Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simba Day 2026, vaibu la miaka 90

VAIBU Pict

Muktasari:

  • Ni tamasha ambalo Simba imekuwa ikilifanya kila mwaka tangu 2009, likiwa maalum kwa ajili ya kutambulisha kikosi cha msimu kinachokwenda kushiriki mashindano mbalimbali. Huu ni mwaka wa 18 linakwenda kufanyika.

MIAKA 90 ya klabu ya Simba inaadhimishwa leo Jumamosi Agosti 8, 2026 katika kilele cha Simba Day, tamasha litakalofanyika kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam huku likitarajiwa kuwapo kwa vaibu la kutosha kutoka kwa mashabiki wa timu hiyo.

Ni tamasha ambalo Simba imekuwa ikilifanya kila mwaka tangu 2009, likiwa maalum kwa ajili ya kutambulisha kikosi cha msimu kinachokwenda kushiriki mashindano mbalimbali. Huu ni mwaka wa 18 linakwenda kufanyika.

Mbali na burudani zingine zote zitakazofanyika, kilele chake kitahitimishwa kwa mechi ya kirafiki ya kimataifa ambapo Simba itacheza dhidi ya Kenya Police.

Hii itakuwa mara ya nne Simba kucheza dhidi ya timu kutoka Kenya kwenye Simba Day baada ya Nairobi City Stars (2012), AFC Leopards (2016) na Gor Mahia FC (2025). Kati ya mechi hizo tatu zilizopita, Simba imepoteza moja dhidi ya Nairobi City Stars kwa mabao 3-1, huku ikizifunga AFC Leopards (4-0) na Gor Mahia FC (2-0).

VAIB 01

Kwa ujumla, Simba imeshinda mechi 11 za Simba Day kati ya 17 ilizocheza tangu 2009, sare mbili na kupoteza nne. Ushindi mkubwa ulipatikana 2020 iliposhinda 6-0 dhidi ya Vital’O ya Burundi.

Matokeo ya mechi 17 zilizopita Simba Day yalikuwa hivi; Simba 1-0 SC Villa (2009), Simba 0-0 Express (2010), Simba 0-1 Victors FC (2011), Simba 1-3 Nairobi City Stars (2012), Simba 4-1 SC Villa (2013), Simba 0-3 ZESCO FC (2014), Simba 1-0 SC Villa (2015), Simba 4-0 AFC Leopards (2016) na Simba 1-0 Rayon Sports (2017).

Matokeo mengine ni; Simba 1-1 Asante Kotoko (2018), Simba 3-1 Power Dynamos (2019), Simba 6-0 Vital’O FC (2020), Simba 0-1 TP Mazembe (2021), Simba 2-0 St George (2022), Simba 2-0 Power Dynamos (2023), Simba 2-0 APR FC (2024) na Simba 2-0 Gor Mahia FC (2025).

Kocha Mkuu wa Simba SC, Steve Barker, ameweka wazi shauku yake kuelekea kilele cha tamasha la Simba Day, akisema kwake itakuwa ni uzoefu mpya ambao hajawahi kuupata tangu aanze majukumu yake ndani ya kikosi hicho.

Barker, ambaye anaonekana kuvutiwa na mazingira ya soka la Tanzania, amesema amekuwa akisikia sifa za Simba Day lakini hajawahi kuishuhudia, hivyo anasubiri kwa hamu kuona kile ambacho mashabiki wa Mnyama wamekiandaa.

VAIB 02

MIAKA 90 YA HISTORIA

Akizungumza na waandishi wa habari, Barker alikumbusha kuwa mwaka huu ni wa kipekee kwa klabu hiyo kwani inatimiza miaka 90 tangu kuanzishwa kwake. Alibainisha kuwa leo itakuwa ni siku ya mashabiki kusherehekea ukubwa wa klabu yao, ambayo aliitaja kuwa moja ya klabu bora zaidi katika bara la Afrika.

“Ni siku ya mashabiki. Ni siku ya Simba kusherehekea sisi ni nani. Tunatimiza miaka 90 mwaka huu kama klabu ya mpira, tunatazamia kuwaburudisha mashabiki wetu,” amesema Barker akionyesha kujiamini.

Barker hakuishia hapo, aliwamwagia sifa lukuki mashabiki wa Simba akisema kuwa hana shaka kuwa ndio mashabiki bora zaidi barani Afrika kutokana na namna wanavyoipenda na kuivaa timu yao popote wanapopita.

“Passion’ yao, namna wanavyosapoti timu na idadi yao inayojitokeza inavutia, inapendeza sana kuendesha gari mitaani na kuona kila mtu wa pili amevaa jezi ya Simba,” ameongeza kocha huyo.

VAIB 03

MZIKI MPYA NA KUREJEA KWA NEO MAEMA

Kuhusu hali ya kikosi, Barker amesema timu imerejea kutoka nchini Rwanda ikiwa katika hali nzuri na wachezaji wapya wameanza kuzoea mfumo vizuri. Amesema kila siku imekuwa bora kwa timu hiyo inayojiandaa na msimu mpya.

Habari njema zaidi kwa mashabiki wa Simba ni kurejea kwa Neo Maema, ambapo Barker alieleza kufurahishwa kwake kumuona mchezaji huyo ndani ya basi la timu asubuhi ya jana baada ya mchakato wa usajili wake kukamilika.

“Nilifurahi sana asubuhi ya leo (jana) kumuona Neo Maema kwenye basi, ilichukua muda kukamilisha hilo, lakini nina furaha yuko nasi,” amesisitiza Barker.

Maema amerejea Simba kwa kipindi kingine cha kuitumikia timu hiyo baada ya msimu uliopita kucheza kwa mkopo akitokea Mamelodi Sundowns.

Mbali na Maema, kuna nyota wapya ambao wanakwenda kushiriki Simba Day kwa mara ya kwanza. Wapya kabisa ni Nathaniel Chilambo, Kelvin Nashon, Bakari Msimu, Keletso Makgalwa, Ibrahim Doumbia na Ibraheem Jabaar waliosajiliwa hivi karibuni.

Wengine ni Baraka Mwangosi, Inno Jospin Loemba, Alain Anicet Oura, Libasse Gueye na Ismael Olivier Toure ambao waliingia dirisha dogo msimu uliopita wakiikosa Simba Day ya 2025. Chama ambaye naye aliingia dirisha dogo, ni mwenyeji ndani ya Simba akishiriki Simba Day ya kwanza mwaka 2018 alipotua klabuni hapo akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia.

Akaondoka 2021 kwenda RS Berkane, akarejea Simba 2022, kisha 2024 akatua Yanga msimu mmoja, 2025 akasajiliwa Singida Black Stars, ndipo dirisha dogo la msimu wa 2025-2026 akarejea Simba.

Baada ya sherehe za Simba Day, Barker amesema kuanzia wiki ijayo akili zote zitahamia kwenye ufunguzi wa msimu wa 2026-2027 ambapo watashuka dimbani kuwania Ngao ya Jamii dhidi ya Yanga.

Kocha huyo amewahakikishia mashabiki kuwa maandalizi yameenda vizuri na wako tayari kupambana kurejesha heshima ya klabu hiyo yenye historia ndefu nchini.

VAIB 04

MSIKIE DUCHU

Beki wa kulia wa Simba, David Kameta ‘Duchu’, akizungumza kwa niaba ya wachezaji, amewataka mashabiki wa klabu hiyo kujitokeza kwa wingi katika kilele cha tamasha la Simba Day, akisisitiza wachezaji wako tayari kutoa burudani baada ya kukamilisha maandalizi yao.

Duchu ameeleza kuwa siku hiyo ni maalum kwa ajili ya mashabiki kufurahi na kupata nafasi ya kipekee ya kuwaona wachezaji wapya waliosajiliwa kwa ajili ya msimu ujao wa mashindano.

“Sisi kama wachezaji kusema ukweli tunatambua umuhimu wa siku ya kesho (leo) ni siku ya ya kufurahi, ni siku ya mashabiki kuja kufurahi na kuja kuwaona wachezaji wapya. Lakini sisi kama wachezaji tuko tayari, ukiangalia tumefanya maandalizi yetu yaliyo mema,” amesema Duchu akionyesha kujiamini.

Duchu, ambaye amekuwa ndani ya kikosi cha Mnyama kwa takriban miaka minne, ameongeza kuwa Simba Day ni tamasha kubwa ambalo mchezaji yeyote mwenye malengo ya kuwa mkubwa katika soka la Afrika anatamani kushiriki.

“Ni tamasha kubwa ambalo kwa mchezaji yeyote ambaye unataka kuwa mkubwa unatamani kuwepo na unatakiwa kucheza, nadhani leo itakuwa ni siku ya furaha kwetu na kuenjoy na kufurahia mpira,” amesisitiza beki huyo.