishia kutozwa faini na uongozi ya Pauni 500,000 kila mmoja.
Na kutokana na matukio hayo, uongozi chini rais Florentino Perez uliamua kumchukua Mourinho kutoka Benfica ili kurejeshe nidhamu, suala ambalo ameshaanza kulifanyia kazi.
Kwa mujibu wa AS, taarifa kutoka klabuni hapo zinaeleza kuwa kocha huyo maarufu ambaye aliwahi kuzifundisha Manchester United, Chelsea na Tottenham Hotspur anapambana kuhakikisha nidhamu na utulivu katika chumba cha kubadilishia nguo vinazingatiwa na hataangalia sura wala cheo kwa watu wake.
Katika jukumu la kusimamia kundi lenye mastaa kama Kylian Mbappe, Jude Bellingham na Vinicius Junior ambaye wiki hii alikubaliana mkataba mpya wa miaka sita na klabu hiyo, Mourinho ameripotiwa kuelekeza nguvu zake katika maeneo matatu muhimu; lishe, muda na uponaji majeraha, ambapo ameanzisha taratibu mpya.
Chakula kinasimamiwa na klabu; wachezaji sasa wanaelekezwa chakula wanachopaswa kula kila siku ni kutoka kwa mtaalamu wa lishe wa klabu.
Mtaalamu huyo ambaye awali alikuwa akitoa ushauri tu, sasa amepewa jukumu la kuandaa menyu za kila mlo, ikiwamo kifungua kinywa na hata vitafunwa vya mchana. Kabla ya Mourinho kuwasili, wachezaji walikuwa na uhuru zaidi katika uchaguzi wa chakula na lishe. Lakini, The special One anataka mfumo wa chakula wa klabu uzingatie utendaji wa uwanjani badala ya matakwa binafsi ya kila mchezaji.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, licha ya kupoteza uhuru wao katika kuchagua baadhi ya vyakula, wachezaji wamepokea mabadiliko hayo kwa mtazamo chanya.
Sheria ya pili ni uchelewaji, ambayo imetungiwa kanuni na kuna adhabu tofauti, ambapo amebadilisha namna wachezaji watakavyoadhibiwa wanapochelewa mazoezini au kwenye mikutano katika kituo cha mazoezi cha Valdebebas.
Awali, mchezaji aliyekuwa akichelewa alitozwa faini ya fedha, lakini kuanzia sasa anayefika kwa kuchelewa atalazimika kufanya mazoezi mbali na kikosi, akiwa peke yake katika ukumbi wa mazoezi. Mourinho anataka wachezaji wafike kituoni hapo saa moja kabla ya muda wa kuanza mazoezi na ameweka wazi kwamba yeyote atakayekiuka sheria hiyo ataadhibiwa bila kujali hadhi, nafasi au ukubwa wake ndani ya timu.
Sheria ya tatu itazingatia matibabu ya majeraha akitaka yafanyike Valdebebas, aliyoagiza kwamba vipindi vyote vya kupona na programu za kurejea uwanjani vifanyike katika kituo cha mazoezi cha Real Madrid, Valdebebas bada ya kila mmoja akaponea akiwa nchi au eneo alipendalo.
Lengo la Mourinho ni kufanya mchakato wa kurejea baada ya majeraha kuwa jukumu la pamoja badala ya kila mchezaji kushughulikia kwa njia yake, na amepiga marufuku matibabu ya nje ya klabu akiagiza kwamba kila taarifa na hatua ya kitabibu kuhusu mchezaji aliye majeruhi iratibiwe kupitia klabu na timu yake ya wataalamu.
Real Madrid, ambayo ilimaliza msimu uliopita ikiwa nyuma ya mahasimu wao Barcelona kwa tofauti ya pointi 12 katika mbio za ubingwa wa LaLiga, itaanza kampeniya msimu mpya kwa kucheza ugenini dhidi ya Espanyol Agosti 22.