Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dalali: Nilisimika bendera ya Simba makao makuu ya Yanga

DALALI Pict

KATIKA sehemu ya kwanza ya mahojiano na mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali alizungumzia mambo mbalimbali kuhusu klabu hiyo, huku akimpongeza mwekezaji Mohammed Dewji ‘Mo’ kwa kuendelea kutoa fedha zinazosaidia uendeshaji wa kikosi hicho.

Pia, aligusia namna klabu hiyo inavyopaswa kujiendesha na historia mbalimbali zinazohusu chama hilo ambalo jana liliadhimisha miaka 90 katika  tamasha la Simba Day.

Leo, Dalali anazungumzia mambo kadhaa yanayoihusu Simba. Twende pamoja!

DALA 02

MATUKIO MAGUMU

Anasema mwaka 1975, Simba ilipoteza kwa Yanga bao 1-0 katika fainali za Afrika Mashariki, matokeo yaliyomuathiri sana shabiki mmoja aliyemtaja kwa jina la Malenda hadi kufikia hatua ya kujiua.

“Fainali hizo zilipigwa Zanzibar. Malenda alikuwa akifanya kazi katika kiwanda cha nyuzi. Katika kiwanda hicho kulikuwa na mapipa ya maji ya moto yaliyokuwa yakitumika kuchuja nyuzi. Alijitumbukiza humo na kufariki kifo kibaya sana,” anasema na kuongeza:

“Lilikuwa tukio la kuumiza ambalo liliacha simanzi kubwa kwa Wanasimba na familia kwa jumla. Tukio lingine lililoniumiza nililiona katika gazeti la Mwananchi, la mtoto wa miaka tisa, Joshua, aliyejinyonga miaka miwili iliyopita baada ya Simba kufungwa bao 1-0 na Yanga. Ndiyo maana najitoa kwa kila hali kuhakikisha Simba inafanya vizuri.”

DALA 03

BENDERA YA SIMBA JANGWANI

Anasimulia tukio lingine la aina yake alilowahi kufanya wakati wa ushindani wa jadi kati ya Simba na Yanga.

“Kuna mwaka nilikwenda kwenye klabu ya Yanga usiku. Nilikuwa nimevalia baibui, nikawakuta wazee wakiwa wanakunywa kahawa. Nikapanda hadi juu ya jengo lao na kufunga bendera ya Simba ikaendelea kupepea. Asubuhi walipoiona walianza kushangaa na kudhani ni uchawi, kumbe nilikuwa nawachezea akili tu,” anasema.

Anaongeza: “Nilifanya hivyo kwa sababu mbele yetu kulikuwa na mechi na tukashinda. Walianza kutumia muda mwingi kuhangaika na ile bendera badala ya kuweka nguvu kwenye timu yao.”

DALA 04

AHMED, KAMWE

Anawashauri Ahmed Ally, msemaji wa Simba, na Ally Kamwe, msemaji wa Yanga, kutambua nguvu waliyonayo kwa kuwa wanaweza kujenga au kubomoa.

“Wajitahidi kuwaleta watu pamoja. Mpira wa miguu ni furaha na amani, ndiyo maana unawakutanisha watu. Wapunguze mambo yanayokuwa ya kibinafsi na wajenge nidhamu katika jamii. Wajue utani wa jadi siyo uadui, bali ni undugu,” anasema.

DALA 05

‘YANGA BINGWA’ YAMSHTUA

Alipoulizwa kuhusu mafanikio ya Yanga kutwaa ubingwa mara tano mfululizo, anaona hali hiyo imetokana na uwekezaji unaofanywa na klabu hiyo pamoja na namna inavyodhaminiwa.

“Mfano Mo Dewji adhamini timu 10, unategemea nini kitatokea? Naiomba Serikali iingilie kati pamoja na TFF, hili si jambo la kufumbia macho. Ndiyo maana viongozi wa Yanga wanapoulizwa kuhusu ushindani wa ligi, wanasema Yanga ni bingwa kabla haijawa bingwa, kwa sababu wanajua wanachokifanya. Viongozi wa Simba wasilinyamazie suala hili,” anasema.

Mbali na hilo, alipoulizwa kama angepewa nafasi ya kumsajili mchezaji mmoja kutoka Yanga, angemchukua nani, alisema:

“Tangu zamani Yanga ndiyo tulikuwa tunawapa wachezaji. Mfano kuna marehemu Alphonce Modest. Hivyo naamini Simba ni klabu yenye jicho la kuona vipaji. Ndiyo maana mchezaji anayehusishwa na Simba, mtani wetu anakimbilia kumsajili kwa sababu anajua hatuna kazi mbovu.”

DALA 06

ALIMGOMEA KAWAWA

Waziri Mkuu wa zamani, hayati Rashid Mfaume Kawawa aliwahi kumuita ofisini kwake na kumwambia Athuman Idd Chuji anatakiwa kwenda Yanga ili aweze kuitwa katika timu ya taifa, Taifa Stars.

“Kawawa alikuwa Simba, mimi ndiye niliyempa kadi ya uanachama. Nikamjibu, kiongozi, kwa nini akicheza Simba hawezi kuichezea Taifa Stars? Akasema kocha mkuu Marcio Maximo ndiye aliyetaka hivyo. Nikamwambia haiwezekani,” anasimulia.

“Akasema unapata wapi ujasiri wa kubishana na mimi? Nenda nje, fikiria halafu rudi unipe jibu.”

Anaongeza: “Nilipotoka nje aliniita tena. Kabla sijamjibu nilimwomba kumuuliza swali ambalo kama angenijibu vizuri ningekubaliana naye. Nikamuuliza, je unaweza kuhama CCM na kwenda CUF ili ugombee urais wa nchi? Akajibu kamwe haiwezi kutokea.”

“Baada ya hapo nikamwambia, wewe ni Simba unawapaje silaha watani wako? Akasema nimekuelewa, mwambie Chuji aendelee na kazi.”

Anaongeza baadaye walikumbana na changamoto nyingine kutoka TFF.

“Ajabu tukakutana na zengwe lingine TFF. Wakasema usajili wa Chuji kuwepo Simba ni batili, hivyo anatakiwa kwenda Yanga. Ikabidi aende, sikuwa na namna ya kufanya.”

DALA 07

AIOMBA TFF

Dalali anaiomba TFF na viongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania kutazama upya baadhi ya kanuni mpya kwa maslahi ya ushindani wa soka.

“Nimeziona kanuni mpya, lakini kwa faida ya uhai na ushindani wa mpira wa miguu, namuomba Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania, Wallace Karia, pamoja na viongozi wa Bodi ya Ligi Tanzania, waangalie upya suala la timu kupokwa pointi tano.”

“Pointi zipokwe kwenye mechi husika, siyo za nyuma. Ikitokea timu imefungwa, basi ije inyang’anywe pointi tatu katika mechi inayofuata. Kwa mtazamo wangu hilo halijakaa vizuri, hivyo marekebisho yakija walifanyie kazi,” anasema.

DALA 08

HAJAFAIDIKA?

Pamoja na urithi kubwa aliouacha Simba, ambayo sasa inaingiza mabilioni ya fedha, Dalali anaweka wazi hakunufaika kifedha kutokana na uongozi wake.

“Simba ilikuwa kwanza, mimi baadaye. Huwezi kuamini kipindi hicho nilipokuwa naongoza nilikuwa nauza hadi friji au vitu vya ndani kuhakikisha mahitaji yanapatikana kwa wachezaji.”

“Nilikuwa nalala sehemu ya wachezaji, nilikula chakula cha wachezaji. Ndiyo maana walikuwa na moyo wa kujitoa kwa sababu waliona namna nilivyokuwa najitoa kwa ajili yao.”

“Unaweza kuwauliza kina Emmanuel Gabriel, Mussa Mgosi, Haruna Moshi ‘Boban’, Kelvin Yondani, Juma Kaseja na wengine, watakwambia ndiyo maana hadi sasa wananipenda na kuniona kama baba.”

Anasema wakati huo mchezaji aliyekuwa ghali zaidi alikuwa Juma Kaseja.

“Kaseja alikuwa analipwa pesa ndefu, ingawa siwezi kutaja kiasi hicho kwa sababu ilikuwa siri yake na klabu.”

Alipoulizwa kuhusu usafiri anaotumia, anasema: “Ukiacha magari binafsi ya watu wengine, napanda daladala. Wengi wanashangazwa hilo kutokana na jina langu kubwa, lakini mimi ninaishi uhalisia. Hata hivyo, kuna watu wakiniona nina safari hunikatia tiketi za ndege.”

Alipoulizwa kama angepewa zawadi kutokana na kuanzisha tamasha la Simba Day ambalo limekuwa likinufaisha hata timu nyingine, alisema: “Siwezi kumpangia mtu kitu cha kunifanyia. Kikubwa legasi yangu inaishi na hilo linanifariji.”

DALA 10

KWA SASA NI NANI?

Kwa sasa anasema ni mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano inayolenga kuondoa migogoro ndani ya klabu.

“Tupo viongozi watano. Kuna Ostadhi Juma ambaye ni mratibu, Ramadhan Hamisi ni katibu, huku wajumbe wakiwa Hamad Haruna na Makoye.”

Anasema amekuwa akisafiri sehemu mbalimbali kuhakikisha umoja unapatikana ndani ya Simba.

“Nimesafiri sana kwenda kusuluhisha changamoto Mbeya na Zanzibar, ambako tayari nimeanzisha matawi matano ya wanachama wa Simba. Lengo ni kuhakikisha tunakuwa wamoja na kufanya maendeleo kwa pamoja.”